NIPASHE
Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Mohamed Enterprises, Mohamed Dewji maarufu kama MO, ameshinda tuzo ya “Mtu wa Mwaka” wa jarida maarufu la Fobes katika hafla zilizofanyika jijini, Johanesburg nchini Afrika Kusini.
Katika shindano hilo, Dewji alishindanishwa katika hatua ya mwisho na mke wa Rais wa Afrika Kusini ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Nkosazana Dlamini Zuma, Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari( aliyeanzisha vita dhidi ya rushwa).
Wengine waliokuwamo katika shindano hilo ni pamoja na Mwandishi maarufu wa vitabu wa Nigeria, Chimanda Ngozi Adichie, ambaye moja ya vitabu vyake vinaelezea picha halisi ya Afrika inavyofikiriwa duniani na Arumna Otei wa Nigeria pia ambaye ni makamu wa Rais wa benki ya Dunia.
Mara baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo, Dewji alisema tuzo hiyo anaielekezea kwa vijana wote wa Kitanzania kwani ndio nguvu kazi ya nchi katika kuubeba uchumi wa nchi.
Alisema tuzo hiyo si ya mkewe, baba, mama wala familia yao bali ni kwa Watanzania ambao wengi wao, wana ajira kupitia kampuni yake ama mashambani.
“Heshima yangu kubwa haitokani na utajiri, maana kama utajiri wako hauna msaada wala kugusa watu maskini hauna maana yeyote, hivyo basi heshima hii ni kutokana na kwanza bidhaa zangu kugusa maisha ya watu kila siku kuanzia sukari na majani ya chai asubuhi pamoja na unga wa ngano, lakini pia chakula cha mchana kwa unga wa sembe, mafuata ya kupikia na maji ya kunywa, bidhaa zote hizo za Mohammed Enterprises zinagusa maisha kila nyakati katika siku,” Dewji.
Alisema utajiri wake unaoonekana, umekuwa kwa kasi kubwa katika kipindi kifupi na hiyo ni kutokana na kufanya kazi sana tena kwa kisasa zaidi na kwamba kampuni zake zimekuwa zikifanya kazi kwa teknolojia ya juu ili kuendana na ushindani wa kibiashara unaobadilika kila siku.
NIPASHE
Polisi mkoani Ruvuma inamshikilia Amani Hyera, mkazi wa kijiji cha Kikunja wilayani Songea kwa tuhuma za kuwaua watu watatu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela, alisema tukio hilo limetokea juzi.
Alisema siku ya tukio Mkuu wa polisi wa Wilaya ya Songea akiwa ofisini kwake, alipokea taarifa ya mauaji ya watu watatu.
Alisema anayedaiwa kufanya mauaji hayo ni Hyera, mkazi wa kijiji cha Kikunja.
Alisema mtu huyo anadaiwa kuwaua watoto wawili na mama yao kwa kuwakatakata mapanga kwa kile kilichosadikiwa kuwa ni wivu wa mapenzi.
Alisema baada ya kufanya mauaji hayo, alijaribu kujiua kwa kujikata na panga shingoni, lakini hakufanikiwa kutokana na wananchi kufika kwenye eneo hilo la tukio na kumdhibiti.
Kamanda Msikhela alisema mtuhumiwa anaendelea kupata matibabu na taratibu za kisheria zinafuata mara tu baada ya afya yake kuimarika.
Aliwataja waliouawa katika tukio hilo kuwa ni Ester Kadege (48), ambaye ni mama mzazi wa watoto waliouawa, Edson Msuha (6) na Kazed Kadege (13).
Alisema marehemu Ester alikuwa na watoto wawili ambao walizaliwa kwa baba tofauti ambapo uchunguzi wa awali wa polisi umebaini kuwa mtuhumiwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na Ester na baadaye waliachana kufuatia Ester kudai kuwa ameokoka na kwamba hataki tena masuala ya kimapenzi.
NIPASHE
Serikali imesema bado wanakabiliwa na tatizo la uvuvi haramu hali inayosababisha samaki kutoweka katika maeneo yenye uvuvi.
Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Yohana Budeba, wakati wa mkutano wa utoaji tuzo kwa wajasiriamali wanaofanya shughuli za uvuvi na usindikaji salama wa bidhaa zao.
Alisema kuwa matumizi ya uvuvi haramu umeongezeka kwa kasi licha ya kwamba kuna sheria ambayo inakataza.
