JAMBOLEO
Mwanamke mmoja mjamzito mkazi wa kijiji cha Chakonka Wilaya ya Uvinza, Kigoma amejifungua mtoto mwenye vichwa viwili na baada ya muda mfupi mtoto huyo alifariki.
Ilidaiwa kuwa awali alikwenda kwenye kituo cha afya lakini hakupatiwa matibabu inavyotakiwa na hatimaye alikimbizwa kwenye hospitali ya rufaa ya Mkoa ambapo alijifungua wa upasuaji.
Mume wake alisema mkewe alipata uchungu saa 8 usiku na kukimbizwa na usafiri wa boti usiku huo hadi kituo cha ifya ingawa hawakuweza kumsaidia na Baadaye alipelekwa hospitali ya rufaa Maweni.
Akithibitisha tukio hilo Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali hiyo Shija Ganai alisema walimpokea mganga huyo saa 11 jioni na walipomchunguza walibaini mtoto ametanguliza miguu ndipo wakaamua kumfanyia upasuaji.
Anasema walibaini kuwa mtoto ana vichwa viwili ndiyo sababu ilichangia kufariki dunia mapema kutokana na kubanwa.
MWANANCHI
Rais mstaafu, Benjamin Mkapa ameponda kauli ya vyama vya upinzani kuwa vitaleta mabadiliko, akisema kazi hiyo tayari imefanywa na CCM.
Akizungumza kwenye Uwanja wa Uhuru mjini Bukoba wakati wa uzinduzi wa kampeini za wagombea wa chama hicho mkoani Kagera, Mkapa alisema chama pekee kilichobobea katika ukombozi ni CCM na Serikali zake zilizotangulia.
Kiongozi huyo wa Serikali ya Awamu ya Tatu alisema kuwa lengo la vyama vya upinzani ni kuing’oa CCM na lengo la chama hicho tawala ni kuendelea kushika dola, hivyo upinzani unatakiwa kujifunza hadi baada ya miaka 50.
Alitaja miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa kwa awamu tofauti kuwa ndiyo aina ya mabadiliko ya maendeleo wanayohitaji wananchi, akitaja uwanja wa ndege wa Bukoba na barabara za lami.
“Hayo ndiyo mabadiliko ya maisha ya Watanzania huwezi kuleta ajira kwa kutamka tu, tulianzisha wilaya na mikoa mipya ili kuchochea maendeleo ya wananchi na maisha yao hayo ndiyo mabadiliko,’’Mkapa.
Jana, alionekana kuzungumza kwa tahadhari kwa kile alichodai akiwaeleza wapinzani ukweli wanadai ana jeuri. Hata hivyo, katika hotuba yake alishindwa kujizuia na kutamka neno mbumbumbu na kusema hataki kuwazungumzia.
Kabla ya kumkaribisha Mkapa kuhutubia, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera, Costancia Buhiye alisema wagombea wote wamepita kwenye mchujo sahihi na
MWANANCHI
Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amejitokeza leo na kujibu tuhuma zilizotolewa dhidi yake na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk Willibrod Slaa wiki moja iliyopita.
Askofu Gwajima amekanusha tuhuma za kuwa alimwambia Dk Slaa kuwa wapo maaskofu ambao walihongwa na mgombea wa Ukawa, Edward Lowassa na kuitwa mshenga wa mgombea huyo.
Askofu huyo amesema kuwa hajawahi kumwambia Dk Slaa kuwa maaskofu wa Kikatoliki wamehongwa na Lowassa ili wamchague hivyo aliyoyasema Dk Slaa ni kuwachafua viongozi hao wa dini.
“Dk Slaa anasingizia kuwa maaskofu 30 wamehongwa na Lowassa, hii ni kuwaondolea maaskofu kuaminika (credibility) ili waonekane kuwa hawafai” alisema Gwajima na kuongeza kuwa “ Maaskofu wakatoliki hawakupewa rushwa, maaskofu wa KKKT hawakupewa rushwa, mimi sikupewa rushwa’’
Wakati Dk Slaa anatangaza kustaafu siasa Septemba Mosi, alimwita kiongozi huyo wa Kiroho kuwa ni mshenga wa Edward Lowassa kwa Chadema na kusema kuwa askofu huyo alimwambia kuwa wapo maaskofu 30 wa Katoliki wamehongwa na Edward Lowassa.
Licha ya kukanusha tuhuma hizo, Akofu Gwajima amesema kuwa kuna watu wanawatumia Dk Slaa na mchumba wake, Josephine, na kuwaonya waache kutumika.
Pia Askofu Gwajima ametoa tuhuma kwa Usalama wa Taifa kuwa wanatumika pamoja na Dk Slaa. “Mimi najua wapo Usalama wa Taifa ambao wanamlinda Dk Slaa lakini nawaomba sana Usalama wa Taifa walinde nchi ikae kwa amani, wasijiingize kwenye siasa au kulinda kikundi flani’’ alisisitiza Gwajima.
Aidha askofu huyo amesema kuwa kama Dk Slaa atajitokeza kumjibu kwenye vyombo vya habari, na yeye atajitokeza kuelezea mambo aliyoyafanya Dk Slaa Afrika ya Kusini akiwa na vijana wa Usalama wa Taifa siku chache kabla ya kutangaza kuachana na siasa. Kiongozi huyo wa Kiroho amewataka wananchi waangalie ni mtu yup
NIPASHE
Ukali zaidi wa maisha kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam unakuja kutokana na viwango vipya vya nauli za magari yaendayo haraka kuwa kati ya Sh. 500 hadi 900 kwa safari moja kwa mtu mzima.
Aidha, nauli ya mwanafunzi itakuwa kati ya Sh. 250 na 450 kwa safari moja, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA), imetangaza jana.
Tangazo la Sumatra kwa vyombo vya habari jana lilieleza kuwa, mamlaka hiyo imepokea maombi ya nauli kutoka kwa Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka Dar es Salaam (Udart) ambao utatoa huduma ya usafiri wa umma katika kipindi cha mpito.
Tangazo hilo lilieleza kuwa, safari katika njia kuu pekee mathalani Kimara Mwisho hadi Kivukoni itakuwa Sh. 700 kwa mtu mzima wakati nauli ya mwanafunzi itakuwa Sh. 350. Hivyo kwenda na kurudi kwa mtu mzima itakuwa Sh. 1,400 na mwanafunzi itakuwa Sh. 700.
Aidha, nauli ya pembezoni (Mbezi hadi Kimara Mwisho), itakuwa Sh. 500 kwa mtu mzima wakati kwa mwanafunzi itakuwa Sh. 250.
Pendekezo lingine la nauli ni kwa abiria watakaopita njia ya pembezoni na kisha njia kuu kama kutoka Mbezi-Kimara Mwisho hadi Kivukoni, nauli itakuwa Sh. 800 kwa mtu mzima wakati kwa mwanafunzi itakuwa Sh. 400.
Safari nyingine ni kwa abiria wanaotumia njia ya pembezoni, njia kuu halafu njia ya pembezoni. Mfano wa safari hiyo ni wanaotoka Mbezi-Kimara Mwisho hadi Morocco; nauli yao itakuwa Sh. 900 na wanafunzi itakuwa Sh. 450.
Akizungumza na Nipashe jana, Meneja Miundombinu wa Udart, Mohammed Kaganda, alisema wanategemea kuanza rasmi kazi ya usafirishaji wa abiria kuanzia Kimara Mwisho hadi Kivukoni mapema mwezi ujao.
“Mabasi sasa yapo kwenye maji (kwenye meli baharini), tunategemea yatawasili mwishoni mwa mwezi huu na tutaanza usafirishaji mwanzoni mwa Oktoba, mwaka huu” alisema.
Hata hivyo, alitoa mfano kuwa safari ya njia ya pembezoni, njia kuu na kisha njia ya pembezoni itaokoa fedha za abiria kwa kuwa badala ya kulipa Sh. 1,700 sasa atalipa Sh. 900 kwa kuwa atatumia magari ya Udart.
