MTANZANIA
Mbunge mteule wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe (CCM) amesema waziri mkuu wa Serikali ya awamu ya tano atatokana na uteuzi wa Rais Dk. John Magufuli na kuinidhishwa na Bunge na wala si taarifa zinazozagaa katika mitandao ya kijamii.
Dk. Mwakyembe ambaye, alikuwa Waziri wa Afrika Mashariki katika Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete, ameyasema hayo mjini hapa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, waliotaka kujua namna alivyopokea taarifa za jina lake kutajwa na wananchi kwa nafasi ya waziri mkuu.
Alisema kwa mujibu wa sheria na katiba ya nchi, waziri mkuu anateuliwa na rais ambaye huwasilisha jina hilo kwa Spika wa Bunge na baadaye kupigiwa kura na wabunge.
“Mimi siwezi kuwasemea wananchi na siwezi kusema kuna watu wengi wanasema hivi, kwani nafasi ya uwaziri mkuu haiji kwa njia ya kura ya maoni, wala kwa njia ya mitandao ya kijamii ni nafasi ya uteuzi inayoidhinishwa na Bunge na ni mamlaka ya rais wa nchi,” alisema Dk. Mwakyembe.
Dk. Mwakyembe, aliwataka Watanzania bila kujali itikadi za dini na vyama vyao wamuombee Rais Magufuli, ili aweze kuteua viongozi watakaowajibika na ambao wataendana na kasi yake.
Wabunge kadhaa wamekuwa wakitajwa katika nafasi hiyo ya juu serikalini na kupewa nafasi huenda mmoja wao akawa waziri mkuu katika Serikali hii ya awamu ya tano.
Wengine wanaotajwa ni Mbunge wa Isimani, William Lukuvi, Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo na Mbunge wa Bumbuli January Makamba.
Wakati mjadala ukiwa hivyo, jina la Kachero namba moja mstaafu wa Jeshi la Polisi, Adadi Rajabu, nalo limechipuka kuwa ni miongoni mwa majina ya wanasiasa machachari yanayopewa nafasi kubwa ya kuteuliwa kushika wadhifa huo.
Kachero Rajabu ambaye alistaafu utumishi katika Jeshi la Polisi akiwa na cheo cha Kamishna na baadaye kuteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, aligombea ubunge wa Muheza kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kushinda na hivi sasa anatajwa kuwamo kwenye orodha ya watu ambao Rais John Magufuli anapendezwa na utendaji kazi wake wa kujituma.
Adadi ameingia katika orodha ya wanasiasa wanaofikiriwa kuteuliwa kushika wadhfa huo ambao kiuhalisia ni watendaji zaidi zikiwa zimesalia siku nne kabla Rais Magufuli hajawasilisha jina la waziri mkuu mteule bungeni kwa ajili ya kuidhinishwa na Bunge..
MTANZANIA
Jeshi la Polisi mkoani Mwanza, jana lililazimika kutumia mabomu ya machozi ili kuwatawanya wafuasi zaidi ya 500 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), waliokuwa wamefurika katika Hospitali ya Rufaa Bugando kwa ajili ya kushuhudia mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Geita marehemu Alfonce Mawazo ambaye alifariki dunia kwa kukatwa mapanga.
Mawazo alifariki juzi katika mazingira ya kutatanisha huku kifo chake kikihusishwa na masuala ya kisiasa.
Wafuasi hao wa Chadema kutoka katika mikoa kadhaa ya Kanda ya Ziwa, walifika hospitalini hapo wakiwa katika msafara wa magari zaidi ya 50.
Mwili wa marehemu Mawazo ulihamishiwa hospitalini hapo kutoka mkaoni Geita, huku ukisindikizwa na wafuasi wa Chadema ambao waliungana na wenzao wa Mkoa wa Mwanza.
Msafara huo wa kusindikiza mwili huo uliwasili Hospitali ya Bugando saa 10 jioni lakini msafara huo ulijikuta ukikwama baada ya walinzi wa hospitali hiyo kuzuia magari mengine, huku wakitoa maelekezo ya kuruhusu magari mawili tu kwa ajili ya kuhifadhi maiti.
Kutokana na maelekezo hayo ya mofisa usalama wa hospitali wafuasi hao wa Chadema waligoma na kutaka magari yote yaruhusiwe kuingia katika eneo la hospitali hali iliyowafanya walinzi hao kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi.
Baada ya dakika chache Polisi walifika katika eneo hilo na kuwataka wafuasi hao kuondoka katika eneo hilo kwani wanaleta usumbufu kwa wagonjwa kutokana na kelele walizokuwa wakipiga, ambapo wengine walikuwa wakiimba nyimbo za Chadema.
Pamoja na jitihada za Polisi kuwataka wafuasi hao wa Chadema kuondoka katika eneo hilo, juhudi zao ziligonga mwamba na kuwalazimu kufyatua mabomu ya machozi ili kuwatanya wafuasi hao waliokuwa wamejaa katika eneo hilo la hospitali.
Kutokana na vurugu hizo MTANZANIA ilimtafuta kwa njia ya simu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo, lakini hakuweza kupatikana huku simu yake ya mkononi ikiita muda mrefu bila majibu.
Mkuu wa Upelelezi wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Augustine Senga, alisema Jeshi la Polisi lililazimika kutumia mabomu ya machozi ili kuwatawanya wafuasi hao wa Chadema, kutokana na vurugu zilizokuwapo.
“Tumefanikiwa kudhibiti vurugu hizo ni suala la kutokuelewa tu, taratibu za hospitali ya rufaa ya Bugando ziko wazi, walitaka kulazimisha vitu ambavyo haviwezekani, tumewakamata baadhi yao tunaendelea na mahojiano,” alisema RCO Senga.
Marehemu Mawazo alikuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Busanda kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alifariki dunia baada ya kushambuliwa kwa mapanga na shoka katika eneo la Katoro wilayani Geita na watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa CCM.
Mawazo alikutwa na mauti saa tisa alasiri juzi akiwa anatibiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita baada ya kushambuliwa alipokwenda kwa ajili mkutano wa kampeni ya udiwani wa Kata ya Ludete.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Latson Mponjoli, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, lakini hakutaka kutoa maelezo zaidi kwa madai kuwa alikuwa akielekea eneo la tukio, lakini kwa mujibu wa mashuhuda, Mawazo alishambuliwa saa tano asubuhi.
Ilidaiwa kuwa kabla ya kwenda katika mkutano wa kampeni, Mawazo alikuwa kikaoni Mjini Katoro na baada ya kumalizika kwa kikao hicho kilichokuwa cha ndani aliondoka kuelekea Ludete, lakini akiwa njiani ndipo alipovamiwa na kundi la vijana hao na kuanza kushambulia msafara wake na yeye kujeruhiwa vibaya.
MTANZANIA
Waziri mkuu wa zamani na aliyekuwa mgombea urais kupitia Chadema, Edward Lowassa, amesema ataendelea kupambana katika siasa na kwamba yawezekana ameshindwa katika pambano lakini si vita.
Lowassa aliyasema hayo jana katika mkutano na waandishi wa habari, baada ya kuulizwa nini hatima yake ya kisiasa baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, ambapo Rais Dk. John Magufuli aliibuka mshindi.
Akijibu swali hilo, Lowassa alisema. “Nitaendelea kuwa active (imara) kwenye siasa, I might lost the battle but not the war ‘yawezekana nimeshindwa pambano lakini si vita,” alisema Lowassa.
Lowassa ambaye katika uchaguzi huo alikuwa mshindi wa pili kwa kupata kura 6,072,848 sawa na asilimia 39.97 nyuma ya Rais Magufuli aliyeshinda kwa kura 8,882,935 sawa na asilimia 58.46.
Kutokana na hali hiyo alisema ataendelea kuipinga Serikali hadi pale watakapoelewana.
Bila kusema ni mbinu gani atatumia kutimiza azma hiyo, alisema kila kitu kitaonekana muda utakapofika kwani hawezi kutoa silaha zake zote kabla ya vita.
Pia waandishi walipotaka kujua endapo wabunge wanaotokana na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) watahudhuria siku Dk. Magufuli atakapohutubia Bunge, alisema. ‘tutavuka daraka tukilifikia’ akimaanisha kuwa kitu kitakachofanywa na wabunge wa Ukawa kitaonekana siku hiyo.
Alisema Ukawa, utaendelea kuwataka Watanzania wakatae matokeo batili ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania bara na kuendelea kuwa watulivu.
Alisema umoja huo una ushahidi wa kutosha kuonyesha jinsi matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano yalivyochakachuliwa na kiasi cha kura zilizoibwa.
“Wakati mwafaka tutaweka bayana ushahidi huo ili Watanzania wajue kwa nini Ukawa inasema kwa dhati kuwa haitambui matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi na kwa nini haitashirikiana na Serikali ya sasa ambayo ni batili kisheria.
“Kama sheria ingeturuhusu tungekuwa mahakamani kupinga uamuzi wa Tume ya Uchaguzi. Uamuzi huo umetekelezwa tu kwa sababu ya fitna ya sheria mbovu zilizotungwa kuhakikisha CCM inabaki madarakani milele. Hii lazma tuendelee kuikataa na kuipinga kwa nguvu zetu zote.
“…Ukawa itaendeleza harakati za kisiasa katika nyanja mbalimbali ili kutekeleza azma ya kuleta mabadiliko ya kweli nchini,” alisema Lowassa wakati akisoma tamko la umoja huo.
Alisema umoja huo utaendelea pia kudai Katiba ya wananchi itakayohakikisha kuwa Tanzania inakuwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Serikali inayowajibika kwa umma.
“Ni wazi kuwa uchaguzi mwingine katika mazingira ya sasa na chini ya Katiba ya sasa hauwezi kuzaa matunda tofauti. Bila Katiba mpya ya wananchi, Tanzania haitakuwa na demokrasia na itaendelea kuwa nchi inayotawaliwa kwa mizengwe na udikteta wa CCM,” alisema.
Lowassa pia alizungumzia hali ya mambo visiwani Zanzibar hasa baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi.
Suala hilo ndilo lilikuwa ajenda kubwa ya mkutano huo na waandishi wa habari, ambapo Lowassa alisema. “Wakuu wa Ukawa kwa kauli moja walikariri tamko lao la kumuunga mkono kwa dhati Maalim Seif Sharif Hamad kwa ushindi wake dhahiri na kuitaka Tume ya Uchaguzi Zanzibar imtangaze kuwa Rais wa Zanzibar mara moja,” alisema.
Alisema katika mkutano wa viongozi hao uliofanyika Novemba 9, mwaka huu jijini Dar es Salaam, walilaani vikali uamuzi wa ZEC kufuta uchaguzi halali na kuonya mbinu mpya za kutaka uchaguzi urudiwe hazikubaliki na zitahatarisha amani na utulivu wa Zanzibar.
“Viongozi wa Ukawa walimpongeza Maalim Seif na viongozi wote wa CUF Zanzibar kwa busara na ustahimilivu wao mkubwa na jitihada zao zinazoendelea kulinda amani,”alisema Lowassa.
Alisema kinyume na Tanzania bara, uchaguzi wa Zanzibar ulikuwa wa wazi na wa amani kwani vyama vyote vya siasa na hata wawakilishi wa kimataifa walikiri hivyo mpaka pale ilipobainika CCM inashindwa.
“Wakuu wa Ukawa walikataa dhana kuwa uchaguzi ule ule unaodaiwa kufutwa kwa kuwa ulikuwa na mizengwe, ulizaa matokeo halali kwa wabunge Bunge la Jamhuri ya Muungano na urais wa jamhuri, lakini batili kwa wajumbe la Baraza la Wawakilishi na Rais wa Zanzibar. Dhana hii haina mantiki yoyote bali ni ubabe wa kisiasa tu.
“Haiwezekani chungu kimoja kikapika halali na haramu kwa pamoja. Kwa kigezo cha ZEC kuwa uchaguzi wa Zanzibar ulikuwa batili basi matokeo yake yote ikiwa ni pamoja na yale ya Rais wa Jamhuri ya Muungano pia ni batili.
MTANZANIA
Msichana mmoja amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Singida, baada ya kumwagiwa maharage ya moto kifuani na dada yake, kwa kile kinachodaiwa kuwa ni wivu wa kimapenzi.
Msichana huyo aliyelazwa wodi namba mbili katika hospitali hiyo, ametambulika kwa jina la Tabu Mohamed (25) ni mkazi wa eneo la Majengo Manispaa ya Singida.
Akizungumza na MTANZANIA huku akiugulia maumivu, Tabu alisema tukio hilo lilitokea juzi asubuhi, wakati alipokwenda kwa dada yake kwa lengo la kumwomba simu ili atumie kujaza vocha ya kumtumia mama yao.
Hata hivyo alisema katika hali ya kushangaza dada yake huyo aitwae Rehema Jumanne (32), baada ya ombi hilo, hakumjibu chochote na badala yake aliingia jikoni na kupakua maharage ya moto kisha akamwagia.
“Mimi namshangaa dada yangu, ananinunia tu bila sababu yoyote, nikimwuliza hata hasemi chochote, na mimi nimeamua kumwacha kama alivyo,”alisema Tabu bila kuweka wazi sababu ya ugomvi wao.
Kwa upande wake mganga wa zamu aliyemhudumia majeruhi huyo, Dk. Amri Mabelwa, alisema hali ya mgonjwa huyo inaendelea vizuri ingawa amekuwa na majereha mwilini.
Kamanda wa polisi Mkoani Singida Thobias Sedoyeka, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo alisema tayari Jeshi la Polisi linamshikilia mtuhumiwa RehemaJumanne, ambaye anadaiwa kuhusika na tukio hilo.
Kamanda Sedoyeka alisema mtuhumiwa akiwa amesimama nyuma ya mdogo wake huyo, ghafla alimwagia maharage hayo kifuani na kumwunguza vibaya sehemu ya shingoni, kifuani na kwenye matiti yake.
“Msichana huyu ameunguzwa vibaya sana kifuani…hadi sasa amelazwa hospitali ya mkoa, wodi namba mbili na madaktari wanaendelea kumtibu,” alisema Kamanda Sedoyeka.
NIPASHE
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mwantumu Mahiza (pichani), amewaambia watendaji wa serikali wilayani Muheza kuwa kama watashindwa kwenda na falsafa ya `Hapa kazi tu’, ya kuwaletea wananchi maendeleo, wafungashe virago mapema.
Mahiza aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na maofisa watendaji wakiwamo wakuu wa idara, viongozi wa dini, vyama vya siasa na madiwani wateule wa Wilaya ya Muheza mjini hapa mwishoni mwa wiki.
Alikuwa akifanya majumuisho ya ziara yake ya siku moja aliyoifanya wilayani Muheza mwishoni mwa wiki.
Alisema kuwa kama mtendaji wa serikali katika Mkoa wa Tanga hataweza kuwaletea maendeleo wananchi, atakuwa hafai na aondoke kwani njia nyeupe.
Mahiza alisema atahakikisha anatembelea kata zote katika halmashauri ya Mkoa wa Tanga kuhakikisha kwamba kila mtendaji anawajibika ipasavyo.
Alisema kuwa lazima watendaji wajipange wapate maendeleo ya uhakikia katika wilaya ya Muheza kuhakikisha wananchi wanakuwa kiuchumi katika wilaya ya Muheza na mkoa mzima kwa ujumla kwa kuwa wanalipwa mshahara na serikali.
Aidha, aliwataka viongozi wa dini kwenda kuwaombea vijana ili waache kukaa vijiweni kwani wazee wamechoka sasa na wanawategemea vijana.
NIPASHE
Spika mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Pius Msekwa (pichani), amesema Spika wa Bunge la 11 anatakiwa awe muadilifu, mwenye busara na atakayeendesha vikao kwa kufuata kanuni na taratibu za Bunge.
Amesema wabunge wanaoingia kwa mara ya kwanza bungeni na wazoefu wanapaswa kuzisoma na kuzielewa kanuni na taratibu za Bunge ili kuepusha mabishano bungeni.
Msekwa aliyasema hayo mwishoni mwa wiki katika kipindi cha Nipashe kunachorushwa na Radio One Stereo.
Alisema Bunge la 11 litakuwa ni Bunge lenye vijana zaidi pamoja na idadi kubwa ya wabunge wa upinzani, hivyo anahitajika Spika mahiri.
Alisema Bunge la 10 lililopita lilikuwa na changamoto ya mabishano kutokana na baadhi ya wabunge kutozifahamu kanuni na kwamba Bunge si mahali pa mabishano.
“Nilikuwa Spika kwa zaidi ya miaka 10, kila Bunge lina vijana, lakini zaidi itakuwa hivi sasa, hawatakiwi wabunge kuleta mabishano kiongozi wa Bunge ni mmoja tu Spika, wamsikilize, wazisome kanuni na kuzielewa,” alisisitiza na kuongeza.
“Wala si maadili kuleta mabishano bungeni. Wabunge wazoefu na wanaoingia kwa mara ya kwanza waziheshimu kanuni na taratibu za Bunge.”
NIPASHE
Mtaalam wa upasuaji wa uti wa mgongo na magonjwa ya mfumo wa fahamu kutoka Hospitali za Apollo, India, amewasili jijini Dar es Salaam na kuendesha huduma hizo.
Tanzania ni moja ya nchi ambazo ina uhaba mkubwa wa madaktari bingwa wa mfumo wa fahamu kitendo kinachosababisha nchi kupoteza fedha nyingi kwa kuwapeleka wagonjwa wa matatizo ya aina hiyo nje ya nchi kupata matibabu na ushauri.
Inakadiriwa kuwa watoto wachanga 1,000 kati 4,000 wanaozaliwa na tatizo la mfumo wa fahamu, hupatiwa matibabu huku wengine 3,000 wakishindwa kupatiwa huduma hiyo.
Kutokana na hali hiyo, Hospitali ya Apollo imemleta nchini daktari bingwa wa upasuaji wa uti wa mgongo na mfumo wa fahamu ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Upasuaji wa magonjwa ya fahamu katika hospitali hiyo, Dk. Alok Ranjan, ambaye atakuwa akitoa huduma na kuwaona wagonjwa wake aliowafanyia upasuaji siku za nyuma.
Nao baadhi ya wagonjwa waliofika katika kliniki hiyo inayofanyikia katika Hospitali ya Hindu Mandal jijini Dar es Salaam, wameiomba serikali kuhakikisha kwamba inasaidia gharama za matibabu ya watu wanaosafiri nje ya nchi kufuata matibabu ya magonjwa mbalimbali.
Wamezitaka pia kampuni za bima ya afya kuhudumia wateja wake katika hospitali za kimataifa badala ya kujikita katika hospitali za hapa nchini pekee.
Katika mkutano huo na waandishi wa habari ulofanyika Hospitali ya Hindu Mandal jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Dk. Ranjan, amewashauri Watanzania kubadilisha mtindo wa maisha ili kuepukana na magonjwa ya mfumo wa fahamu na uti wa mgongo.
Alisema kwa watu wazima ugonjwa huu mara nyingi husababishwa na ukaaji mbaya ambao hudhuru uti wa mgongo, trauma, shinikizo la damu, ajali, kisukari, uzito wa kupitiliza na sababu nyinginezo.
Tanzania kwa sasa inakadiriwa kuwa na madaktari saba wa mfumo wa fahamu ambao wote kwa sasa ni watendaji katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
HABARILEO
Benki ya Maendeleo ya TIB na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, zimeingia makubaliano ya kuuendeleza ufukwe wa Oysterbay maarufu Coco Beach. Mradi huo uliopewa jina la ‘Oysterbay Beach Development’ unalenga kuufanya ufukwe huo kuwa wa kisasa na hivyo kuchangia uchumi wa Manispaa hiyo na nchi kwa ujumla.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mradi huo jana, Mkurugenzi wa benki hiyo, Peter Noni alisema, wametoa mchango wa dola za Marekani 40,000 sawa na Sh mil 86 kwa ajili ya kuendeleza ufukwe huo.
Alisema, kiasi hicho cha pesa hawakitoi kama mkopo, bali kimetolewa kama utekelezaji wa majukumu yao ya ushirikiano na jamii kwa kufanya jambo ambalo litawanufaisha wananchi wengi.
Noni alisema mradi huo ambao kwa sasa umemalizika katika hatua za awali za ubunifu wa miundombinu umegharimu Sh mil 260, ambapo mbali na kuchangia uchumi pia utasaidia kuongeza ajira kwa vijana na idadi ya watalii watakaotembelea ufukwe huo.
“Baada ya kupita kwa hatua hizi miundombinu yake itagharimu Sh bilioni sita, tunatarajia ufukwe huu kuwa na maeneo ya maduka, migahawa ya vyakula, maegesho ya magari na maeneo ya michezo ya watoto, lengo ni kuufanya kuwa ufukwe wa kisasa,” Noni alisema.
Aidha, alisema washirika wengine ambao wameonesha nia ya kusaidia mradi huo ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambalo limetoa Sh mil 86 na Shirika la Ukuzaji wa Mitaji la Umoja wa Mataifa (UNCDF), huku manispaa hiyo ikitoa dola za Marekani 30,000 kwa ajili ya mradi huo.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Mhandisi Mussa Natty alisema walianza mradi huo baada ya kuiomba benki hiyo kushiriki katika kuendeleza eneo hilo la ufukwe wa Coco.
Alisema, mradi huo tayari umepitia katika hatua mbalimbali ambapo sasa wanaupeleka kwa wananchi na wadau wengine ili watoe maoni yao kama mwongozo wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi unavyotaka.
Natty alisema wameamua kuendeleza ufukwe huo ili kuweza kuingiza mapato ambapo alisema, katika nchi mbalimbali zikiwemo za Afrika, ufukwe umekuwa ukiongeza mapato ya serikali na sehemu ya kuongeza ajira kwa vijana, jambo ambalo wanataka lifanyike hapa.
Hata hivyo, alisema manispaa hiyo inataka ufukwe huo kuendelea kubaki kuwa wa umma kwa watu kuingia bila malipo isipokuwa watakapohitaji kutumia huduma zitakazokuwepo.
Alisema, ufukwe huo baada ya kukamilikia utakuwa na faida kubwa ya kiuchumi kwani kutakuwa na maeneo yanayomilikiwa na Manispaa hiyo na machache yatamilikiwa na wawekezaji.
“Faida itakuwa kubwa mno kwa yale maeneo ambayo yatamilikiwa na halmashauri fedha zitakazokuwa zinapatikana zitakuwa zinarudi kwa jamii kwa kuwajengea miundombinu, madawati na vitu vingine vya muhimu,” Natty alisema.
Alisema, ufukwe huo baada ya kukamilika utakuwa na mchango mkubwa kwa nchi na manispaa hiyo kwa ujumla. Alisema wanakadiria nusu ya bajeti ya manispaa hiyo itatokana na ufukwe huo ambao unakadiriwa kuingiza Sh bil 17 kwa mwaka.
HABARILEO
Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imemaliza kazi yake na sasa mgombea nafasi ya Spika kupitia chama hicho ni ama Job Ndugai, Abdullah Ali Mwinyi au Dk Tulia Ackson Mwansasu.
Pia Kamati Kuu imesema utaratibu iliotangaza awali wa namna ya kumpata Naibu Spika haukuzingatia Katiba na suala hilo linapaswa kushughulikiwa na Kamati ya Wabunge wa CCM, hivyo leo wataanza kutoa fomu kwa waombaji wa nafasi hiyo. Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati Kuu chini ya Mwenyekiti wa Taifa, Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Nape Nnauye alisema pia leo Kamati ya Wabunge wa CCM itapiga kura kuchagua jina moja kati ya hayo matatu yaliyoteuliwa jana.
Ndugai (55) ni Naibu Spika katika Bunge la 10 lililomaliza muda wake chini ya Spika Anne Makinda akishika nafasi hiyo tangu mwaka 2010. Amekuwa Mbunge wa Jimbo la Kongwa mkoani Dodoma tangu mwaka 2000 na alishinda tena katika uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka huu. Alitajwa kuwa mbunge mwenye mchango mkubwa katika Bunge la Tisa.
Dk Tulia aliyezaliwa Novemba 23, 1976 wilayani Tukuyu mkoani Mbeya, ni Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliyeteuliwa kushika wadhifa huo na Rais mstaafu Kikwete, Septemba 9, mwaka huu. Alikuwa Mjumbe wa Bunge la Katiba na ni mtaalamu katika sheria za hifadhi za jamii, kazi, uhifadhi wanyamapori, udhamini, sheria ya usimamizi wa mirathi, ufadhili miradi na madini.
Abdullah, ambaye ni mtoto wa Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi maarufu Mzee Ruksa, ni Mbunge wa Afrika Mashariki tangu mwaka 2007. Aliwania ubunge ndani ya CCM katika Jimbo la Kigamboni mwaka huu, lakini kura hazikutosha kumfanya apitishwe kupeperusha bendera.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuchukua fomu hizo wiki hii Dar es Salaam, Ndugai alisema ameamua kuwania nafasi hiyo kutokana na ukweli kuwa Bunge la 11 ni Bunge litakalokuwa na changamoto hivyo linahitaji Spika mwenye weledi, uvumilivu na uzoefu wa kutosha katika mambo ya kuongoza Bunge.
“Jina hilo moja litakalopitishwa, ndilo litakalopelekwa bungeni kwa ajili ya kupigiwa kura kuwania Uspika kwa tiketi ya CCM,” alisema Nape na kukataa kutaja vigezo walivyotumia kupata wateule watatu kati ya zaidi ya 20 walioomba nafasi hiyo zaidi ya kusisitiza wote ni wanachama wa CCM.
Wagombea wengine wa nafasi ya Spika ambao majina yao yameshindwa kupenya kwenye Kamati Kuu ni aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta, Mbunge wa zamani wa Mbulu ambaye amepata kuwa Waziri katika Awamu ya Kwanza ya Serikali ya Awamu ya Nne na pia aliyepata kuwa Balozi, Philip Marmo. Sitta alikuwa Spika wa Bunge la Tisa akijinasibu kuwa Spika wa Viwango na Kasi, lakini akakatwa mwaka 2010 alipojaribu kuwania tena kiti hicho.
Hii ni mara ya pili lake kutopitishwa kuwania kiti hicho, na mwaka huu hakuwania tena ubunge jimboni kwake Urambo Mashariki. Wengine waliokatwa ni Mbunge mteule wa Chato, Dk Medard Kalemani, Diwani wa Goba jijini Dar es Salaam, Mwakalika Watson, Julius Pawatila, Agnes Makune, aliyewahi kuwa Naibu Waziri, Ritha Mlaki na mhitimu wa chuo kikuu mwenye umri wa miaka 28, Veraikunda Urio na Meya wa zamani wa Dar es Salaam, Didas Masaburi.
Pia walikuwamo aliyekuwa Mbunge wa Karagwe, Gosbert Blandes na aliyekuwa mmoja wa wagombea takribani 42 waliojitokeza kuwania nafasi ya Urais ndani ya CCM, Dk Kalokola Muzzamil Mbunge wa zamani wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi; Balozi wa zamani wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu, Mbunge wa zamani wa Afrika Mashariki, George Nangale, Simon Rubugu, Banda Sonoko na Leonce Mulenda.
Ada ya fomu hiyo itakuwa Sh 100,000 tu ambazo zitalipwa wakati mgombea anarudisha fomu kwa Katibu wa Kamati,” alisema Nnauye. Alieleza kutokana na hali hiyo wabunge wanaotaka kuwania nafasi hiyo watachukua fomu kuanzia leo kwa Katibu wa Kamati ya Wabunge wa CCM na mwisho wa kuirudisha ni kesho saa kumi alasiri, ambapo kutafanyika Uchaguzi wa Naibu Spika utakaofanywa na kamati ya wabunge wa CCM.
Kabla ya uamuzi huo wa Kamati Kuu, mgombea pekee aliyekuwa amejaza fomu kuwania nafasi hiyo alikuwa Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu. Akizungumzia vyama vingine kuhusu nafasi ya Spika, Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Ramadhani Kailima alisema majina ya watu 23 kutoka vyama sita vya siasa nchini yalipelekwa kwao yakiwemo kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa wale wasio wabunge.
“Kwa taratibu sisi tunatakiwa kuangalia wagombea uspika ambao sio wabunge kama wana sifa za kuwa wabunge, na tumepitia wasifu wa majina yote 23 tuliyoletewa na vyama na tumeona wana sifa za kuwa wabunge,” alisema Kailima na kuongeza: “Baada ya kukamilisha kwa upande wetu, tumeshamuandikia Katibu wa Bunge kutaka vyama viendelee na taratibu zao na kuwa wote wana sifa,” alisema.
Kailima alisema kati ya majina hayo 23, 17 walipelekwa na CCM, mmoja na Chadema, CHAUMMA ikitoa majina mawili, NRA, TLP na DP kila kimoja kimetoa mtu mmoja. Kwa mujibu wa Kanuni ya 9(4) ya Kanuni za Bunge inataka wagombea nafasi ya uspika wasio wabunge, vyama vinatakiwa kupeleka majina kwa NEC ili kuangalia kama watu hao wana sifa za kuwa wabunge. Imeandikwa na Amir Mhando, Dodoma na Anastazia Anyimike, Dar.
MWANANCHI
Wachimbaji wadogo wa madini katika machimbo ya Nyangalata wilayani Kahama, wameingiwa na hofu baada ya uvumi kwamba wenzao sita kati ya saba waliofukiwa na kifusi siku 42 zilizopita bado wapo hai.
Hali hiyo ya hofu iliibua upya tukio hilo na kusababisha waokoaji na watoa huduma kutoka kikosi cha uokoaji kuanza kazi ya kufukua shimo walimofukiwa wachimbaji hao, wakiwa na imani kwamba ni wazima.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyangalata, Abdul Komba alisema hali hiyo iliibuka baada ya wachimbaji kwenye mashimo jirani na shimo husika walipodai kuwa watu hao wapo hai na kwamba, walipokuwa shimoni walisikia wakizungumza.
“Mpaka sasa watu wapo wengi sana wakijaribu kufukua kupitia mashimo jirani na kila anayeingia chini anarudi na kudai amewasikia wakiongea na kuwa walipojaribu kuwasemesha waliwajibu,” alisema Komba.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Vita Kawawa alisema anafuatilia suala hilo ili kujua ukweli wake, ingawa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha alisema halina ukweli licha ya kutaka ufuatiliaji zaidi ufanyike.
Mwanzoni mwa Oktoba, mwaka huu mashimo katika mgodi huo yalititia na kusababisha vifo vya watu saba ambao walikuwa wameingia ndani kwa lengo la kuwaokoa wenzao waliokuwa wamefunikwa na kifusi.
Baada ya kuwaokoa wenzao, wachimbaji hao walipatwa na mkasa huo kutokana na kukatika kwa kifusi kingine kilichowafunika hadi leo. Kufuatia hali hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mgodi wa Shigomico, Hamza Tandiko alisema kwa mujibu wa wataalamu wa uokoaji kutoka mgodi wa Bulyanhulu, wachimbaji hao walifukiwa umbali wa mita 100.
Tandiko alisema kuwafukua kulihitaji gharama kubwa, lakini baada ya tukio la juzi la kudaiwa wapo hai, waokoaji wameanza upya ufukuaji kwa njia za kienyeji kuwatafuta chini ya mashimo hayo.
Aliyekuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Kitwanga alipotembelea eneo hilo alisema kuwatoa watu hao ardhini ni kazi ngumu inayohitaji mitambo mikubwa yenye uwezo wa kufukua eneo lote la mgodi ili kuwafikia.
Alisema kutokana na changamoto iliyopo, kazi hiyo ingehitaji muda mrefu na wataalamu zaidi.
MWANANCHI
Polisi mkoani Geita wanawashikilia watu wanne kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Mwenyekiti wa Chadema mkoani humo, Alphonce Mawazo.
Mawazo alishambuliwa juzi na watu wasiojulikana katika Kijiji cha Katoro, Geita muda mfupi baada ya kutoka kwenye kikao cha ndani cha ya maandalizi ya uchaguzi wa diwani wa Kata ya Ludete.
Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Mponjoli Mwabulambo alisema watu hao wamekatwa kwa kuhusishwa na mauaji hayo yaliyofanyika juzi saa 12.45 mchana katika eneo la Ludete A.
Mwabulambo alisema siku ya tukio kabla ya mauaji hayo, wafuasi wa Chadema walikuwa na kikao cha ndani katika eneo la Ludete B huku wenzao wa CCM wakiwa na kikao eneo la Ludete A.
“Hawa wa Chadema walivyokuwa kwenye kikao aliingia mtu akamnong’oneza Mawazo, hali iliyozua hofu kwa wengine na walipotoka nje wakakutana na kundi la watu na hapo kukazuka tafrani iliyosababisha watu wawili kujeruhiwa,” alisema.
Kamanda alidai kuwa haieleweki Mawazo alitokaje katika eneo walilokuwa wanafanyia kikao, lakini baada ya muda mfupi, wafuasi wa Chadema walipata taarifa kuwa yupo eneo la Ludete A karibu na ofisi za CCM na hali yake ni mbaya.
Alisema inadaiwa watu waliompiga Mawazo ni kundi la watu zaidi ya 10 na polisi wanaendelea na uchunguzi kuwabaini watu hao na chanzo cha mauaji hayo.
Unataka kutumiwa MSG za habari zote kubwa kutoka kwa Millard Ayo? ukiwa na line ya tiGO andika ‘AYO’ tuma kwenda 15510, msg utayotumiwa jibu OK ili uanze kupokea matukio yote kwa sms, pia ungana na Millard Ayo kwenye Twitter, FB, Instagram na YouTUBE wa kubonyeza hapa >>>INSTAGRAMTWITTERFBYOUTUBE.