Dk. Budeba alisema sheria ya uvuvi inaelekeza nyavu zinazotakiwa kutumika katika kuvua samaki, lakini matokeo yake wavuvi hao wamekuwa wakitumia nyavu ambazo haziruhusiwi.
Alisema wavuvi hao wamekuwa wakivuna hadi mazalia ya samaki hali ambayo inasababisha kupotea kwa samaki katika maeneo yanayotumika kwa shughuli za uvuvi.
“Uvuvi haramu umeongezeka sana kwani wanatumia nyavu ndogo sheria ya uvuvi inaelekeza nyavu ziwe na macho ya aina gani hawa wanatumia chandarua ya kuzuia mbua kuvulia samaki, “alisema.
Aidha alisema mbali na changamoto hiyo, kumekuwa na idadi kubwa ya wavuvi wa samaki ambao hawaendani na hali halisi ya samaki waliopo.
Alisema kila anayepata mkopo anataka kuwekeza kwenye uvuvi bila kufikiria biashara nyingine na kusababisha idadi ya wavuvi kuongezeka.
“Wavuvi kuwa wengi nayo ni changamoto kwa upande wetu waliopo hawaendani na wingi wa samaki unajua mtu akipata mkopo wake ama akistaafu kazi wanakimbilia kuwekeza kwenye uvuvi, “alisema.
Alisema kupotea kwa dagaa wa Kigoma imesababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa kwani maeneo mengine ya uvuvi yamekuwa makame.
Naye Mkurugenzi wa Maendeleo, Hosea Mbirinyi, alisema kukosekana kwa sheria inayowaongoza katika nchi nne ambazo zinaizunguka ziwa Tanganyika ni chanzo cha kuendelea kuwapo kwa uvuvi haramu.
Alisema wavuvi haramu huama kutoka eneo moja na kwenda eneo jingine wakifanya uvuvi kwa kukiuka sheria.
Aidha alisema kuna wavuvi ambao huvua dagaa kwa kutumia jenereta kwa ajili ya kuwasha taa ili wapate samaki wengi jambo ambalo halitakiwi.
Alisema nchi hizo nne zikikaa kwa pamoja na kuweka mikakati itasaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti uvuvi haramu pamoja na kuwapo kwa ulinzi.
Naye Fatuma Katula ambaye anajishughulisha na ujasiriamali wa kuuza dagaa, alisema changamoto kubwa ambayo inawakabili ni upatikanaji wa vifaa pamoja na masoko.
Alisema mkutano huo umewawezesha kujifunza mbinu mbalimbali wanazotakiwa kuzitumia katika uvuvi wao.
MWANANCHI
Mamia ya wakazi wa Mwanza na mikoa ya jirani jana walijitokeza kwa wingi kuaga mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo, huku aliyekuwa mgombea urais wa chama hicho, Edward Lowassa akisema waliomuua mwanasiasa huyo wanajulikana na endapo polisi hawatawakamata, Chadema watachukua hatua wenyewe.
Heshima za mwisho za kuaga mwili wa Mawazo aliyeuawa Novemba 14 mkoani Geita kwa kushambuliwa na watu wanaodaiwa ni wafuasi wa CCM, zilitolewa jana katika Uwanja wa Furahisha kuanzia saa tano asubuhi hadi saa tisa alasiri.
Utoaji wa heshima za mwisho kwa mwili wa Mawazo ziliongozwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliyekuwa ameambatana na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Lowassa na viongozi waandamizi wa chama hicho wakiwamo wabunge zaidi ya 50 wa Ukawa.
Akizungumza wakati wa kutoa salamu za rambirambi, Lowassa alisema; “Mawazo ameuawa kinyama, polisi wasipochukua hatua kwa watu waliyofanya mauaji hayo tutachukua hatua wenyewe.” Aliongeza: “Imeshaelezwa kwamba wahusika wanajulikana tena kwa majina, sasa watu hawawezi kusubiri haki kama wanaona vyombo husika vya kutenda haki vinashindwa kufanya kazi yao.”
Akizungumzia tukio la kuzuiwa kuaga mwili huo hadi kwa amri ya Mahakama, Lowassa alisema kinachofanywa na polisi ni kutafuta uhalali wa kutumia fedha za wananchi walizozitumia kununua silaha ambazo zilishindwa kufanya kazi wakati wa uchaguzi.