Alisema mabasi yanayotegemea kuanza kazi katika kipindi cha awali ni 80 na kwamba yatafanyakazi sambamba na daladala za kawaida.
“Katika awamu hii, daladala zitaendelea kufanyakazi kama kawaida lakini hazitatumia njia za mwendo kasi, zitakuwa kwenye barabara hizi za kawaida zinazotumika sasa,” alisema Kaganda.
Nauli ya sasa kutoka Mbezi hadi Posta/Kivukoni ni Sh. 600 kwa mtu mzima wakati kwa mwanafunzi ni Sh. 200 na nauli ya kutoka Mbezi hadi Kimara Mwisho au Ubungo ni Sh. 400 kwa mtu mzima wakati kwa mwanafunzi ni Sh. 200.
Mara ya mwisho kwa Sumatra kupandisha usafiri wa daladala ilikuwa Aprili, mwaka 2013.
Hata hivyo, kabla ya kupitishwa kwa nauli hizo za mabasi yaendayo kasi, Sumatra imeitisha mkutano wa wananchi kwa ajili ya kupata maoni kuhusu maombi hayo kwenye mkutano utakayofanyika Jumanne ijayo.
NIPASHE
Jumla ya watahiniwa 775,729 watafanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi utakaoanza leo hadi kesho utakaoshirikisha shule za msingi 16,096 nchini kote.
Baraza la Taifa la Mitihani limepiga marufuku wagombea wa vyama vya siasa kufanya kampeni karibu na maeneo la shule ili wanafunzi hao wafanye mitihani yao kwa utulivu.
Kati ya watahiniwa hao, wavulana ni 361,502 sawa na asilimia 46.6 na wasichana ni 414, 227 sawa na asilimia 53.4.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Charles Msonde, alisema masomo yatakayotahiniwa ni matano ambayo ni Kiswahili, Kingereza, Sayansi, Hisabati na Maarifa ya Jamii.
“Mtihani wa kumaliza elimu ya msingi (PSLE) utafanyika leo na kesho katika shule 16,096 za msingi, huku watahiniwa waliondikishwa kufanya mtihani huo ni 775,729 kati yao wavulana 361,502 sawa na asilimia 46.6 na wasichana 414,227sawa na asilimia 53.4,” alisema.
Dk. Msonde alisema jumla ya watahiniwa 748,514 watafanya mtihani kwa Kiswahili na watahiniwa 27,215 watafanya wa Kiingereza ambazo ni lugha walizokuwa wakitumia katika kujifunza.
Alisema kati ya watainiwa hao, wasioona ni 76 wakiwamo wavulana 49 na wasichana 27 na watainiwa wenye uoni hafifu ambao huhitaji maandishi makubwa ni 698 kati yao wavulana ni 330 na wasichana 368.
Dk. Msondea alisema maandalizi ya mtihani huo yamekamilika pamoja kusambazwa kwa karatasi za mitihani, fomu maalum za OMR za kujibia mtihani na nyaraka zote mhimu zinazohusu mtihani huo kwenye vituo vyote.
Alitoa wito kwa kamati za mitihani za mikoa na wilaya kuhakikisha taratibu zote za mitihani zinazingatiwa ipasavyo pamoja na kuhakikisha mazingira ya vituo vya mitihani kuwa salama, tulivu na kuzuia mianya inayoweza kusababisha udanganyifu.
Pia aliwataka wasimamizi wa mitihani kujiepusha na vitendo vya udanganyifu kwani Necta itachukua hatua kali kwa yeyote atakayebainika kukiuka taratibu za uendeshaji wa mitihani ya taifa.
NIPASHE
Taasisi tatu nchini, zimejipanga kusaidia gharama za matibabu kwa wanawake wanaougua kansa ya kizazi hususani wenye maisha duni na waishio vijijini.
Taasisi hizo ni Vodacom Foundation ,T-Marc Tanzania na taasisi ya kimataifa ya Pink Ribbon Red Ribbon.
Taasisi ya Vodacom imetoa Dola 87,400 za Marekani kwa kuwawezesha wanawake wanaosumbuliwa na kansa ya kizazi kusafiri kutoka maeneo wanayoishi hadi jijini Dar es Salaam ilipo Taasisi ya Uchunguzi na Matibabu ya Kansa ya Ocean Road (ORCI) kufanyiwa uchunguzi wa awali na matibabu.
Msaada huo kwa kuanzia utawalenga wanawake wanaoishi sehemu ambazo taasisi ya Pink Ribbon Red Ribbon inaendesha miradi yake ya mikoa ya Iringa, Mbeya na Mwanza.
Katika ushirikiano huo, T-Marc itawapatia walengwa kwa ushirikiano na taasisi za afya kwenye mikoa hiyo ambapo baada ya kupatikana, wataunganishwa na mabalozi wa mradi huo kutoka taasisi ya Comprehensive Community-Based Rehabilitation in Tanzania (CCBRT).
CCBRT watapatiwa fedha za kusafirisha walengwa kutoka T-Marc kwa njia ya M-Pesa kununua tiketi za usafiri na watakapofika jijini Dar es Salaam, watapokelewa na ufuatiliaji, gharama za uchunguzi na za matibabu yao, yatafanywa na T-Marc.
Aidha, T-Marc itahakikisha pia wamalizapo uchunguzi na matibabu, wanarejeshwa makwao.
Huduma hiyo pia itatolewa kwa wagonjwa watakaopenda kutibiwa katika Hospitali ya Bugando ya jijini Mwanza ambayo itaanza kutoa huduma kwa wagonjwa wa kansa karibuni.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo uliofanyika jana katika Taasisi ya Ocean Road, Meneja wa Miradi wa T-Marc, Doris Chalambo, alisema tayari umehudumia wanawake 17 kutoka mikoa ya Iringa na Mbeya.
Alisema Tanzania pia ni nchi yenye vifo vingi vya kansa barani Afrika.
“Kupitia msaada huo wa Vodacom Foundation na Pink Ribbon Red Ribbon, wanawake wote waliojitokeza kuchunguzwa na kukutwa wameathirika kwa kiasi kikubwa, wanaendelea kusaidiwa gharama za matibabu,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Vodacom Foundation, Renatus Rwehikiza, alisema msaada wa Dola za Marekani 87,400 umelenga kusaidia matibabu ya akina mama na kupunguza vifo vinavyosababishwa na ugonjwa wa kansa ya kizazi
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Ocean Road, Beatrice Erasto, alisema wananchi wengi wameanza kuuelewa ugonjwa huo na wanajitokeza kwa wingi kufanyiwa uchunguzi wanapohisi dalili tofauti na awali.
Alitoa wito kwa akina mama wenye umri wa kati ya miaka 30 na 50 kujitokeza kufanyiwa uchunguzi wanapohisi dalili ya ugonjwa huo kwani ukigundulika mapema, rahisi kutibika.
NIPASHE
Mgogoro kati ya wakulima na wafugaji Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, sasa umechukua sura mpya baada ng’ombe 11 wa wafugaji wa jamii ya Kimasai wa kata ya Doma wilayani humo, kushambuliwa kwa mapanga na wengine 50 kuibiwa na kundi la watu wanaosadikiwa kuwa wakulima wakiwa na silaha za jadi.
Tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki katika mashamba yanayozunguka kata ya Doma wakati vijana wa wafugaji hao wakiwapeleka ng’ombe hao malishoni.
Mmoja wa vijana waliokuwa wakichunga mifugo hiyo, Mbayani Liongoti, alisema wakati wakiwapeleka ng’ombe hao malishoni, ghafla walivamiwa na kundi la watu hao wenye silaha ikiwamo mishale na mikuki na kuwaamuru kukimbia na kuiacha mifugo hiyo huku wakiwatishia kuwachoma mikuki.
Mchungaji mwingine, Msungu Ibrahim, alisema baadaye waliporejea eneo hilo, walikuta baadhi ya ng’ombe wamekatwa mapanga miguuni na maeneo mbalimbali kiasi cha kuwafanya washindwe kutembea na wengine wameibiwa na hivyo wakatoa taarifa katika Kituo cha Polisi Doma.
Hata hivyo, alisema licha ya kutoa maelezo kuhusu tukio hilo na kuwatambua baadhi ya wahusika, lakini mpaka sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa ikiwamo kutafutwa kwa ng’ombe walioibiwa.
Mmliki wa ng’ombe hao, Ibrahim Rweishuro, alielezea kusikitishwa kwake na hatua hiyo huku akivitaka vyombo vya dola kutenda haki kwa kulinda raia na mali zao.
Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro, Leonard Paulo, alipotafutwa kuzungumzia hatua zilizochukuliwa dhidi ya tukio hilo, alisema bado hajapata taarifa lakini akaahidi kuwa atawasiliana na maofisa wake kufahamu kilichotokea na hatua zilizochukuliwa.
HABARILEO
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema kitendo kilichofanywa na mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa cha kuomba kura kwa kuwataka waumini wa madhehebu ya Kilutheri kumchagua yeye, kamwe hakikubaliki.
Imesisitiza kuwa kitendo hicho, kinawagawa Watanzania na kuwapa mwelekeo wa kuchagua viongozi kwa misingi ya udini na ni ukiukwaji wa Kifungu cha 2.2 (i) cha Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani 2015, kinachosema “Vyama vya Siasa au Wagombea hawaruhusiwi kuomba kupigiwa kura kwa misingi ya Udini, Ukabila, jinsia au rangi.”
Onyo hilo la NEC lilitolewa jana na Mwenyekiti wake, Jaji mstaafu Damian Lubuva ikiwa ni muda mfupi tangu CCM ilipoitisha mkutano wa waandishi wa habari, kuzungumzia suala hilo, huku ikiitaka NEC kuchukua hatua dhidi ya ukiukwaji wa kanuni wa mgombea huyo wa Chadema.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, NEC imewakumbusha wagombea na vyama kuzingatia Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ambayo walikubali kuyafuata kwa kutia saini Julai 27, mwaka huu. Ilisema inasikitisha kuona kiongozi au mgombea anatumia madhabahu kufanya kampeni na mbaya zaidi kuomba kura kwa misingi ya kidini.
“Kitendo kilichofanywa na mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Edward Lowassa kuomba kura kwa kuwataka waumini wa madhehebu ya Kilutheri kumchagua yeye hakikubaliki,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Alisema Tume inavikumbusha Vyama vya Siasa kuzingatia Kifungu cha 2.1 (k) cha Maadili kinachoelekeza vyama au wagombea kutotumia majengo ya Ibada kufanya kampeni, na pia vyama au wagombea kutowatumia viongozi wa dini kupiga kampeni kwa ajili ya vyama vya siasa au wagombea wao.
“Tunatumia fursa hii tena kuwaasa viongozi wa madhehebu yote ya dini kutoruhusu vyama au wagombea au wanachama wa vyama vya siasa kutumia nyumba za Ibada kufanya kampeni za uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani.” Jaji Lubuva alisema mbali ya hilo, Lowassa na viongozi wengine wa Chadema wamekuwa na kauli za kuwaogofya wananchi kuwa ‘kura zitaibiwa’ na kwamba Tume itasababisha machafuko, bila kutoa ufafanuzi jambo ambalo ni hatari.
“Kauli hizo zinashangaza na kustaajabisha na ni kauli za hatari sana kipindi kama hiki, kwa sababu maelekezo kwa vyama vya siasa na wagombea, ambayo wagombea wote na vyama vya siasa walipewa, yana maelekezo kuhusu utaratibu mzima wa kupiga na kuhesabu kura katika ngazi ya kituo, kujumlisha kura katika ngazi ya kata, jimbo na taifa.
Akifafanua utaratibu ulivyo, Jaji Lubuva alisema taratibu zote hizo hushuhudiwa na Mawakala wa Vyama vya Siasa na Wagombea, ambapo kura zikihesabiwa ngazi ya Kituo, mawakala hupewa nakala ya matokeo katika fomu Na. 21A Kura za Urais, 21B Kura za Mbunge na 21C Kura za Udiwani.
Alisema katika ngazi ya Jimbo, hesabu ya kura za kila kituo zilizopo pia katika nakala la Fomu 21A za Urais na 21B za Mbunge hujumlishwa na matokeo kujazwa katika fomu 24A kwa Rais na 24B Mbunge na Nakala ya matokeo wanapewa mawakala wa vyama na wagombea waliopo katika kituo cha kujumlishia kura ngazi ya jimbo.
Kwa upande wa ngazi ya Taifa, alisema Tume hujumlisha matokeo ya kura za Rais mbele ya wagombea na mawakala wa vyama na kutangaza matokeo. Aliongeza kuwa katika hatua hizo, Chadema wanapaswa kueleza wizi unafanyika wapi? “Jana Freeman Mbowe (Mwenyekiti Chadema Taifa) naye amesema kuwa Tume inaegemea Chama Tawala, hivyo itasababisha uvunjifu wa amani. Hili nalo ni tamshi lisilo la ukweli kabisa.
“Wakati wote Tume haiegemei wala kupendelea chama chochote katika kazi zake. Mbowe anajua hivyo, chaguzi zote Tume imefanya kwa kutegemea kura halali zote na ndiyo maana hata wabunge wa vyama vingine walitangazwa.
Alisema viongozi wote hasa wakuu wanaogombea Urais, yafaa wawe waangalifu katika matamshi yao, vinginevyo matamshi ya aina hiyo yanaweza kujenga msingi wa vurugu baadaye.
“Tume ya Taifa ya Uchaguzi inakumbusha vyama vya siasa vijielekeze kwenye kutumia muda mwingi kuelezea Sera za vyama vyao ili ziweze kupimwa na wapiga kura, badala ya kuchochea uhasama kati yao na Serikali na Tume ya Uchaguzi. Kwa mujibu wa Jaji Lubuva, NEC haitasita kukifikisha chama au mgombea mbele ya Kamati ya Maadili ili aweze kuthibitisha kauli yake ;na anaposhindwa Kamati itaweza kutoa adhabu kali kwa chama au mgombea husika, ikiwa ni pamoja na kukatazwa kampeni kwa mhusika.
CCM yaja juu Saa chache kabla ya tamko la NEC la kulaani kitendo cha Lowassa kudaiwa kuomba kura kanisani, ikielezwa amewataka waumini wake kusali ili kanisa la KKKT litoe rais wa nchi kwa mara ya kwanza, CCM nayo ililaani kauli hiyo na kuitaka NEC kuchukua hatua.
CCM kupitia kwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye aliyezungumza jijini Dar es Salaam jana, ilisema inalaani matumizi ya lugha zinazoligawa Taifa kwa misingi ya udini, ukanda, ukabila na ubaguzi wa aina yoyote ili kutafuta madaraka.
Alisema: “Katika hali ya kushangaza na kusikitisha tarehe 6/09/2015, Siku ya Jumapili mjini Tabora, mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chadema, Edward Lowassa aliamua kutumia udini kuomba kura.
“Lowassa akihudhuria ibada katika Kanisa la Kilutheri (KKKT) mjini Tabora amenukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii akidai kuwa kwa kuwa toka nchi ipate Uhuru hajawahi kutokea rais kutoka dhehebu la Kilutheri, hivyo mwaka huu ni zamu ya Walutheri.”
Nape alisema kauli hiyo ya Lowassa, licha ya kuwa ni kinyume na Sheria za Uchaguzi, kinyume na Kanuni za Maadili ya Uchaguzi zilizosainiwa na vyama vyote, lakini ni kinyume na mila na desturi za Kitanzania katika kuhakikisha Taifa linabaki kuwa moja, lenye umoja, amani na mshikamano.
Akinukuu mazuio yanayopinga kile kilichofanywa na Lowassa, Nape alisema;”Kwa mfano Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2015, yaliyotolewa na Tangazo la Serikali Namba 294 la tarehe 27/7/2015 chini ya Kifungu cha 124A cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343 Ukurasa wa 5 Kifungu 2.1 (k) kinasema;
“Viongozi wa vyama vya siasa, wagombea au wafuasi wao wahakikishe kuwa majengo wanayotumia kufanya kampeni si ya Ibada. Vile vile vyama vya siasa vihakikishe kuwa havitumii viongozi wa dini kupiga kampeni kwa ajili ya vyama vya siasa au wagombea wao.”
Nape alisema lakini katika maadili hayo hayo, ukurasa wa saba Kifungu cha 2.2 (i) kinasema; ”Vyama vya siasa au wagombea hawaruhusiwi kuomba kupigiwa kura kwa misingi ya udini, ukabila, jinsia au rangi.”
Akizungumzia kauli ya rais kutokana na Walutheri, Nape alisema matamshi hayo ni uthibitisho tosha kuwa Lowassa, chama chake cha Chadema na vyama vinavyomuunga mkono chini ya Ukawa ni wabaguzi, wachochezi na waroho wa madaraka wasiojali masilahi mapana ya nchi na kwamba kwao madaraka ni muhimu kuliko nchi.
HABARILEO
Tanzania imetajwa kuwa kinara katika nchi za Afrika Mashariki kwa kutunza amani na utulivu tangu ipate uhuru, huku Rais Jakaya Kikwete akiibuka kiongozi bora katika ukanda huo kwa kujitolea kuleta amani katika Bara la Afrika na kutunza amani hiyo nchini mwake.
Kwa hali hiyo, Rais Kikwete ametunukiwa tuzo mbili na Taasisi ya East Africa Book of Records ya nchini Uganda, moja ikiwa ni kwa ajili ya Tanzania ambayo imefanikiwa kutunza amani pamoja na utulivu tangu uhuru na nyingine ni ya Rais Kikwete mwenyewe kutokana na juhudi zake za kupigania amani nchini mwake na eneo lote la ukanda wa mashariki mwa Afrika.
Kutokana na tuzo hizo, sasa Rais Kikwete ameacha kumbukumbu katika vitabu vya nchi za Afrika Mashariki, kama mtu na kiongozi maarufu aliyetoa mchango mkubwa katika kuleta amani kwenye nchi za ukanda huu.
Akikabidhi tuzo hizo jana Ikulu, Dar es Salaam, Kiongozi wa taasisi hiyo Dk Paul Bamutaze alisema wametoa tuzo hizo baada ya kuangalia mchango wa Rais Kikwete katika kuleta amani katika baadhi ya nchi barani Afrika, akitoa mfano namna kiongozi huyo alivyoleta amani mwaka 2008 nchini Kenya, kufuatia machafuko baada ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu.
“Tuzo ya kwanza tunaitoa kwa Tanzania kama nchi kwani ndio nchi pekee katika eneo la Afrika Mashariki ambayo imedumisha amani na utulivu tangu kupata uhuru na ndio imekuwa inasaidia kutatua migogoro mbalimbali kwa majirani zake na inaendeshwa kwa utawala wa sheria,”Dk Bamutaze.
Alisema tuzo ya pili wanamkabidhi Rais Kikwete kutokana na kuwa kiongozi bora, ambaye amedumisha amani nchini mwake, lakini pia ameshiriki kutatua migororo mbalimbali. Alisema licha ya Kenya, lakini ni Rais Kikwete ambaye ameshiriki kuleta amani nchini Burundi na kurejesha serikali iliyokuwepo madarakani baada ya kuwepo jaribio la uasi.
Rais Kikwete pia amesaidia kuleta amani katika nchi za Sudan Kusini, Comoro, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) baada ya Jeshi la Tanzania kuwasambaratisha kundi la waasi la M23.
Mkuu wa Kitengo cha Utafiti wa taasisi hiyo, Adam Buyinza alisema katika utafiti ambao wameufanya, wamegundua kuwa Tanzania imedumu kuwa na amani kutokana na kuongozwa na CCM ambacho kina sera zinazoeleweka.
Kwa upande wake, Rais Kikwete alisema kwamba misingi ya amani na utulivu uliopo nchini umewekewa misingi yake na Mwalimu Julius Nyerere, ambaye uongozi wake haukubagua watu kwa misingi ya kidini, rangi na kabila au eneo ambako anatoka mtu.
Alisema tuzo hiyo aliyoipokea sio yake peke yake, bali ni ya wananchi wa Tanzania pamoja na wasaidizi wake ambao yeye kama nahodha wa meli wamesaidiana kuhakikisha kuwa meli yao inaenda vizuri hata pale panapotokea mawimbi wanasaidiana kukiendesha chombo hicho.
Rais Kikwete alisema kuwepo kwa amani nchini, kumetokana na watu wake kuamini kwenye majadiliano badala ya kupigana na alisema hata pale ilipotokea tofauti kati ya Serikali na vyama vya upinzani, walikaa meza moja wakazungumza na pale ilipotokea tofauti kati ya Waislamu na Wakristo pia walitatua migogoro yao kwa mazungumzo.
MTANZANIA
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis jana alieleza mabadiliko mapya yanayolenga kuwarahisishia Wakatoliki kuvunja ndoa zao na kuoa upya.
Dhamira hiyo ni ishara nyingine ya dhamira ya Papa huyo kutaka kulifanya Kanisa Katoliki liwe rafiki zaidi na kuendana matakwa ya walio wengi.
Akizungumza kuhusu mabadiliko hayo, Papa alisema si haki kwa wenzi kuishi muda mrefu ‘wakikandamizwa na wingu la shaka’ kuhusu uhalali wa ndoa zao.
Ikumbukwe kwamba ni msimamo wa Papa kumkatalia Mfalme Henry the VIII wa Uingereza kumtaliki mkewe Catherine wa Aragon katika karne ya 16 uliosababisha England ijitenge na Rome na kushuhudia kuundwa kwa Kanisa la England huku mfalme akiwa mlinzi wa Imani wa kanisa hilo.
Mabadiliko makuu matatu aliyotangaza na Papa jana ni kuondoa mchakato wa mapitio ya mara ya pili wa uamuzi wa kutoa talaka kupitia mahakama ya kanisa kabla ya ndoa kuvunjwa.
Mengine ni kuwapatia maaskofu uwezo wa kuharakisha na kuvunja ndoa wenzi wanapoamua wenyewe katika mazingira fulani kama vile ukatili katika ndoa au uasherati na mchakato huo wa talaka kuwa bure, isipokuwa kwa kulipa ada ndogo kwa ajili ya gharama za utawala.
Kabla ya sheria hiyo, Wakatoliki waliotaka talaka walihitaji kibali kutoka kwa mahakama mbili za kanisa, wakati sheria mpya inabakiza moja ingawa rufaa bado zinaruhusiwa.
Kabla ya sheria hiyo, wanandoa wa Wakatoliki wanaotalikiana bila idhini ya kanisa na kuolewa upya walihesabiwa kama wazinifu na hawakuruhusiwa kupokea komunio.
Lakini kwa mujibu wa utaratibu mpya, wanaotalikiana wakioa au kuolewa tena watabakia kuwa wafuasi wa kanisa hilo.
Mwaka jana Papa aliunda tume ya wanasheria wa kanisa hilo kuboresha na kurekebisha taratibu hizo kurahisisha wanandoa kuachana na kupunguza gharama.
Mageuzi hayo yalikuja katika mfumo wa nyaraka mbili zinazoitwa ‘motu proprio’, neno la kilatini lililobuniwa na Papa mwenyewe.
Taratibu hizo zitakuwa rasmi kama sehemu ya sheria za kanisa (canon law) ifikapo Desemba 8 mwaka huu wakati Papa atakapoanza kutangaza Mwaka wa Jubilee ambao kwa kawaida huhusishwa na msamaha.
PAPO KWA PAPO zipate habari zote zinazonifikia za siasa muziki, michezo, maisha, Breaking news na nyingine kwa kujiunga hapa na mimi >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos