MWANANCHI
Wakati Rais Jakaya Kikwete akitangaza kuwa leo ni siku ya mapumziko nchi nzima ili kutoa nafasi kwa Watanzania kushiriki na kufuatilia sherehe za kuapishwa kwa Rais mteule, Dk John Magufuli kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam, wanafunzi wa kidato cha nne wataendelea na mitihani yao ya kuhitimu elimu ya sekondari kama kawaida.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, Rais Kikwete ametoa uamuzi huo kwa mujibu wa mamlaka aliyo nayo chini ya Kifungu cha 3 cha Sheria ya Sikukuu za Kitaifa.
Dk Magufuli ataapishwa leo kwenye uwanja huo na kufuatiwa na hafla fupi ya kumpongeza itakayofanyika kwenye Viwanja vya Ikulu.
Kidato cha nne Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), Dk Charles Msonde alisema mitihani ya taifa ya kidato cha nne iliyoanza mwanzoni mwa wiki hii itaendelea kama kawaida.
Dk Msonde alisema kwa mujibu wa kanuni za mitihani za Necta, Sura ya 7 kifungu kidogo cha 3, endapo kutatokea sherehe ya kitaifa, wakati mitihani ya kitaifa ikiwa imeanza, mitihani hiyo itaendelea kama kawaida.
Alisema wafanyakazi waliopangwa maalumu kwa ajili ya kusimamia mitihani, wataendelea na shughuli hiyo na wale wasio na kazi wataendelea na mapumziko.
“Tumepokea taarifa ya mapumziko kwa furaha maana wafanyakazi mbalimbali watapata fursa ya kuhudhuria sherehe za kumwapisha rais wa awamu ya tano… lakini kwa mujibu wa kanuni za mitihani za Necta, mitihani hii iliyokwishaanza itaendelea kama ilivyopangwa” Dk Msonde.
Tucta yaponda Wakati hayo yakijiri, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Nicholaus Mgaya ameponda uamuzi huo wa mapumziko leo akisema sikukuu za kitaifa zinajulikana.
MWANANCHI
Rais Jakaya Kikwete jana alikutana kwa saa moja na mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kuzungumzia hali ya kisiasa Zanzibar.
Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, ilisema mazungumzo hayo yalitokana na ombi la Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, kutaka kukutana na kuzungumza na Rais Kikwete.
Viongozi hao walikubaliana kwamba mashauriano yaendelee kufanyika baina ya pande zote zinazohusika na hali ya kisiasa Zanzibar.
Mazungumzo hayo yanalenga kutatua mgogoro wa kisiasa uliotokana na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar kwa madai ya kuwapo kasoro nyingi na kutaka kuitisha uchaguzi upya baada ya siku 90.
Mkutano huo umefanyika siku saba tangu Maalim Seif atangaze msimamo wa kutoshiriki tena uchaguzi mwingine huku akiitaka ZEC itangaze matokeo ya uchaguzi uliofutwa.
Pia, mazungumzo yamefanyika siku tatu baada ya Rais Kikwete kusema hakukuwa na maombi ya Maalim Seif kuonana naye, bali kulikuwa na malalamiko dhidi ya utendaji wa polisi Zanzibar na kutaka miadi na Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange.
Rais Kikwete aliiagiza ofisi yake kufanikisha mazungumzo baina ya mgombea huyo wa urais na Jenerali Mwamunyange.
Awali, aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alimtaka Rais Jakaya Kikwete kumaliza tatizo la Zanzibar kwa kuiamuru ZEC kumtangaza mshindi wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 ili kuliepusha Taifa kuingia kwenye machafuko.
Oktoba 28, Mwenyekiti wa ZEC, Salum Jecha Salum alitangaza kufuta matokeo ya uchaguzi huo.
MWANANCHI
Mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Nne wametakiwa kurejesha Ikulu magari wanayotumia mara baada ya kuapishwa Rais Mteule John Magufuli kwenye Uwanja wa Uhuru leo.
Mawaziri hao wamekuwa wakiyatumia magari hayo tangu Bunge la Muungano lilipovunjwa, huku baadhi wakiwa wameshapoteza nafasi ya kurudi bungeni baada ya kushindwa kwenye majimbo yao na wengine kuanguka kwenye kura za maoni.
Jana, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema katika taarifa yake kuwa mara baada ya kumalizika kwa sherehe za kumuapisha Dk Magufuli, magari hayo yatabandikwa kibao cha namba za ST na madereva kuwarejesha nyumbani mawaziri waliokuwa wakiyatumia na baadaye kuyapeleka Ikulu kusubiri kupangiwa kazi nyingine.
Agizo hilo linawahusu mawaziri wote wa Serikali ya Awamu ya Nne, isipokuwa aliyekuwa Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk. Makongoro Mahanga ambaye tayari alisharejesha gari hilo baada ya kuamua kuhama CCM, hivyo kupoteza sifa za kuendelea kuwa waziri.
Wengine ni aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda na aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi), Celina Kombani ambao walifariki dunia hivi karibuni. “Utaratibu uko wazi miaka yote,” alisema Balozi Sefue.
“Waziri anabaki kuwa waziri mpaka siku na muda Rais mpya anapoapishwa. “Pale kiwanjani (uwanja wa uhuru) wakati bendera ya Rais wa Awamu ya Nne inashuka, na wale mawaziri ndiyo unakuwa mwisho wao.
Kuanzia hapo hawaruhusiwi kutumia magari hayo na yanatakiwa kurudi Ikulu kufanyiwa matengenezo na kusubiri mawaziri wengine.
” Balozi Sefue alisema Serikali haina utaratibu wa kununua magari mapya na kwamba magari yanayotumiwa sasa yangeweza kubaki wizarani na kutumiwa na makatibu wakuu, lakini utaratibu ulibadilika ili kubana matumizi.
“Kwa hiyo yatarejeshwa kwa ajili ya kutumiwa na mawaziri wengine,” alisema.
Alisema wakati Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa akimuachia kijiti Rais Kikwete, utaratibu wa kurejesha magari uliotumika ni huohuo. Alipoulizwa kama utaratibu huo ulikuwa ukitumia nyuma ya hapo alisema ulitumika mwaka 2005, lakni hana kumbukumbu ya kabla ya hapo.
NIPASHE
Wagombea wanne urais wa Zanzibar wametaka kufutwa kwa uteuzi wa Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad na kufunguliwa mashtaka kutokana na kitendo chake cha kujitangaza ameshinda urais kabla ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kutangaza matokeo.
Wagombea hao walitoa tamko hilo jana wakati wakizungumza na waandishi wa habari, Vuga, mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Akisoma tamko hilo kwa niaba ya wenzake, mgombea wa urais kupitia chama cha AFP, Soud Said Soud, alisema kitendo cha Maalim Seif kujitangaza kuwa mshindi katika uchaguzi huo kabla ya Zec ni kinyume cha sheria ya uchaguzi Namba 11 ya mwaka 1984.
“Tunamshauri Rais wa Zanzibar kufuta uteuzi wa Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad katika kipindi hiki cha mpito kutokana na kiongozi huyo kupoteza sifa za kuendelea kushika wadhifa huo na nafasi hiyo apewe mtu mwingine,” Soud.
Alisema inashangaza kuona vyombo vya sheria na Zec wanakuwa wazito kuchukua hatua za kisheria wakati ni kosa kwa mgombea kujitangaza mshindi kabla ya matokeo rasmi ya tume hiyo.
Aidha, alisema kauli na matamshi ya Maalim Seif ambayo amekuwa akiyatao hadharani dhidi ya Rais wa Zanzibar yanamuondolea sifa ya kuendelea kushika wadhifa huo akiwa mshauri mkuu wa Rais katika kutekeleza kazi zake kwa mujibu wa kifungu cha 39 (5) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Wagombea hao wameunga mkono uamuzi wa Mwenyekiti wa Zec kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu wa Zanziba uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Wagombea waliotoa tamko hilo ni, Ali Khatibu Ali (CCK), Hafidhi Hassan Suleiman (TLP) na Issa Mohamed Zonga ambao wamesema wanasubiri taarifa ya siku ya kufanyika uchaguzi mwingine.
NIPASHE
Kaimu Mkurugenzi Mkuu Idara ya Sheria wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Kokukulage Kazaura (39), amedai mahakamani kwamba mkataba wa mradi wa ujenzi wa gati namba 13 na 14, haukufuata taratibu za kisheria na Sheria ya Manunuzi ya Umma kati ya mamlaka hiyo na Kampuni ya Ujenzi ya China Communications Ltd.
Kazaura alitoa madai hayo jana wakati akitoa ushahidi wa Jamhuri dhidi ya kesi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa TPA, Ephraim Mgawe na Naibu Mkurugenzi Mkuu, Hamad Koshuma, ya matumizi mabaya ya madaraka kwa kusaini mkataba wa kuipa kazi Kampuni ya Ujenzi ya China Communications Ltd bila kutangaza zabuni.
Ushahidi huo unasikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Mfawidhi, Cyprian Mkeha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.
Alidai kuwa idara yake inashughulika na masuala yote ya kisheria ikiwamo kuingia mikataba na kutunza nyaraka zote za kisheria.
“Mikataba ambayo ninahusika nayo katika ofisi yangu ni pamoja na manunuzi, ujenzi na upangishaji … mchakato wa kuandaa mikataba inaanzia idara husika ikiwamo ya manunuzi au ujenzi,” alidai shahidi huku akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Pius Hilla.
Alifafanua kuwa hatua inayofuata ni kuhakikisha idara ya manunuzi inatangaza zabuni na baada ya kampuni zinzojitokeza zinachambuliwa na kutangazwa.
“Baada ya hatua hiyo, idara ya manunuzi wanaandaa rasimu ya mkataba na kuileta idara ya sheria ili kuangalia kama imekidhi matakwa ya kisheria, ndipo idara yangu inawasilisha kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ili iangalie kama taratibu za manunuzi zimefuatwa,” alidai Kazaura.
Hata hivyo, alidai kuwa mkataba wa kuipa kazi Kampuni ya Ujenzi ya China Communications Ltd, haukupitia mchakato huo na kwamba alishtukia kuona mradi unaendelea na alipohoji idara ya mipango ilitoa mkataba kati ya TPA na kampuni hiyo uliosainiwa Desemba 5, mwaka 2011.
Alidai kuwa aliomba mkataba huo kwa ajili ya kuhifadhi kwenye idara yake na kwamba baada ya kuukagua, ulikuwa umesainiwa kati ya washtakiwa Mgawe na Koshuma na wawakilishi wa kampuni ya ujenzi Guo Qing na Yu Peng.
Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa ushahidi wa Jamhuri Novemba 30, mwaka huu.
HABARILEO
Mgombea udiwani kata mpya ya Kanda wilaya ya Sumbawanga Vijijini mkoa wa Rukwa, Ozem Chapita (CHADEMA) amepinga matokeo yaliyompatia ushindi mdogo wake Yowtai Meshack (CCM) kwa tofauti ya kura moja.
Katika matokeo ya uchaguzi huo yalimtangaza Meshack (CCM) kuwa mshindi wa udiwani kata ya Kanda.
Alijizolea kura 997, akifuatia kwa karibu na mpinzani wake wa karibu ambaye ni kaka yake, alipata kura 996 .
Chapita ambaye ni Katibu wa Chadema mkoa wa Rukwa, amedai kuwa atayapinga matokeo hayo mahakamani kwa kuwa uchaguzi wenyewe uligubikwa na kasoro kadhaa .
Alitaja kasoro hizo kuwa ni pamoja na orodha ya wapiga kura kubandikwa kwa kuchelewa saa 8:00 mchana Oktoba 24, siku moja kabla ya uchaguzi kufanyika Oktoba 25. Alidai, wapiga kura wapatao 40 walishindwa kupiga kura katika kata ya Kanda kwa kuwa majina yao yalitokea katika Kata ya Chitete ambayo ipo kilomita tano kutoka Kata ya Kanda.
“Isitoshe wakati wa mikutano ya uchaguzi viongozi wa CCM walinipaka matope na kunivunjia heshima kisiasa mbele ya jamii wakinituhumu hadharani kwenye mikutano yao ya kampeni kuwa nilimuua Mwenyekiti wa kijiji cha Lula Kata ya Kaengesa Yoktan Meshack mwaka 2001, tuhuma ambazo hazina ukweli,”alisema.
Chapita ambaye kwa miaka mitano iliyopita alikuwa diwani wa kata ya Kaengesa, alidai kuwa dosari nyingine ni pamoja na kuzuiwa kufanya mikutano ya kampeni katika kijiji cha Lyapona wakati wagombea wa CCM waliruhusiwa.
HABARILEO
Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Vunjo na Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema amempongeza Rais Mteule, Dk John Magufuli kwa kushinda urais na kumuomba katika uongozi wake amfikirie.
Aidha, mwanasiasa huyo, amelia na kile alichodai ni kuhujumiwa jimboni kwake Vunjo na hivyo kushindwa katika uchaguzi wa ubunge.
Aliyeshinda ni James Mbatia wa NCCR- Mageuzi. Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uchaguzi mkuu ambao alishindwa kutetea kiti chake cha ubunge jimboni Vunjo.
“Naomba Dk Magufuli atimize ahadi yake aliyoitoa baada ya kuja kwenye kampeni Vunjo na kusema, endapo sitapata ubunge, atanifikiria kwa kuwa anatambua utendaji kazi wangu,” alisema.
Mrema alisema Dk Magufuli alipokwenda jimboni kwake, pia na yeye alitumia nafasi hiyo kumnadi kwa kuwa barabara zilizojengwa Vunjo, zilitokana na kazi yake (Magufuli).
Alisema haikuwa jambo baya kwake kumnadi mgombea wa chama kingine kwa kuwa ni mtendaji mzuri na ana matumaini kwamba wananchi watanufaika.
Akizungumzia matokeo ya uchaguzi na hujuma alizofanyiwa, Mrema alidai vilitumika vipeperushi vilivyokuwa vinaonesha vina alama ya ndiyo bila ya ruhusa ya msimamizi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Kwa mujibu wa Mrema, hakuwa mtu wa kushindwa katika uchaguzi huo kwa kuwa wananchi wake wanampenda na hawaamini matokeo ya uchaguzi huo. Wakati huo huo, aliyekuwa mgombea Urais wa TLP, MacMillian Lyimo alisema uvyama hautalifikisha taifa mahali pazuri isipokuwa kwa kuunda serikali ya Kitaifa.
Lyimo alisema, kitendo cha Mrema kumnadi Magufuli si tatizo bali ni ishara ya kuwa na serikali inayokubalika na vyama vyote.
Mwenyekiti wa wanawake jimbo la Vunjo kupitia TLP, Venancia Msoya alisema Mrema aliwasaidia katika uongozi wake kwa kudhamini vikundi 43 vya wanawake na kuwa bega kwa bega na wananchi wa jimbo hilo.
Alisema wanasikitika kuona kiongozi wao amekosa ubunge kwa hujuma alizofanyiwa na wapinzani wake.
Unataka kutumiwa MSG za habari zote kubwa kutoka kwa Millard Ayo? ukiwa na line ya tiGO andika ‘AYO’ tuma kwenda 15510, msg utayotumiwa jibu OK ili uanze kupokea matukio yote kwa sms, pia ungana na Millard Ayo kwenyeTwitter,FB,Instagram na YouTUBE wa kubonyeza hapa >>> INSTAGRAMTWITTERFB YOUTUBE.