MTANZANIA
Kwa vijana wa mjini, wanaweza kusema kwamba alichofanya Dk. Willibrod Slaa juzi kwa kuachana na siasa na kurusha tuhuma kwa chama chake, ni sawa na kumwaga ugali, na majibu aliyotoa mkewe wa kwanza, Rose Kamili jana, ni sawa na kumwaga mboga.
Mke huyo aliyedai kutelekezwa na Dk. Slaa mwaka 2010 pamoja na watoto, alisema kiongozi huyo ni mwongo na ni dhaifu kwa wanawake.
Rose alisema ameshtushwa na kauli zilizotolewa na Dk. Slaa, na hasa zile zilizoelekezwa kwake moja kwa moja na familia yake.
Rose ambaye ni mke wa ndoa wa kiongozi huyo wa zamani wa Chadema, alisema kauli Dk. Slaa kuwa familia yake imekuwa ikishindia mihogo kwa sababu ya kuhangaikia na Chadema, ni kiashiria cha uongo wa wazi.
“Siwezi kusema kwamba mihogo ni mibaya kuliwa, lakini napenda kukiri kwamba katika maisha yetu niliyokaa na Dk. Slaa kuanzia mwaka 1986, sikuwahi kushuhudia familia yetu ikila mihogo kwa sababu ya kukosa chakula kama alivyosema kwenye hotuba yake,” .
Aliongeza kuwa hata kauli yake kwamba Serikali ilimwekea pingamizi ili asifunge ndoa na mchumba aliye naye sasa, Josephine Mushumbusi, ni uongo kwani ni yeye ndiye aliyeweka pingamizi hilo kwa sababu ni mkewe rasmi wa ndoa.
“Jambo la kujiuliza hapa ni kwamba tangu lini Serikali ikaweka pingamizi wakati aliyepinga ni mkewe. Ukweli ni kwamba mimi ndiye niliyeweka pingamizi hilo ili kunusuru kunyang’anywa nyumba na hatimaye kuhangaika na watoto,”.
Kuhusu kauli ya Dk. Slaa kwamba anamchukia Lowassa na hajazungumza naye kwa muda mrefu, Rose alisema waziri mkuu huyo wa zamani, ndiye aliyemshauri kuhamia Chadema mwaka 1995 na kugombea ubunge wa Karatu baada ya jina lake kukatwa na Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM.
“Nakumbuka wakati tukizungumzia suala hilo ilikuwa jioni na tulikwenda nyumbani kwa Lowassa, Monduli baada ya jina lake kukatwa na CCM, ndiyo akamshauri kuhamia chama kingine, sasa hizo chuki zinatoka wapi?” alisema na kuhoji.
Kuhusu Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Rose alisema pia ni uongo mwingine kwa sababu wawili hao walipigiana simu na kufanya mazungumzo wiki iliyopita.
“Kwanini aonyeshe chuki na watu wakati sisi ametutelekeza kwa muda mrefu, lakini tumekuwa tukimlinda? Sasa inashangaza ni kwa nini padri huyu mstaafu anaonyesha chuki kwa wengine,”.
Aidha Rose pia alionyesha kusikitikia hatua ya mumewe kuzusha maneno ya uongo kwa viongozi wa dini, akiwatuhumu kuhongwa zaidi ya shilingi milioni 60 na Lowassa ili wamuunge mkono.
Pia alisema kumuhusisha Mchungaji Josephat Gwajima wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, kwamba ndiye alimleta Lowassa Chadema ni kichekesho kwa sababu muunganishaji mkubwa wa suala hilo ni yeye (Dk. Slaa) ambaye anasali katika kanisa hilo.
Uongo mwingine alioutaja mkewe huyo wa ndoa ni kuhusu kukataa kwake kutojiandaa kuwania urais kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), wakati inajulikana kuwa alikuwa akifanya maandalizi ndani na nje ya nchi kwa ajili ya suala hilo.
MTANZANIA
Jeshi la Polisi mkoani Arusha linamshikilia mwanafunzi wa mwaka wa tano wa masomo ya falsafa katika Chuo cha Dini cha Kanisa Katoliki kilichopo Segerea, Dar es Salaam kwa tuhuma za mauaji.