“Hapa kulitolewa sababu za kipindupindu ili watu wasiage mwili wa Mawazo, lakini sababu hizo zilikuwa ni uongo mtupu.. hakuna cha kipindupindu wala nini.
Mahakama imetenda haki, hata Biblia inasema waacheni watu wazike wafu wao, uamuzi wa Mahakama Kuu itakuwa somo kwa nchi nzima, mimi nampongeza jaji aliyeruhusu watu kumuaga Mawazo,” alisema Lowassa.
Wakati Lowassa akisema hayo, Sumaye alisema haki isipopatikana kwa amani itapatikana kwa njia nyingine, huku akitoa mfano wa askari wa makaburu walivyowakandamiza watu wa Afrika Kusini, lakini walipoamua kutafuta haki walifanikiwa kuwatoa.
“Mimi ni mgumu sana kutoa machozi, hata baba yangu alipofariki sikutoa machozi, lakini leo nimetoa machozi kwa sababu nchi ambayo ilikuwa na misingi ya amani, leo tunashuhudia watu wanaodai haki wanauawa, ni jambo la kusikitisha,” alisema Sumaye.
Aliwataka waombolezaji wasimamie amani lakini wasikubali kuonewa, kwa kuwa ni lazima wapinge dhuluma.
HABARILEO
Wazee wanaoishi katika kituo cha kulea wazee kinachomilikiwa na serikali kilichoko Kilima Bukoba Vijijini, wanalazimika kulala katika bweni moja wanaume na wanawake baada ya jengo la wazee wanawake kuezuliwa na upepo miaka minane iliyopita.
Wakizungumzia hali hiyo wazee wanaoishi katika kituo hicho walisema kuwa tangu jengo la wazee wanawake lilipoezuliwa na upepo hadi sasa wanalazimika kukaa katika jengo moja.
Mwenyekiti wa Wazee kambini hapo, Evarister Kayogera alisema kuwa nyumba ya kulala wazee wanawake iliezuliwa muda mrefu, serikali haijairekebisha na kwamba huwa wanakuja wanaangalia tu wanaondoka hawarudi, hivyo hawafahamu lini serikali italirekebisha ili wanawake wahamie katika jengo lao ili waache kubanana sehemu moja.
Mbali na tatizo hilo mzee Kayogera alisema wamekuwa wakikosa usafiri wa kupelekwa hospitali na wakati mwingine wakipelekwa wanapimwa na kuandikiwa dawa na kuambiwa kuwa hazipo waende kununua mitaani wakati wao hawana kipato chochote.
“Wahudumu wetu wakiwa na fedha ndiyo huwa wanachanga na kutununulia dawa, na wakati mwingine wakiwa hawana fedha wanatafuta dawa za kienyeji mbugani wanachemsha wanatupa tunakunywa ili tuone kama tutaendelea kuishi,” alisema.
Mzee mwingine John Rwiza alisema kuwa ni muda mrefu sasa kituo hicho hakina mafuta ya taa hali inayosababisha kula na kulala gizani, kutokana na kutokuwa na umeme.
Rwiza alisema chakula cha usiku wanalia gizani hawana mafuta ya taa na kwamba wanapika chakula mfano wali usio na mafuta wanachemsha tu na maharage hayawekwi chochote, wanakunywa uji usio na sukari na hawana pa kujisaidia.
HABARILEO
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue ametoa ufafanuzi mpya kuhusu maagizo ya Rais John Magufuli, kwa watendaji wakuu na maofisa masuhuli wote wa wizara, idara na taasisi za Serikali, katika suala zima la kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ya fedha za umma.
Katika ufafanuzi huo uliotumwa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Balozi Sefue ametaka kila mtendaji wa Serikali kujihoji mwenyewe, kwamba endapo Rais Magufuli ataamua kufika katika eneo lake la kazi, ni kwa kiasi gani atakuta ametekeleza maagizo yake.
“Rais ameonesha njia, sasa kwa wakati huu ni vyema kila Mtendaji Mkuu wa Serikali, ajiulize endapo Rais Magufuli atafika katika eneo lake la kazi, ni kwa kiasi gani atakuta nimetekeleza maagizo yake,” ameeleza Balozi Sefue katika ufafanuzi huo.
Akiingia kwa ndani, Balozi Sefue ametoa mfano wa uchapishaji wa kalenda na vitabu vya kumbukumbu (diaries) na kutaka kila Mtendaji Mkuu au Ofisa Masuhuli wa Serikali, apime mwenyewe kama ni lazima kutengeneza na kuchapisha vitu hivyo na kama kuna ulazima, wachapishe kwa kiasi gani.
“Ni matumizi mabaya ya fedha za umma kwa kila wizara, idara na taasisi za Serikali kuchapisha idadi kubwa ya kalenda na diaries ambazo wakati mwingine hata hazitumiki mpaka mwaka unakwisha,” alisema Balozi Sefue.
Kadi, sherehe Ufafanuzi huo umekuja baada ya hatua mbalimbali kuchukuliwa na Dk Magufuli katika kubana matumizi ya fedha za Serikali yasiyokuwa ya lazima, ikiwemo kupiga marufuku utengenezaji na uchapishaji wa kadi za sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.
Magufuli wiki hii alipiga marufuku wizara, idara au taasisi za umma kuchapisha kadi hizo kwa kutumia fedha za Serikali.
Badala yake, aliagiza fedha zilizopangwa kugharamia utengenezaji na uchapishaji wa kadi hizo, zitumike kupunguza madeni ambayo wizara, idara na taasisi hizo zinadaiwa na wananchi, wazabuni waliotoa huduma na bidhaa kwao au zipelekwe katika matumizi mengine ya kipaumbele.
Mbali na kadi, pia alizuia kufanyika kwa maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yaliyotarajiwa kufanyika Desemba mosi mkoani Singida, na badala yake fedha za sherehe hizo zitumike kununulia dawa za kupambana na makali ya virusi vya Ukimwi kwa wagonjwa.
Safari za nje Ukiacha kuzuia uchapishaji wa kadi, Novemba saba mwaka huu, Rais Magufuli, alitangaza kuzuia safari za watumishi wa umma nje ya nchi, kutokana na ukweli kuwa safari hizo zimekuwa zikigharimu mabilioni ya fedha pasipo kuzingatia umuhimu kwa maslahi ya Taifa.
Kutokana na hatua hiyo, Rais aliamuru mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania, watumike kwenye mikutano ya kimataifa au shughuli zilizokuwa zikitakiwa kufanyika nje ya nchi.
Kwa waliokuwa na ulazima wa kwenda safari za nje, Rais Magufuli alitaka wafuate kibali kwake mwenyewe au kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Sefue. Sherehe ya wabunge Jitihada za kuzuia matumizi ya Serikali za Dk Magufuli, zilifika mpaka kwa wabunge baada ya kuagiza fedha zilizochangwa kwa ajili ya kugharamia hafla ya kuwapongeza, zipelekwe katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kununulia vitanda vya wagonjwa.
Rais Magufuli alitoa agizo hilo baada ya kupokea taarifa kuwa, wadau mbalimbali walikuwa wamechanga Sh milioni 225 kwa ajili ya kugharamia hafla ya wabunge katika siku ya uzinduzi wa Bunge. Alitoa maagizo kuwa kiasi kidogo tu cha fedha ndicho kitumike kwenye hafla hiyo na sehemu kubwa ipelekwe Muhimbili, ili zikatumike kununulia vitanda vya wagonjwa.
Siku chache baada ya uamuzi huo, fedha hizo zilitolewa na Katibu wa Bunge kwenda Bohari ya Dawa (MSD), ambao walinunua vitanda 300, viti maalumu vya wagonjwa 30, vitanda maalumu vya kubebea wagonjwa 30, mashuka 1,695 na mablanketi 400 kwa ajili ya wagonjwa. Sherehe za Uhuru Eneo lingine ambalo limekumbwa na hatua za kupunguza mapato ya Serikali, ni sherehe za miaka 54 ya Uhuru, ambazo zimekuwa zikifanyika Desemba 9, kila mwaka.
Rais Magufuli amezuia kufanyika kwa sherehe hizo mwaka huu na kuamuru siku hiyo itumike kufanya kazi ikiwemo usafi kwenye maeneo mbalimbali nchini, ili kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli, wananchi hawapaswi kusherehekea miaka 54 ya Uhuru wa Tanzania Bara, huku wakiendelea kufa kwa ugonjwa huo unaosababishwa na uchafu.
Aidha, fedha zilizokuwa zitumike kugharamia sherehe hiyo, sasa zitapangiwa matumizi mengine ya maendeleo hususan kuboresha huduma za afya.
Vikao kwa televisheni Hatua zingine za kupunguza matumizi zilizochukuliwa na Serikali ni pamoja na katazo la maofisa wa Serikali kusafiri kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine kwa ajili ya vikao vya kazi, ambalo limewahusu wakurugenzi, makatibu tawala wa mikoa na wilaya pamoja na wafanyakazi wengine wa umma.
Badala yake watumishi hao wametakiwa kufanya mikutano kwa kutumia mfumo wa mawasiliano kwa njia ya video, ili kupunguza gharama za kuendesha vikao hivyo, kwa sababu washiriki wataunganishwa kwa mfumo wa video wakiwa kwenye vituo vyao vya kazi. Maofisa wa TRA Katika hatua nyingine, maofisa watatu wa Mamlaka ya Mapato (TRA) ambao Waziri Mkuu Majaliwa Kassim, aliagiza juzi wahamishwe kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa mingine, jana aliwabadilishia maelekezo na kupewa adhabu ya kusimamishwa kazi.
Taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana, iliwataja maofisa hao kuwa ni Anangisye Mtafya, Nsajigwa Mwandengele na Robert Nyoni.
“Kazi ya kuwachunguza ilianza jana ileile na sasa, tumeona hawa watu wanapaswa kuwa nje ya utumishi, ili kupisha uchunguzi ufanyike kwa uhuru zaidi,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa katika taarifa hiyo.
Pia Waziri Mkuu amemuagiza Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA, Dk Philip Mpango atekeleze maagizo hayo kwa kuwaandikia barua watumishi hao.
Kwa hatua hiyo, watumishi waliosimamishwa kazi mpaka jana, wamefikia tisa kutokana na kashfa ya kupotea kwa makontena 349 yaliyopita bandarini, lakini hayakulipa kodi ya Serikali yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 80.
Wengine waliosimamishwa kazi juzi ni pamoja na Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade, aliyechukuliwa hatua hiyo na Rais Magufuli na nafasi yake kukaimiwa na Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dk Mpango.
Waliowekwa mahabusu Mbali na hao wanne ambao wamesimamishwa kazi tu na kuzuiwa kusafiri nje ya nchi, kwa kunyang’anywa hati zao za kusafiria, Waziri Mkuu Majaliwa pia juzi aliwasimamisha vigogo wengine kazi, lakini adhabu yao ikawa kubwa kidogo baada ya kukabidhiwa kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Ernest Mangu.
Vigogo hao waliosimamishwa na kuwekwa rumande ni Kamishna wa Forodha, Tiagi Masamaki, Mkuu wa Kituo cha Huduma kwa Wateja, Habibu Mponezya, Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Haruni Mpande, Hamisi Ali Omari (hakutaja ni wa idara gani) na Mkuu wa Kitengo cha Bandari Kavu (ICD In-Charge), Eliachi Mrema.
MTANZANIA
Mkazi wa Ngulelo, Arusha Neema Obedi amehukumiwa kifungo cha miezi sita jela kwa kosa la kumtukana Zubeda Efasi kuwa ni mgumba, hana kizazi na alichonacho hakina faida, hivyo angemwazima chake ilia pate watoto.
Hukumu hiyo ilitolewa juzi na hakimu Smathon Joseph wa mahakama ya mwanzo ya Maromboso Mkoani Arusha.
Hakimu alisema mshtakiwa huyo alimfuata mlalamikaji na kumtolea matusi hayo huku akijua ni kinyume na sharia na kutakiwa kwenda jela miezi sita na kulipa faini ya shilingi 300,000.
“Matusi hayafai mbele ya jamii, hii ni aibu kutoa maneno mazito kama hayo kw akuwa sote tumetokana na mwanamke, hivyo anapaswa kuheshimiwa na haipendezi kutoa maneno mazito kama hayo”…
Unataka kutumiwa MSG za habari zote kubwa kutoka kwa Millard Ayo? ukiwa na line ya tiGO andika ‘AYO’ tuma kwenda 15510, msg utayotumiwa jibu OK ili uanze kupokea matukio yote kwa sms, pia ungana na Millard Ayo kwenye Twitter, FB, Instagram na YouTUBE wa kubonyeza hapa>>>INSTAGRAM TWITTER FB YOUTUBE.