MWANANCHI
Mkoa wa Arusha umetajwa kati ya mikoa ya pembezoni nchini ambayo inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu wanaomiliki silaha za moto, hasa bastola.
Katika maeneo ya burudani katika jiji la Arusha kumekuwapo na matukio ya watu kutishiana kwa bastola jambo ambalo limesababisha ulinzi kuimarishwa katika maeneo haya na baadhi ya wateja kuzuiwa kuingia ndani na silaha hizo.
Uchunguzi wa kina uliofanywa na Mwananchi umebaini kuwa idadi kubwa ya vijana katika jiji la Arusha wanamiliki bastola, baadhi kihalali na wengine kinyume cha sheria.
Kwa wanaomiliki kihalali ni wale waliofuata utaratibu za kisheria za umiliki, ambao unaanzia ngazi ya kijiji au mtaa, kujadiliwa na baadaye kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya, kamati ya mkoa na hatimaye makao makuu ya polisi.
Hata hivyo, kati ya wanaomiliki kihalali, kuna kundi ambalo linamiliki bastola hizo kihalali kupitia mawakala ambao hulipwa kati ya Sh1.5 milioni hadi Sh2 milioni.
Uchunguzi umebaini kuwa watu wengi wanaomiliki silaha hizo kinyume cha sheria ndiyo wanazitumia katika matukio ya uhalifu.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas licha ya kukiri vijana wengi kumiliki bastola katika jiji hilo, alisema wengi wanaozimiliki wamezipata kwa kufuata sheria.
Hata hivyo, katika kudhibiti silaha hizo, alisema jeshi hilo kwa kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama limesitisha kutoa vibali vya umiliki wa bastola.
“Tumesitisha kutoa vibali vya bastola lakini tunatoa vibali vya silaha nyingine kwa mahitaji maalumu, lakini silaha zilizopo mikononi mwa watu ni zile ambazo zilitolewa kipindi kirefu cha nyuma,” alisema.
Alisema baadhi ya waliopata bastola kipindi cha nyuma ni wafanyabiashara na wachimbaji wa madini katika maeneo ya Mererani kulingana na biashara zao.
Hata hivyo, alisema silaha hizo zilitolewa kihalali lakini baadhi ya wamiliki wamekuwa si waangalifu katika utunzaji na hivyo kufanya baadhi kuwafikia watu wasio waaminifu.
“Katika matukio ya ujambazi ambayo yanatokea hapa Arusha, silaha ambazo tunakamata ni zile ambazo zilizotolewa kihalali lakini wamiliki wake waliibiwa au kupoteza,” alisema.
Alisema uhakiki wa silaha ambao umekuwa ukifanywa na jeshi hilo na kwa kiasi kikubwa umesaidia kuziondoa bastola mikononi mwa watu wasio waaminifu.
Kuuzwa kwa silaha Mwananchi imebaini kuwa, baadhi ya wamiliki wa silaha hasa bastola wamekuwa wakiuza mitaani kutokana na hali ngumu ya maisha.
Joram Kaaya mkazi wa Ngulelo alilieleza gazeti hili kuwa kipindi cha nyuma vijana wengi wa Mirerani walinunua silaha kihalali kutokana na biashara zao lakini sasa kutokana na kuporomoka biashara ya madini ya Tanzanite wamekuwa wakiuza.
“Bastola zinauzwa kati ya Sh1,000,000 hadi 2.5 milioni kutoka kwa wamiliki lakini wanakueleza kufuata taratibu za umiliki, kwa kuandika barua ya umiliki wa silaha ngazi ya mtaa na kwenda polisi kabla ya kukabidhiwa silaha na kitabu chake,” alisema.
Mkazi mmoja wa Arusha, aliyeomba kuhifadhiwa jina, lake alikiri kuwapo kwa madalali wa silaha ambao wamekuwa wakifuata taratibu za umiliki wa silaha.
“Mimi mwenyewe nimenunua bastola yangu kwa mtu lakini kabla ya kumiliki nilifuata taratibu zote za kipolisi na kiserikali na nimekuwa nikiilipia kila mwaka,” alisema.
Hata hivyo, Kamanda Sabas alikemea utaratibu wa kununua silaha mitaani akisema ni kuvunja sheria. “Ni makosa kisheria, kuuza na kununua silaha mitaani ambao watakamatwa watafikishwa katika vyombo vya sheria, kuna taratibu za umiliki kwa ambao wanahitaji silaha ni vyema kuzifuata,” alisema.
Silaha kutoka nje Wakati polisi wakieleza kuwapo udhibiti mkubwa katika uingiaji wa silaha katika njia haramu, taarifa zilizolifikia Mwananchi zinaeleza kuwa wapo watu wanaziingiza kutoka nje ya nchi kupitia njia za panya.
Silaha hizo, zinaelezwa kuingizwa kwa kubadilishana na bidhaa mbalimbali kama vyakula, mifugo na fedha. Katika Wilaya ya Ngorongoro pekee, ambayo ipo mpakani na nchi jirani na Kenya, mara kadhaa polisi, wamekuwa wakikamata silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria ambazo zinamilikiwa na makundi ya wafugaji na wakulima ambao wamekuwa wakipigana mara kwa mara kugombea ardhi.
MWANANCHI
Watu wanne juzi walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na shtaka la kusambaza taarifa za uwongo.
Wakili wa Serikali, Wankyo Simon akishirikiana na Mwanasheria Mwandamizi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Johannes Kalungula mbele ya Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha, waliwataja washtakiwa hao kuwa ni Leila Sinare (36), Godfrey Soka (45), Deo Edmund Soka (40) na Monica Soka, wote wakazi wa Dar es Salaam.
Akiwasomea hati ya mashtaka, Wankyo alidai kuwa washtakiwa walifanya makosa hayo kinyume na Kifungu cha 16 cha Sheria ya Mtandao namba 14 ya mwaka 2015.
Alidai kuwa kati ya Oktoba 20 na 30, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa Leila alisambaza taarifa za uongo kwa njia ya sauti kupitia mtandao wa whatsapp kwenye ‘kundi la soka’, uliokuwa na lengo la kuupotosha umma katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25.
Wakili huyo wa Serikali alidai shtaka la kwanza linamkabili Leila anayedaiwa kusambaza ujumbe usemao: “Ndugu zangu wa kigango cha siasa, hakuna cha kutakiana uchaguzi mwema wala nini, nchi yetu inaingia kwenye machafuko muda wowote kuanzia sasa hivi.
“Kama tulivyoambiwa kwamba nchi hii itageuka kuwa nchi ya vita, ni kweli imeingia kwenye vita maboksi yenye kura feki yamekamatwa, Jimbo la Vunjo yamekamatwa maboksi matatu, tumekamata maboksi matatu feki Moshi Mjini, maboksi sita 6 Ilemela, maboksi 12 Hanang’.
“Kwa kifupi, uchaguzi umeshavurugika na Tanga nasikia magari yamesimama sehemu, makamanda wetu bado wanaendelea kufuatilia, lakini inasemekana kuna maboksi ya kura na mpaka sasa hivi hali siyo nzuri, CCM wameingiza kura nyingi feki na niseme kutokana na hali halisi ambayo ipo, hatuponi, hatuponi kwa sababu Mwanza vijana wameshaanza kuuawa, wameshakufa vijana wanne, watano mpaka sasa hawajulikani walipo na hali hiyo inaendelea, CCM jamani tunaomba mtuachie nchi kwa amani, kweli ingelipaswa kutuua angalau kwa sumu mkabaki wenyewe, msitutese msitutese.”
Washtakiwa Godfrey, Deo na Monica, wanadaiwa kuwa kati ya Oktoba 20 na 30, 2015 kwa pamoja, walisambaza taarifa za uongo kwa njia ya mtandao wa whatsapp ujumbe kama aliousambaza Leila kwa lengo la kuupotosha umma.Kesi hiyo iliahirishwa hadi Desemba 3, kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa waliachiwa kwa dhamana.
MWANANCHI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli amefuta safari zote za nje ya nchi kuanzia leo hadi hapo maamuzi mengine yatakapotolewa.
Dk Magufuli ameagiza shughuli zote zinazotakiwa kufanywa nje ya nchi zifanywe na kusimamiwa na mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nchi za nje.
Uamuzi huo wa rais ameutoa Ikulu jijini Dar es Salaam katika kikao kilichojumuisha watendaji mbalimbali wa serikali wakiwemo Makatibu wakuu, Manaibu Makatibu wakuu, Gavana wa Benki Kuu na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari ruhusa ya safari nje ya nchi inaweza kutolewa kwa jambo la dharura ambalo hata hivyo jambo hilo lazima lipate kibali cha Katibu Mkuu Kiongozi. “Badala yake rais ametaka ziara nyingi zielekezwe kwenda vijijini ili kuwawezesha watendaji kujua na kutatua kero za wananchi” imesema taarifa hiyo.
Katika kikao hicho, rais ameelekeza pia mambo kadhaa ambayo watendaji hao wanapaswa kuyasimamia, kuyawekea mikakati na kuyapanga vizuri ili yasimamiwe mara moja na Baraza la Mawaziri atakaloliteua.
Mambo hayo ni pamoja na kuanza kwa mikakati ya kuhakikisha wanafunzi wote wanaanza kupatiwa elimu ya bure kuanzia Januari mwakani.
Taarifa hiyo imetaja jambo la pili kuwa ni suala la uratibu wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ambapo ameagiza lifanyiwe kazi na mipango yake ikamilike kwa ajili ya utekelezaji mzuri zaidi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, rais amemuagiza Kamishna wa TRA kusimamia kwa makini zoezi la ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha kero ndogo ndogo zinazowakabili wananchi zinaanza kushughulikiwa mara moja.
Ameitaka TRA kukusanya mapato toka kwa wafanya biashara wakubwa na wakwepa kodi bila kuogopa mtu wala taasisi yoyote na kusisitiza kuwa hakuna mwenye mamlaka ya kubatilisha maamuzi hayo zaidi yake.
Dk Magufuli ametaka usimamizi mzuri katika suala la manunuzi ya umma ambalo amesema limekuwa likitumika vibaya na kuwa mwanya wa maofisa wasio waaminifu kuiibia serikali kwa kuongeza bei za bidhaa na huduma tofauti na bei halisi ya manunuzi.
MWANANCHI
Mchakato wa uteuzi wa wabunge wake wa viti maalumu wa Bunge la kumi na moja, umeacha simanzi kubwa baada ya orodha iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuonyesha kuwa wabunge 47 wametoswa katika vyama vya CCM, Chadema na CUF huku 33 wakipitishwa tena kuingia ‘mjengoni’.
Katika Bunge la 10 lililomaliza muda wake, CCM ilikuwa na wabunge 67 wa viti maalumu, Chadema 25 na CUF 10, hata hivyo kwa mujibu wa NEC katika uchaguzi wa mwaka huu idadi ya viti maalumu kwa CCM imeshuka hadi 64, Chadema imepanda hadi 36 na CUF ikibaki na viti 10.
Katika orodha hiyo wabunge wapya bungeni kutoka vyama vyote vitatu watakuwa79, CCM ikiwa na 39, Chadema 28 na CUF 10, akiwamo Riziki Lulida ambaye awali alikuwa mbunge wa viti maalumu CCM.
Mchanganuo uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa wabunge 36 wa CCM waliokuwapo katika Bunge la 10 wametoswa, huku 25 waliokuwa katika bunge hilo wakirejea tena.
Mchanganuo unaonyesha kuwa wabunge wanne wa viti maalumu CCM, walijitosa kugombea ubunge majimboni na kuibuka na ushindi ambao ni Mary Chatanda (Korogwe Mjini), Dk Prudenciana Kikwembe (Kavuu), Magreth Sitta (Urambo Mashariki) na Stella Manyanya (Nyasa).
Ester Bulaya alikuwa mbunge wa viti maalumu CCM, lakini alikihama chama hicho na kujiunga na Chadema na kugombea ubunge jimbo la Bunda Mjini na kuibuka mshindi. Anna Abdallah alistaafu siasa.
Baadhi ya wabunge wenye majina makubwa CCM waliotoswa ni Zarina Madabiba ambaye ni mke wa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dar es Salaam, aliyekuwa Naibu Waziri wa wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, Pindi Chana, aliyekuwa mwenyekiti wa Bunge, Lediana Mng’ong’o, Zainabu Kawawa, Diana Chilolo, Sarah Msafiri, Dk Maua Daftari na Ritha Kabati.
Chadema Kwa upande wa Chadema wabunge tisa wa zamani wametemwa ambao ni Christina Lissu, Raya Hamisi, Rebecca Mngodo, Christowaja Mtinda, Maulida Komu, Mwanamrisho Abama, Naomi Kaihula, Rachel Mashishanga na Lucy Owenya. Wabunge wa zamani wa viti maalumu walioteuliwa tena ni Sabrina Sungura, Joyce Mukya, Mariam Msabaha, Susan Lyimo, Cecilia Paresso, Conchestar Rwamlaza, Rose Kamili na Grace Kiwelu.
Chama hicho kimepata sura mpya 28, akiwemo Katibu wa Baraza la Wanawake Chadema (BAWACHA), Grace Tendega na Jesca Kishoa ambaye ni mke wa aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kusini (NCCRMageuzi), David Kafulila.
CUF Kwa upande wa CUF wameteuliwa wabunge tisa wapya ambao ni Riziki Lulida, Mgeni Kadika, Raisa Mussa, Salma Mwassa, Riziki Mngwali, Hadija Ally, Halima Mohammed, Saumu Sakala, Miza Haji pamoja na Savelina Mwijage ambaye alikuwa mbunge wa viti maalumu 20052010. Kati ya wabunge 10 wa zamani wa viti maalumu wa chama hicho, Naibu Katibu MkuuBara, Magdalena Sakaya ndiye mbunge pekee aliyegombea ubunge wa jimbo na kushinda wengine tisa hawakuteuliwa.
HABARILEO
Rais John Magufuli, ametoa agizo mahususi katika usimamizi wa manunuzi ya Serikali, ambayo yamekuwa yakitumika vibaya kwa kugeuzwa mwanya wa kuiibia Serikali.
Ametoa agizo hilo Ikulu jijini Dar es Salaam jana katika kikao chake cha kwanza na watendaji wakuu wa Serikali; wakiwemo makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu, Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Benno Ndulu na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rished Bade.
Katika kikao hicho, Rais Magufuli ameagiza usimamizi katika suala la manunuzi ambalo limekuwa likitumika vibaya kwa watendaji wabadhirifu kununua vitu vya Serikali kwa bei ya juu kuliko bei halisi iliyopo sokoni.
“Ikitokea suala hilo likagundulika kwa watu kuongeza bei ya vitu, watendaji watawajibishwa mara moja,” ameonya Rais Magufuli na kusisitiza kwamba kuwajibishwa huko kutahusu yeyote atakayeongeza bei, hata kama bei iliyoongezwa ni ya vitu vya bei ndogo kabisa katika jamii.*Mkakati wa Magufuli
Kauli za Rais Magufuli katika kikao hicho cha jana na cha juzi alipofanya ziara ya kushtukiza ya Wizara ya Fedha, zimedhihirisha mkakati wake wa kuongeza mapato ya Serikali, kwa kuwa katika vikao vyote hivyo, amesisitiza umuhimu wa kukusanya kodi kwa kila mfanyabiashara mkubwa bila woga.
Mbali na dhamira hiyo ya kuongeza zaidi mapato, agizo la kuchunga manunuzi ya umma, imeonesha dhamira nyingine aliyonayo katika kubana matumizi, kwa kuwa eneo la manunuzi ya umma, ndilo linalochukua asilimia 70 ya matumizi ya Serikali.
Mbali na eneo hilo kuchukua sehemu hiyo kubwa ya mapato ya Serikali, lakini eneo hilo pia limekuwa likiathiriwa zaidi na vitendo vya rushwa hasa katika utoaji wa zabuni za Serikali.
Mkakati huo wa Rais Magufuli, umezidi kudhihirisha dhamira yake aliyotangaza wakati wa kampeni, ya kwenda kuziba mianya ya rushwa na uvujaji wa mapato, ili fedha za Serikali zikatekeleze ahadi zake na kutatua kero za Watanzania wa kipato cha chini.
HABARILEO
Jeshi la Polisi nchini, limezuia maandamano yoyote ya vyama vya siasa mpaka hali itakapotengemaa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Msemaji wa Jeshi hilo, Advera Bulimba, alisema kuna baadhi ya vyama vya siasa vimeomba kufanya mikutano na maandamano nchi nzima.
Alisema tathimini iliyofanywa na vyombo vya usalama hapa nchini inaonyesha kuwa bado kuna mihemko ya kisiasa ndani ya jamii, hivyo mikutano au maandamano ya aina hiyo yakiruhusiwa, yanaweza kusababisha uvunjifu wa amani.
“Hakuna chama chochote kinachoruhusiwa kufanya maandamano au mikutano, tunawaomba sana wajiepushe tutaruhusu mikutano na maandamano baada ya hali kutengemaa,” alisema Bulembo.
Aliongeza kuwa Jeshi la Polisi nchini, linatoa mwito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kama walivyofanya kipindi chote cha uchaguzi, kwa kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani na badala yake waendelee na shughuli zao za kila siku za ujenzi wa taifa.
Kauli hiyo ya jeshi la polisi imekuja baada ya vyama vya siasa ikiwemo Chama cha Demokrasia na Mendeleo (Chadema) na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuandikia jeshi hilo barua ya kutaka kufanya mikutano ya hadhara na maandamano.
HABARILEO
Serikali imesitisha matumizi ya picha ya Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli katika ofisi za umma na wananchi kwa ujumla.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo ilisema awali majira ya saa 6: 00 mchana juzi serikali ilitangaza kuanza rasmi kwa matumizi ya picha ya Rais lakini baadaye ilitoa taarifa ya kusitisha matumizi ya picha hiyo.
“Serikali inapenda kuzitaarifu ofisi za umma na wananchi kwa ujumla kwamba imesitisha matumizi ya picha ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Serikali ya Awamu ya Tano, Dk John Joseph Pombe Magufuli ambayo ilikuwa inauzwa kwa gharama ya shilingi 15,000 mpaka hapo itakapotangazwa tena,” ilisema sehemu ya taaifa hiyo.
MTANZANIA
Mbunge mteule wa Butiama Nimrodi Mkono wa CCM ndiye mwenye umri mkubwa zaidi kuliko wabunge wote waliotangawa na tume ya Taifa ya uchaguzi NEC.
Mkono anashikilia rekodi hiyo ya kuwa mbunge mwenye unri mkubwa kuliko wenzake wote akiwa na umri wa miaka 72 akifariwa na Mbunge wa Urambo Mashariki Margaret Sitta mwenye umri wa miaka 69.
Kwa mujibu wa orodha ya wabunge wa bunge la 11 iliyotolewa jana Mkurugenzi wa NEC Ramadhan Kailima, mbunge menye umri mdogo ni wa jimbo la Kasulu vijijini Holle Vuma kupitia CCM mwenye miaka 25.
Katika Bunge lililopita aliyekuwa Mbunge wa Muhambwe kupitia NCCR, Felix Mkosamali ndiye aliyekuwa na umri mdogo wa miaka 24.
NIPASHE
Bodi ya huduma za maktaba nchini (TLSB) imeanzisha mradi wa maktaba kwa maendeleo, wenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 630 ili kuzijengea uwezo.
Walengwa katika mradi huo ni wajasiriamali, wafugaji, wakulima, wafanyakazi na wafanyabiashara kwa lengo la kuwafundisha namna ya kutumia maktaba katika kupata taarifa muhimu za kuendesha shughuli zao kwa ufanisi.
Mkurugenzi wa Bodi ya Maktaba nchini, Dk. Alli Mcharazo, alisema hayo alipokuwa akitoa taarifa kwa washiriki wa warsha ya umuhimu wa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) na maktaba kwa maendeleo ya Taifa.
Dk. Mcharazo alisema kuwa mradi huo utatumia zaidi teknolojia ya Tehama kwa kutumia maktaba zinazohamishika ambazo zitawafikia walengwa moja kwa moja ambao ni jamii katika maeneo yao ya uzalishaji.
Alisema lengo ni kuiwezesha jamii husika kupata taarifa muhimu katika kuendeleza shughuli zao za kila siku kwa njia ya Tehama kupitia mafunzo yatakayotolewa toka maktaba zilizopo nchini.
Wakutubi wa maktaba Mkoa wa Dodoma, ambao husimamia shughuli za maktaba, walisema mradi huo utatumia zaidi ya teknolojia ya habari na mawasiliano na utasaidia kuboresha huduma za maktaba ambazo mfumo wake wa uendeshaji wa awali ulikuwa ukikabiliwa na ushindani.
Mmoja wa washiriki ambaye ni mjasirimali waliopatiwa mafunzo kuhusu mradi huo Rebeca Ngambile alisema kuwa utawasaidia katika kuongeza ufanisi wa biashara zao ambapo wataweza kuzitangaza kwa njia mtandao wa Tehama.
Naye Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Degratias Yinza, aliwataka washiriki kutumia mafunzo hayo kwa kuongeza mapato zaidi kwa kuwa watakuwa wamejihakikishia kwa kupata taarifa zaidi.
Unataka kutumiwa MSG za habari zote kubwa kutoka kwa Millard Ayo? ukiwa na line ya tiGO andika ‘AYO’ tuma kwenda 15510, msg utayotumiwa jibu OK ili uanze kupokea matukio yote kwa sms, pia ungana na Millard Ayo kwenye Twitter, FB, Instagram na YouTUBE wa kubonyeza hapa >>>INSTAGRAMTWITTERFBYOUTUBE.