Elijus Lyatuu, anashikiliwa kwa tuhuma za kumuua Alfred Kimbaa maarufu kwa jina la Mandela mwanzoni mwa wiki katika Hoteli ya A Square Belmont katikati ya Jiji la Arusha.
Mtuhumiwa huyo anadaiwa alimuua Kimbaa usiku wa kuamkia Jumatatu katika hoteli hiyo na kuchukua baadhi ya viungo vyake vya mwili kikiwamo kichwa, sehemu za siri, matiti na viganja vya mikono.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa Septemba mosi mwaka huu katika barabara ya Makongoro eneo la TRA jirani na Kituo Kikuu cha Polisi Arusha.
Kamanda Sabas alisema upelelezi uliofanywa na jeshi hilo uliwezesha kumkamata Lyatuu ambaye aliwasili jijini Arusha wiki mbili zilizopita na kufikia nyumbani kwa Kimbaa eneo la Mianzini na walikuwa wanaishi chumba kimoja ila ilitokea sintofahamu kati yao kiasi cha kushindwa kuelewana.
Alisema viungo vya mwili wa marehemu vimepatikana katika eneo la Mto Misheni, Usa River, baada ya mtuhumiwa huyo kuhojiwa na polisi na kuwapeleka katika eneo hilo alikokuwa ameviweka.
Kamanda Sabas alisema siku ya tukio Lyatuu na Kimbaa walikuwa hotelini hapo ili kusuluhisha tofauti zao, lakini wakashindwa kuafikiana na ndipo mtuhumiwa akamuua mwenzake.
“Mtuhumiwa alifika Arusha wiki mbili zilizopita na akawa amefikia nyumbani kwa Kimbaa kwa vile ni watu wanaofahamiana ikizingatiwa mtuhumiwa ni ndugu wa mmiliki wa duka alilokuwa akifanya kazi Kimbaa na wakawa wanaishi chumba kimoja.
“Lakini kulitokea kutokuelewana kati yao na katika kutokuelewana huko ndipo mtuhumiwa akafikia hatua ya kumuua mwenzake,” alisema Kamanda Sabas na kuongeza:
“Pamoja na kukamatwa kwa mtuhumiwa, pia kumeweza kupatikana vielelezo vyote, yaani viungo vya marehemu baada ya mtuhumiwa kuwapeleka polisi kule alipovitupa Mto Misheni…upelelezi unakamilika ili mtuhumiwa afikishwe mahakamani kujibu tuhuma za mauaji zinazomkabili.”
Kamanda Sabas alipoulizwa kuhusu chanzo cha Kimbaa na Lyatuu kutokuelewana, hakuwa tayari kuzungumzia mgogoro kati yao, akisema kuwa mambo mengine yataenda kujulikana mahakamani mtuhumiwa huyo atakapopelekwa kujibu mashtaka yanayomkabili.
Inadaiwa kuwa chanzo cha sintofahamu kati ya Kimbaa na mtuhumiwa huyo ni fedha. Inaelezwa kuwa mtuhumiwa kabla ya kufanya mauaji hayo aliachiwa ufunguo wa duka hilo na Mandela na baada ya kurudi dukani alikuta zaidi ya Sh milioni 10 zikiwa hazipo.
NIPASHE
Jinamizi la kukimbiwa na wanachama limezidi kukiandama Chama Cha Mapinduzi, baada ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM) Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro, Beatrce Shirima, kujiuzulu wadhifa wake baada ya kutuhumiwa ana muunga mkono mgombea urais aliyesimamishwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kupitia Chadema, Edward Lowassa.
Beatrice amefikia uamuzi huo ikiwa ni siku chache baada ya Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Kilimanjaro, Fredy Mushi na Katibu wa Uchumi na Fedha wa CCM mkoani hapa, Paul Matemu kujiunga na Chadema.
Akitangaza uamuzi huo jana, Beatrice alisema kwa kipindi kirefu amekuwa akinyimwa ushirikiano kutoka kwa viongozi wa CCM kutokana na kile anachodaiwa kuwa, yeye ni mmoja wa waliokuwa wanamuunga mkono Lowassa.
“Nadaiwa kwamba nina kisaliti chama na kuwasaidia Ukawa katika kampeni zao. Siyo jambo la kweli na sijawahi kuhusika katika kuwapigia kampeni Chadema,” .
Alisema ameamua kujiuzulu nafasi hiyo na kujivua uanachama wa CCM bila ya kushinikizwa na mtu yeyote, kwa kuwa ni maamuzi yake binafsi.
“Nimeamua kujiweka pembeni na nimejitoa CCM; mimi sio kiongozi tena wa vijana na maamuzi haya sijashauriwa na mtu yeyote bali ni maamuzi yangu binafsi” alisema.
NIPASHE
Mgombea Ubunge Jimbo la Ubungo kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Didas Masaburi, amekanusha taarifa za kufadhili vijana wanaodaiwa kuandamana wakipinga aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADCEMA) kuondoka ndani ya chama hicho.
Dk. Masaburi alikanusha taarifa hizo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusiana na uvumi uliozagaa kwenye mitandao ya jamii kuwa vijana 10 wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi kwa sababu ya kuandamana bila ya kibali wakimtaka Dk. Slaa asiondoke kwenye chama hicho walitumwa na yeye.
“Tuhuma hizo si za kweli, hata kama ninaunga mkono hoja zilizotolewa na Dk. Slaa kuhusiana na tuhuma za ufisadi dhidi ya viongozi waliohamia Chadema kutoka CCM, lakini siwezi kufadhili maandamano ya wanachama wa Chadema ya kushinikiza kubakia kwa Dk. Slaa ndani ya chama hicho,” alisema.
Alisema vijana aliowapokea katika ofisi ya CCM Jimbo la Ubungo zilizoko Manzese juzi baada ya kurudisha kadi za vyama vyao kikiwamo cha Chadema walifanya hivyo kwa mapenzi yao wakisema wamechoshwa na hadaa katika vyama walivyotoka.
Aidha, Dk. Masaburi aliwataka viongozi wa Chadema kujibu hoja zilizotolewa na Dk. Slaa badala ya kutafuta mchawi baada ya kuona amewaumbua na wanachama wao wanakihama chama hicho.
Wakati huohuo, Jeshi la Polisi mkoa wa Kinondoni, jijini Dar es Salaam limesema linaendelea na upelelezi ili kubaini vijana walioandamana juzi eneo la Morocco, jijini humo iwapo ni wanachama wa Chadema au la.
Juzi vijana takribani 100 wanaodaiwa kuwa wanachama wa Chadema waliandamana katika eneo hilo wakishinikiza kurudi katika chama hicho kwa aliyekuwa katibu mkuu wake, Dk. Willibrod Slaa, ambaye alitangaza kujitoa na kujitenga na siasa, huku akimtuhumu mgombea urais wa chama hicho, Edward Lowassa, masuala mbalimbali ua ufisadi.
Kamanda wa Polisi wa kanda ya Kinondoni, Camilius Wambura kupita msaidizi wake, jana aliliambia Nipashe kuwa bado wanawashikilia vijana 10 kati ya 100 ambao walitawanywa kwa mabomu ya machozi baada ya kukaidi amri ya jeshi hilo ya kutakiwa kutawanyika, huku wakiendelea na upelelezi kubaini wanatoka chama gani.
NIPASHE
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Maxmillan Lyimo, amesema akipata ridhaa ya kuwaongoza Watanzania katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, atahakikisha makundi yote ya jamii yanapewa mikopo ambayo itafuta machungu ya ukosefu wa ajira.
Lyimo atoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na wakazi wa Mwika, Jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro, ikiwa ni siku ya tano, tangu TLP ilipozindua kampeni za mgombea urais wa chama hicho.
“Nataka nimalize kabisa tatizo la ajira ambalo linaitesa nchi yetu kwa miaka 52 sasa; mkinipa ridhaa ya kuunda serikali ya awamu ya tano, nitaweka utaratibu wa kuyawezesha makundi yote kupata mikopo, kuanzia ngazi ya vijiji, sera hii inatekelezeka kwangu na siyo CCM inayowadanganya itawapa milioni 50,”alisema mgombea huyo.
Alisema katika suala la elimu, atafanya mabadiliko makubwa, kwa kufuta mfumo wa kibaguzi uliopo hivi sasa ambao unatoa fursa ya kuwagawa Watanzania kwa makundi ya watoto wa matajiri na masikini, katika kupata elimu bora.
Lyimo ni miongoni mwa wagombea wanane ambao wamejitokeza kuwania nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Wagombea wengine wa kiti hicho ni Dk. John Magufuli (CCM), Anna Mgwira (ACT-Wazalendo), Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowasa ambaye anapeperusha bendera ya vyama vinavyounda Ukawa, kupitia Chadema; Chief Lutalosa Yemba (ADC), Janken Kasambala (N.R.A) na Hashim Rungwe (Chaumma).
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Taifa wa TLP na mgombea ubunge wa Jimbo la Vunjo, Augustino Mrema, alirejea kauli yake ya muda mrefu kwamba, bado ana nguvu ya kushughulikia changamoto na kero za jimbo hilo, hivyo ana kila sababu ya kuchaguliwa ili azitafutie ufumbuzi wa kudumu.
“Mimi nazijua siasa za upinzani, kuliko mtu mwingine yeyote na ndio maana wananiogopa wakisema eti mimi ni CCM ‘B’ sasa hebu rudisheni mioyo yenu mkanichague ili niendelee kusaidia miradi ya maendeleo pamoja na kutatua kero zinazowakabili wananchi wangu,”Mrema.
HABARILEO
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeishtaki polisi Kanisa la Ufufuo na Uzima, linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima kutokana na kuharibu miundombinu ya umeme katika maeneo ya shirika hilo Jumamosi iliyopita na kusababisha umeme kukatika kwa baadhi ya mikoa na Jiji la Dar es Salaam.
Kutokana na kukatika kwa umeme kwa muda huo, shirika limepata hasara ya zaidi ya Sh milioni 30 ambayo ni mapato kama kungekuwepo umeme mbali na usumbufu mwingine wlaiopata kama kuwasha mitambo upya.
Meneja Uhusiano wa Tanesco, Adrian Severin alisema shirika hilo limefungua jalada namba 4397/2015 dhidi ya kanisa hilo katika Kituo cha Polisi Kimara katika Manispaa ya Kinondoni kwa sababu hiyo.
Severin alisema kuwa Agosti 29, mwaka huu kuanzia saa tisa alasiri hadi saa 12 jioni, umeme ulikatika katika Jiji la Dar es Salaam na mikoa iliyoungwanishwa katika gridi ya Taifa.
Alisema baada ya uchunguzi wa kina waligundua chanzo cha kuzimika umeme siku hiyo ilikuwa ni hitilafu ya umeme iliyotokea eneo la Ubungo Chai Bora kwenye kanisa hilo la Askofu Gwajima.
“Watu wanaosadikiwa kuwa watumishi wa kanisa hilo walikuwa wakishusha kontena kwa kutumia crane (winchi) chini ya nyaya za umeme wakati wakinyanyua kontena hilo liligusa laini ya msongo mkubwa wa kilovoti 132 inayopeleka umeme Zanzibar,” alifafanua Meneja Uhusiano wa Tanesco.
Severin alieleza kuwa tukio hilo lilisababisha mlipuko mkubwa ulioambatana na kuzimika kwa kituo kikubwa cha kupoozea umeme na mitambo ya kuzalisha umeme iliyopo Ubungo jijini Dar es Salaam.
“Kukatika huko kwa umeme kuliathiri shughuli za uchumi na kijamii ikiwemo mikutano ya kampeni za siasa kwa baadhi ya vyama iliyokuwa unaendeleo katika Mkoa wa Dar es Salaam na mikoa mingine,” alisema ofisa huyo.
Siku hiyo ilikuwa na uzinduzi wa kampeni za urais za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na baadhi ya watu walihusisha tukio hilo kuwa ni makusudi na hujuma za kisiasa; jambo linalothibitika si kweli.
Meneja Uhusiano wa Tanesco alisisitiza kwamba kukatika kwa umeme siku hiyo, haikuwa makusudi au kwa nia ya kuhujumu vyama vya siasa, kama ambavyo imekuwa ikielezwa na baadhi ya watu kwenye vyombo vya habari na hasa mitandao ya kijamii.
Kwa upande wake, Askofu Gwajima alipoulizwa kwa simu kuhusu tuhuma hizo, alisema hana taarifa na ndiyo kwanza anazisikia kutoka kwa mwandishi, licha ya kuwepo taarifa za Tanesco kuonana na uongozi wa kanisa hilo na kuzungumzia jambo hilo. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura alisema hajapata taarifa hizo na atazifuatilia.
HABARILEO
Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli ameelezea namna alivyokuwa akikwepa vishawishi kutokana na hulka yake ya kusimamia uadilifu, uchapakazi na utoaji huduma kwa umma kwa wakati.
Akizungumza katika ziara yake ya siku kumi katika mikoa saba iliyoisha juzi katika Mkoa wa Mtwara, alikokuwa akinadi Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2015-2025, Dk Magufuli alisema yeye si tajiri, lakini kazi aliyokabidhiwa ilikuwa na vishawishi vingi vya kutajirika.
Kishawishi cha kwanza kilichokuwa mbele yake kwa mujibu wa Dk Magufuli, ni idadi kubwa ya wataalamu wa fani mbalimbali za ujenzi walio chini yake ambao amekuwa akiwapa kazi za mabilioni ya fedha.
Alisema amekuwa akisimamia sekta yenye makandarasi 8,500, wahandisi zaidi ya 15,000 na wakadiriaji majengo zaidi ya 1,300 ambao katika usimamizi huo wamenufaika na kazi za Serikali za mabilioni ya shilingi.
Alitoa mfano wa kada ya wakandarasi hao 8,500, ambao alisema angetaka kumuomba kila mmoja wao ampe Sh milioni moja tu kwa mwaka, sawa na Sh milioni 85 kwa mwezi, angeweza kujikusanyia pato binafsi lisilo halali la Sh bilioni 102 kutoka kwa kada hiyo moja tu ya ujenzi kila mwaka.
“Pamoja na kuwa karibu na kishawishi hicho, lakini sikula hata senti moja na kama kuna hata mmoja anayeweza kusema niliwahi kumuomba fedha, ajitokeze,” amekuwa akisema kwa kujiamini.
Katika kuonesha alivyo muadilifu na asivyo na shaka katika kusimamia kazi zenye thamani kubwa, Dk Magufuli alisema pale makandarasi hao walipozembea kazi, aliwafukuza kazi makandarasi 3,000 bila kujali utajiri wao, kwa kuwa kwake alijali kazi tu.
Mbali na kusimamia watu wenye kada hizo za ujenzi nchini huku akiwapa kazi za mabilioni ya shilingi, Dk Magufuli alisema pia Wizara aliyoiongoza kwa muda mrefu ya Ujenzi, ndiyo imekuwa ikipewa fedha nyingi ambapo mwaka jana ilikabidhiwa bajeti ya Sh trilioni 1.2 za wizara, huku Mfuko wa Barabara ulio chini ya wizara hiyo, ukikabidhiwa zaidi ya Sh bilioni 866.
Kwa mujibu wa Dk Magufuli, akipiga hesabu ya fedha za umma alizosimamia kwa ajili ya miradi ya ujenzi wa barabara inayofikia kilometa 17,000 nchini, katika miaka 10 ni zaidi ya Sh trilioni 9.5, lakini hakula hata senti tano, badala yake akajenga mtandao wa barabara za lami nchi nzima.
Dk Magufuli alisema Serikali aliyoitumikia kwa miaka 20 na rasilimali anazozifahamu za nchi ikiwemo gesi, vinaonesha wazi kuwa nchi ni tajiri, hivyo inahitaji mtu mwadilifu kusimamia utajiri huo ushuke kwa watu.
Mgombea huyo aliyenadi ilani hiyo kwa kutembelea wananchi wa vijijini na mijini kwa gari kwa zaidi ya kilometa 3,500 za barabara za vumbi na lami kutoka Katavi mpaka Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe, Ruvuma mpaka Mtwara alielezea kwa ufupi namna nchi ilivyo tajiri.
Alisema kuwa nchi ni tajiri yenye kila aina ya rasilimali ya bahari na mito, ardhi na mbuga na hifadhi za taifa, madini ya aina mbalimbali ya vito na ujenzi na hazina kubwa iliyogundulika hivi karibuni ya gesi, huku kukiwa na uwezekano wa kupatikana kwa mafuta.
Matumizi sahihi ya rasilimali hizo kwa mujibu wa Dk Magufuli, ndiyo utajiri unaoizunguka nchi ambayo amekuwa akisema atautumia kwa uadilifu ili umnufaishe kila mmoja. Alisema umasikini wa Watanzania umeshuka kutoka asilimia 32 mpaka asilimi 28, lakini kwa utajiri uliopo kazi ya Rais ajaye ni kuhakikisha umasikini unashuka zaidi na hili litawezekana kwa kuwa na kiongozi uadilifu atakayesimamia vizuri utajiri wa nchi.
Alikiri kuwa ndani ya CCM na katika Serikali kuna mchwa wa rasilimali za Taifa, lakini akajinasibu kuwa wabadhirifu hao ndani ya chama na Serikali waliposikia ameteuliwa kugombea urais, wameanza kukimbia wenyewe.
Dk Magufuli alisema katika kusimamia vita dhidi ya rushwa na ubadhirifu, ambao umechangia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa umasikini nchini, CCM katika Ilani yake imedhamiria kuanzisha Mahakama Maalumu ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.
Aliwaomba wananchi wa kipato cha chini kwa kuwa wako wengi, wampigie kura kwa wingi, kwa kuwa wabadhirifu hao ambao ni wachache hawampendi, hawatampigia kura na watafanya mbinu nyingi ili asiingie Ikulu.
Kuhusu kukiondoa CCM madarakani kutokana na tuhuma za rushwa na ufisadi, Dk Magufuli alisema ingawa tayari baadhi ya watuhumiwa wameanza kumkimbia, lakini chama hicho pia kina mema mengi kilichofanya na kinachohitaji ni mabadiliko ndani yake, ili kilete mabadiliko kwa Watanzania.
Alitoa mfano wa China, kuwa baada ya miaka mingi ya ukomunisti, chama chao cha kikomunisti hawakukiondoa madarakani ili kufanya mabadiliko, bali walifanya mabadiliko ndani ya chama hicho, ndio wakaleta mabadiliko kwa Wachina, ambayo leo si tu yanaishangaza nchi kubwa ya Marekani, bali hata dunia nzima.
HABARILEO
Rais Jakaya Kikwete amesema kuwa kiongozi anapokuwa amemaliza muda wake wa uongozi na kustaafu, hawezi tena kuanza kudai kwa nini hasikilizwi na uongozi mpya na kwa nini kuomba ushauri.
Rais Kikwete aliyasema hayo usiku wa kuamkia Jumatano alipozungumza katika hafla ya kumuaga ambayo iliandaliwa na Majeshi ya Ulinzi na Usalama ya Tanzania kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, mjini Dar es Salaam.
“Nilisikia mtu mmoja analalamika majuzi kuwa anahama chama kimoja kwenda kingine kwa sababu haombwi ushauri. Sasa wewe ulikwishakuwa Waziri Mkuu, umemaliza ngwe yako ya uongozi, unalazimisha kuombwa ushauri kwa nini?” Alieleza Rais Kikwete.
Aliongeza: “Mimi namaliza ngwe yangu ya uongozi. Nastaafu. Naondoka. Kama Rais anayekuja ataona ni jambo mwafaka kutaka ushauri, nitachangia kwa kadri ya uwezo wangu. Lakini kiongozi aliyestaafu hawezi kulazimisha kuombwa ushauri.
“Rais yeyote anakuwa amekamilika. Anao washauri wake. Kama ni kuhusu usalama mpo nyie wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo vimekamilika. Mtampa ushauri Rais anayekuja kama mlivyokuwa mnanipa mie.”
Aidha, aliwaambia maofisa hao wa vyombo vya ulinzi na usalama: “Na wala siombi nyie mje kwangu kuomba ushauri kwangu. Nendeni kwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu wetu. Vinginevyo mtanitengenezea fitina na kiongozi wangu.
Sitalazimisha wala kulalamika kuwa sijaombwa ushauri.” Rais Kikwete anamaliza muhula wake wa pili kikatiba baadaye mwaka huu kumpisha Rais wa Awamu ya Tano.
MWANANCHI
Mgombea urais wa Chadema chini ya mwamvuli wa Ukawa, Edward Lowassa amesema akichaguliwa kuwa rais wa Awamu ya Tano, ataunda tume tatu ikiwamo ya kuchunguza upya sakata la Operesheni Tokomeza Ujangili ambalo utekelezaji wake ulilalamikiwa na wananchi.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Kashaulili mjini Mpanda mkoani hapa, Lowassa alitaja tume nyingine kuwa ni za kuchunguza mgogoro wa ardhi kati ya Kanisa la Efatha na wananchi na mgogoro kati ya wakulima.
“Kuhusu Operesheni Tokomeza wananchi wengi wamekuwa wakija kuniona na kunieleza wazi kuwa licha ya madhara yaliyojitokeza katika operesheni hiyo hawakulipwa, pia walipoteza haki zao, ndugu na mifugo. Lowassa aliyetokea Namanyere alikofanya mkutano mwingine wa kampeni, aliwataka wananchi kuichagua Ukawa, kwa maelezo kuwa umoja huo utaleta mabadiliko.
Operesheni Tokomeza Ujangili ilibuniwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa lengo la kupambana na ujangili ambao ulikithiri hadi taasisi za kimataifa kuingilia kati.
Hata hivyo, ilisitishwa Novemba Mosi, 2013 ili kupisha uchunguzi wa malalamiko yaliyojitokeza, yakiwamo ya wananchi kuuawa, kuteswa na kuporwa mali zao.
Uchunguzi huo ulifanywa na Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira na sakata hilo lilipowasilishwa bungeni na kamati hiyo, lilisababisha mawaziri wanne kushinikizwa na Bunge kujiuzulu, kutokana na kuhusishwa na yaliyojitokeza wakati wa utekelezaji wa operesheni hiyo.
Mawaziri waliong’oka ni Dk Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani ya Nchi), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa), Balozi Hamis Kagasheki (Maliasili na Utalii) na Dk Mathayo David Mathayo (Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi).
Hata hivyo, hivi karibuni Ikulu iliwaondolea doa mawaziri hao kutokana na ripoti ya Tume iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete kuchunguza tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu, wakati wa utekelezaji wa operesheni hiyo kwa maelezo kuwa waliwajibika kisiasa na hawakuhusika moja kwa moja na vitendo hivyo na hakuna hatua inayostahili kuchukuliwa dhidi yao.
Kuhusu mgogoro wa kanisa la Efatha na wananchi alisema: “Suala hili linalalamikiwa sana na kwa muda mrefu linawatesa wakulima na wawekezaji. Katika kuwalinda wakulima wadogowadogo itaundwa tume ili kuchunguza suala hili ili hatua za haraka zichukuliwe.”
“Kwa muda mrefu kumekuwa na ugomvi kati ya wakulima na wafugaji, hasa waliopo katika Bonde la Mto Rukwa. Nitaunda tume ili kuhakikisha kuwa naondoa migogoro hii ambayo imedumu kwa muda mrefu,” alisema. “Serikali yangu itanunua mahindi kwa wakulima na itawalipa riba.
Haya ndiyo mabadiliko ninayoyataka. Wanaosema hawana sera wanajidanganya sana nawaambieni mkinipa kura nikaingia Ikulu wataisoma namba,” alisema. Mbowe: Tumeunganisha nguvu Akizungumza katika mkutano huo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema: “Tumeunganisha nguvu za Watanzania wenye dhamira na mapenzi mema wanaotaka kuona mabadiliko ya nchi yetu. Tumempokea Lowassa kwa sababu tunaamini atatusaidia safari yetu ya kuwakomboa Watanzania.
“ Mgombea (Lowassa) ameteswa sana CCM na ndoto yake ya uongozi ilikuwa siku nyingi, lakini CCM hawakuiona hiyo na wakampuuza kwa maneno ya uongo.
” Mbowe alisema Rais Kikwete alimtosa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda katika mchakato wa CCM kupata mgombea wake wa urais na kushangazwa na kitendo cha Pinda kuendelea kubaki CCM. Mawaziri wakuu wastaafu, Frederick Sumaye na Lowassa nao walichukua fomu za kuomba ridhaa ya CCM, lakini baada ya kutopitishwa kuwania urais walihamia Ukawa.
Kada mpya wa Chadema, Hamis Mgeja alisema: “Miradi ambayo Magufuli (Dk John) alishindwa kuijenga kwa ubora itajengwa na kumalizwa .
MWANANCHI
Mgombea mwenza wa urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan amesema anayaelewa matatizo ya wazazi kwa kuwa ameshajifungua watoto wanne hivyo ataweza kuyashughulikia vizuri iwapo chama hicho kitashinda kiti cha urais.
Makamu mwenyekiti huyo wa Bunge la Katiba alisema hayo jana jijini Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Nzasa Ninja, Mbagala Charambe wilayani Kigamboni, akiendelea na mikutano yake ya kampeni.
“Nawasikia wanzetu wanasema wanaboresha huduma za kujifungulia wanawake, wao wanajuaje shida za huko (vyumba vya kujifungulia wanawake)? Walifika lini?” alihoji Samia.
“Mimi nina uzoefu kwa sababu nimepita huko mara nne. Pale ndipo tunapowakaribisha watu kuja duniani panatakiwa kuwa safi na salama. Nitahakikisha ninasimamia eneo hili kwa umahiri zaidi.”
Kada huyo mwanamke wa kwanza kuwa mgombea mwenza wa urais katika historia ya Tanzania, alisema inasikitisha kuona kuwa dawa hazipatikani kwenye hospitali za Serikali, lakini kwenye maduka zipo.
Samia pia alizungumzia tatizo la msongamano wa magari jijini Dar es Salaam akisema limekuwa kero kwa wakazi na hivyo chama chake kikishinda kitaendeleza ujenzi wa barabara za juu kwenye makutano.
Alisema pia mabasi ya kwenda haraka, daraja la Kigamboni na ujenzi wa reli za jiji vikikamilika vitapunguza msongamano kwa kiasi kikubwa. Kuhusu elimu, Samia alisema anatambua kuwa wilaya za Temeke na Kigamboni zina shule moja ya serikali ya elimu ya juu ya sekondari ambayo ni Kibasila.
Lakini akasema chama hicho kitajenga shule nyingine ya elimu ya juu ya sekondari wilayani Kigamboni itakayokuwa ya kulala ili kuondoa usumbufu kwa wanafunzi kutembea umbali mrefu.
Kuhusu maji na umeme, Samia alisema mahitaji ya jiji la Dar es Salaam ni kutumia lita milioni 450 kwa siku wakati uzalishaji wa maji ni lita milioni 300 kwa siku.
Alisema miradi mbalimbali ya maji katika jiji inaendelea ikiweamo kuchimba visima virefu katika wilaya ya Kigamboni ili jiji liweze kuzalisha lita milioni 750 kwa siku. Alisema kutakuwa na ziada ya maji na akataka wananchi hao kumchagua kwa mara nyingine aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Kigamboni, Dk Fautine Ndungulile ili aweze kumalizia kazi ya kuwaletea maji.
Aliwaomba wamchague Issa Mangungu kuwa mbunge wa jimbo la Mbagala ili aweze kupambana na matatizo mbalimbali ya wananchi. Akiomba kura, Dk Ndungulile alisema Desemba mwaka huu daraja la Kigambo
PAPO KWA PAPO zipate habari zote zinazonifikia za siasa muziki, michezo, maisha, Breaking news na nyingine kwa kujiunga hapa na mimi >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos