HABARILEO
Makatibu wakuu na Naibu Makatibu Wakuu walioteuliwa na kuapishwa juzi wamekutana katika ukumbi wa mikutano wa Ikulu jijini Dar es Salaam kwa ajili ya semina elekezi iliyoongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.
Akizungumza kabla ya kuanza kwa mada zilizoandaliwa katika semina hiyo jana, Katibu Mkuu Kiongozi Sefue, alisema semina hiyo ni ya kikazi zaidi na kwamba lengo la serikali ni kuhakikisha viongozi hao waandamizi wanatekeleza wajibu wa kusimamia utendaji kazi wa serikali vizuri.
Balozi Sefue alisema kila Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu anapaswa kutambua kuwa nafasi yake ni ya maamuzi, hivyo serikali inatarajia kuona wanafanya maamuzi kwa usahihi na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazomuongoza kila mmoja katika majukumu yake.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano inawatarajia viongozi hao kuwa wasimamizi wazuri wa fedha za umma na kwamba haitarajii kuwepo kwa hati za ukaguzi wa mahesabu zenye kasoro.
Balozi Sefue aliongeza kuwa Makatibu Wakuu hao na Naibu Makatibu Wakuu ni mamlaka ya nidhamu katika wizara zao, hivyo serikali haitarajii kuona wanakuwa na kigugumizi katika kuchukua hatua dhidi ya watumishi watakaokuwa na makosa.
Aliwakumbusha pia kwamba haikubaliki kwa mtumishi aliyefanya makosa katika sehemu moja ya kazi, kuhamishiwa katika sehemu nyingine badala ya kuchukuliwa hatua palepale alipo.
HABARILEO
Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba amesema hakutakuwa na msamaha na huruma kwa watakaobainika kuhujumu sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi nchini.
Nchemba alisema hayo baada ya kubaini kuwepo kwa utafunwaji wa mapato ya serikali ya vibali vya mifugo, yanayokusanywa katika Mnada wa Pugu, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Alibaini kuwepo kwa hujuma hizo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza ya kukagua mnada huo na machinjio ya Vingunguti yaliyopo Manispaa ya Ilala juzi usiku.
Baadaye alitangaza hatua kadhaa, ikiwemo Mkuu wa Mnada huo wa Pugu na watumishi waliokuwa zamu Desemba 24 mwaka jana na Januari Mosi mwaka huu, kesho Jumatatu wafike ofisi ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo.
Pili, Mwigulu alisema kuanzia sasa amesitisha ukusanyaji wa ushuru kwenye eneo la Mnada wa Pugu, badala yake makusanyo yote ya fedha za Serikali, yatafanyika kwenye Machinjio la Vingunguti kwa kutumia mashine za kielektroniki za Mamlaka ya Mapato Tanzania (EFDs).
Alisema mnada wa Pugu sasa utakuwa unatumika kutoa vibali tu vya mifugo ili kudhibiti ubora wa mifugo inayotakiwa kuchinjwa. “ Sitakuwa na huruma na hatua stahiki zichukuliwe kwa mtu yeyote mwenye dhamana ya kusimamia sekta hiyo atakayebainika kutowajibika kwa mujibu wa Sheria,” alisema.
Akizungumza katika machinjio hayo, Nchemba alisema ubadhirifu uliopo ni wa uandikaji wa vibali kwa mifugo wachache kwa ajili ya kwenda machinjioni, tofauti na idadi ya mifugo inayoingizwa machinjioni hapo. Alisema mifugo mingi inaingizwa machinjioni bila kibali.
Katika ukaguzi huo, Mwigulu alibaini uwepo wa utafunwaji wa kodi ya mifugo zaidi ya 1,107 kwa siku, kati ya mifugo 1450 iliyolipiwa ushuru, kwa ajili ya kupelekwa katika machinjio hayo kutoka Mnada wa Pugu.
“Kwa hatua za awali nimekutana na ubadhirifu wa kutafunwa kwa kodi ya mifugo zaidi ya 1,107 kwa siku, kati ya mifugo 1450 iliyolipiwa ushuru kwa ajili ya kuja kwenye machinjio ya Vingunguti kutoka Mnada wa Pugu Desemba 26,2015,” alisema.
Aidha, Nchemba alisema alisikiliza kero na maoni ya wananchi wanaotumia machinjio hayo pamoja baadhi ya viongozi wenye dhamana na kusimamia juu ya uendeshwaji wa machinjio hayo.
Nchemba aliagiza uongozi wa machinjio hayo, kukutana kwa ajili ya kuchukua hatua stahiki kwa watakaobainika kukiuka taratibu na sheria. Uchinjaji wa ng’ombe na mbuzi katika machinjio hayo, hufanyika nyakati za usiku kuanzia saa 4 hadi 10 alfajiri.
HABARILEO
Watu sita wamekufa papo hapo na wengine 25 kujeruhiwa na kulazwa hospitalini kutokana na ajali mbili tofauti. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo, alisema mjini hapa jana kuwa ajali ya kwanza, ilihusisha basi la abiria lililokuwa na abiria 42, ambalo liligonga kingo za daraja, likaparamia miti miwili kisha kutumbukia ndani ya mto Lukosi, Iyovi eneo la Msosa huko Mikumi wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, katika barabara kuu ya Iringa – Morogoro.
Alisema tukio hilo ni la Januari Mosi mwaka huu majira ya saa 8 mchana. Basi hilo lilitokea Dar es Salaam, lilikuwa linakwenda Mbeya. Kamanda Paulo alisema dereva wa basi hilo aliendesha gari kushoto zaidi, akaenda kugonga kingo za daraja hilo, akaenda kuparamia miti miwili kisha alilitumbukiza ndani ya mto huo.
Kamanda huyo alisema katika ajali hiyo, watu watatu walikufa akiwemo dereva wa basi hilo na kujeruhi wengine 16, ambapo majeruhi 14 walilazwa katika Kituo cha Afya cha Tandika kilichopo eneo la wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa. Majeruhi wengine sita walisafirishwa hadi Hospitali ya Mkoa wa Iringa na kulazwa.
Kamanda alisema basi hilo lilibeba abiria 42 na chanzo za ajali hiyo kilielezwa na mashuhuda kuwa ni uzembe wa dereva wa basi, aliyeshindwa kufuata sheria za usalama barabarani katika eneo hilo la safu ya milima ya Iyovi, lenye kona nyingi na mito yenye madaraja. Alisema maiti mmoja ametambulika na ni dereva wa basi hilo.
Maiti wawili, mmoja mwanamume na mwingine mwanamke, bado hawajatambuliwa na wamehifadhiwa katika chumba za maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro. Alitoa mwito kwa watu kufika kuwatambua.
Kamanda huyo wa Mkoa alisema ajali ya pili ilitokea Januari Mosi mwaka huu, ambapo watu watatu walifariki papo hapo na wengine watano kujeruhiwa na kulazwa katika Kituo cha Afya cha Gairo wilayani Gairo mkoani Morogoro.
Alisema ajali hiyo ilihusisha gari ndogo, lenye namba za usajili T 252 CGV aina ya Toyota Vitz, lililokuwa likiendeshwa na Bundala Charles Mahimbo, mkazi wa Dar es Salaam. Gari hilo liligongana uso kwa uso na lori, lenye namba za usajili T531 CFE lenye tela namba T 509 AFY aina ya Scania, lililokuwa likiendeshwa na dereva, Ally Said Magimbi (33), mkazi wa Mtongani , Dar es Salaam.
Alisema ajali hiyo ilitokea jioni eneo la Ngiroli wilayani Gairo barabara kuu ya Morogoro- Dodoma. Gari ndogo lilikuwa likitokea Mkoa wa Tanga kwenda Mwanza wakati lori kubwa lilitokea Kagera kwenda Dar es Salaam.
Kamanda Paulo alisema watu watatu waliokuwa katika gari ndogo, walikufa papo hapo na wengine watano walijeruhiwa, miongoni mwao mmoja ni abiria wa lori. Kamanda huyo wa Polisi aliwataja waliokufa katika ajali hiyo ni Bundala Mahimbo ambaye ni mkazi wa Dar es Salaam, Flora Mugabo na Emmanuel Mahimbo, wote wakazi wa Nyakato mkoani Mwanza.
Majeruhi waliolazwa Kituo cha Afya Gairo ni dereva wa lori, Ally Magimbi, mkazi wa Mtongani Dar es Salaam, Peter Mahinda ambaye ni mkazi wa Nyakato na Hassan Mwera. Walioruhusiwa ni Judith Joseph na Scolastica Fransis aliyekuwa abiria kwenye gari kubwa.
HABARILEO
Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) wiki ijayo inakutana na wadau kujadili nauli zitakazotumika kwa mabasi yaendayo kasi.
Kwa sasa kampuni ya UDA-RT inapendekeza nauli ya chini kuwa Sh 700 na wanafunzi kulipa nusu yake.
Aidha, katika mapendekezo yake, UDA-RT inataka nauli ya safari kwenye njia kuu kuwa Sh 1,200 na safari katika njia kuu na pembeni kuwa Sh 1400 na wanafunzi nusu ya nauli hizo.
Taarifa iliyotolewa jana na Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra ilisema maombi hayo kwa ajili ya kutoa huduma za mpito za usafiri wa mabasi yaendayo haraka katika awamu ya kwanza ya mradi wa DART yatajadiliwa na wadau ili kuona uhalali wake.
Ilisema kwa mujibu wa sheria, Sumatra inapaswa kukusanya maoni ya wadau kabla ya kufikia uamuzi wa kuridhia viwango vya nauli.
“Katika kutekeleza hilo, mamlaka imeandaa mkutano ili kupokea maoni ya wadau ikiwa ni pamoja na watoa huduma, watumiaji wa huduma na wananchi kwa ujumla,” ilisisitiza sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mkutano huo wa wadau utafanyika Januari 5, mwaka huu katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam kuanzia saa tatu asubuhi ambapo wadau wote wa usafiri wanaalikwa.
MWANANCHI
Kasi ya Mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Tano jana ilichukua sura ya aina yake wakati mawaziri watatu walipoibuka kwenye machinjio ya Vingunguti, na kutoa maamuzi magumu kutokana na kukithiri kwa uchafu, ubadhilifu wa makusanyo ya fedha za ushuru.
Wakiwa katika eneo la machinjio hayo mawaziri hao, Mwigulu Nchemba (Kilimo, Mifugo na Uvuvi), Dk Hamisi Kigwangalla (Afya), na George Simbachawene (Ofisi ya RaisTamisemi), walishuhudia hali ya uchafu wa eneo hilo na baadaye kubaini ubadhilifu mkubwa.
Baada ya kufanya ziara hiyo iliyoanza saa 4:47 asubuhi na kumalizika saa 5:32, mawaziri hao hawakuridhishwa na hali ya usafi kwenye maeneo ya kuwekea nyama.
Mbali na hayo walisikiliza kero za wadau ambao ni wachinjaji na wauzaji wa mifugo, waliodai wanatozwa ushuru mkubwa kama malipo ya Sh11,000 kwa ng’ombe mmoja, fedha ambazo hulipwa mnada wa Pungu (sh6,000) na Vingunguti (Sh5,000).
Catherine Severine, ambaye ni mchuuzi aliyekuwa zamu usiku wa Desemba 24 mwaka jana, aliwaambia mawaziri hao kuwa kumekuwepo udanganyifu wa utoaji wa vibali kwenye mnada wa Pugu.
Alidai kuwa siku hiyo walifikishwa mbuzi 1,407 huku wenye vibali wakiwa 300 , ng’ombe 700 lakini wenye vibali halali 492, hivyo kwa hesabu za haraka, zaidi ya Sh3.4 milioni zilipotea.
Alisema kwa ujumla wanatakiwa wakusanye kiasi cha Sh75 milioni kwa mwezi, lakini walikuwa wanakusanya Sh18 milioni huku Sh55 milioni zikiingia mifukoni mwa wajanja. Simbachawene alimpa siku tatu mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala kuwaondoa wale wote waliokaa muda mrefu katika eneo hilo na kujimilikisha kila kitu.
“Kigwangalla naomba usitufungie, Jumanne nitataka kupata maelezo ya waliohusika na haya mabanda. Si kweli kwamba yamegharimu Sh100 milioni. Hadi Jumatatu umeme uwe umerudishwa kwenye hayo mabanda, yatumike ili kupunguza mbanano,” aliagiza Simbachawene.
Mwigulu aliwataka wote waliokuwepo mnadani Desemba 24, kufika kwa katibu mkuu wa Wizara Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Jumatatu na kuanzia leo waanze kutafuta kazi ya kufanya kwa sababu ya kujumlisha ng’ombe na mbuzi imewashinda.
Mwigulu alisema hayo baada ya juzi usiku kukuta machinjio ya Vingunguti kuna vibali 300 vya mbuzi, lakini kukiwa na mbuzi zaidi 1,000 na ng’ombe zaidi ya 200 hawakuwa na vibali, kitu alichosema kinaashiria wanafanya makusudi siyo kwamba hawajui kujumlisha.
“Kuanzia sasa vibali vyote vya wanyama wanaotakiwa kuchinjwa hapa, vitolewe kwenye mnada wa Pugu, huku wakusanya ushuru wa Serikali Kuu na Halmashauri watakusanya hapa katika machinjio ya Vingunguti.
Mnaolipia ushuru hakikisheni mnaondoka na risiti, lango la kuingizia ng’ombe lijengwe mara moja hata matatu, manne tena kwa fedha inayopatikana hapa hapa machinjioni,” alisema Mwigulu huku akishangiliwa.
Kigwangalla alisema anakubali ombi la Simbachawene la kutaka wasifungiwe kwa muda na watavamia wakati wowote kukagua maagizo waliyotoa kama yanafanyiwa kazi. Alisema mambo aliyoyaona akiwa katika Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa miaka miwili iliyopita ndiyo aliyoyakuta jana , hivyo hatawavumilia wanaohusika.
MWANANCHI
Jeshi la Polisi limemkamata raia wa Nigeria kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA), kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya ambazo thamani yake ni kubwa ingawa haijajulikana.
Kamanda wa polisi wa JNIA, Martin Ottieno alisema mtuhumiwa huyo, Ejiofor Ohagwu, alikamatwa na kilo nne za dawa hizo ambazo alisema licha ya kutofahamu thamani yake kwa sasa, inaweza kuwa kubwa kwa sababu hawajawahi kukamata dawa za kiwango hicho.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa Mwananchi, kilo moja ya heroin kwa bei ya mitaani ni kuanzia Sh90 milioni. Ottieno alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa saa 8:00 usiku wa kuamkia jana kwenye sehemu ya ukaguzi ya eneo la wasafiri wanaoondoka.
Alisema awali polisi walipata taarifa za kiintelijensia kuhusu Ohagwu na alipopekuliwa alikutwa na dawa alizodai kuwa ni heroin zilizofungwa katika pakiti sita za plastiki.
“Mtuhumiwa huyo alikuwa anasafiri kuelekea mji wa Lagos, Nigeria, akitumia Shirika la Ndege la Ethiopia,” alisema. “Dawa hizi alizificha kitaalamu kwa kushonea pakiti zote pembeni mwa mabegi yake mawili ya nguo ili asibainike haraka na vyombo vya dola.” Alisema polisi bado inamshikilia mtuhumiwa huyo na upelelezi utakapokamilika, atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka.
Pia, alisisitiza kuwa kwa sasa viwanja vya ndege si vichochoro vya kupitisha dawa hizo, kwa kuwa polisi ikishirikiana na wadau wengine, imejipanga kupambana na aina hiyo ya uhalifu.
“Mbali na kuwakamata hawa, pia tumelenga kuwakamata mapapa wanaoagiza dawa hizi, ” alisema Kamanda Ottieno. Desemba 17 mwaka jana, Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga alikutana na maofisa wa polisi wa Kanda ya Dar es Salaam na kutaka wamueleze mipango ya kukabiliana na dawa za kulevya.
MWANANCHI
Wakati watu mbalimbali wakimminia sifa Rais John Magufuli kwa kubana matumizi, aliyekuwa Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk Makongoro Mahanga amesema uwingi wa makatibu wakuu unakinzana na dhana ya yake ya kupunguza ukubwa wa Baraza la Mawaziri.
Lakini naibu waziri huyo kwenye Serikali ya Awamu ya Nne amesifu hatua mbalimbali za kupambana na ufisadi anazochukua Rais Magufuli akisema amefanikiwa kutumbua majibu, lakini sasa anatakiwa awe na ubunifu katika kutatua matatizo ya wananchi.
Dk Mahanga alikuwa Naibu Waziri wa Kazi na Ajira tangu mwaka 2008 na hakuwahi kuhamishwa wala kupandishwa hadi ngazi ya uwaziri hadi Serikali ya Rais Jakaya Kikwete ilipomaliza muda wake na baadaye kujiunga na Chadema.
Akizungumza na Mwananchi jana, mbunge huyo wa zamani wa Jimbo la Segerea (CCM) alisifu kazi inayofanywa na Rais Magufuli akisema inaonekana wazi. “Kweli ametumbua majipu ambayo hakika yalikuwa yameiva,” alisema Dk Mahanga. “Naweza kusema alikuta nyumba chafu na inanuka, ameisafisha.
Sasa tunapenda kuona baada ya kusafisha ataiweka katika hali gani? Atabuni nini ili kuwasaidia vijana dhidi ya tatizo la ajira ili wengi waweze kumudu gharama za maisha.
” Lakini katika waraka wake alioutoa kwenye mitandao ya kijamii, Dk Mahanga alimkosoa Rais Magufuli akisema ameongeza ukubwa wa Baraza la Mawaziri baada ya kuteua makatibu wakuu 27 wakati anawaaminisha wananchi kwamba wizara ni 15 tu.
Dk Magufuli ameunda baraza lenye mawaziri 15, na manaibu waziri 19 na hivyo kufanya baraza lake kuwa na jumla ya mawaziri 34, tofauti na baraza lililopita lililokuwa na mawaziri 55. Uamuzi wa kupunguza idadi ya wizara ulikumbana na changamoto ya nafasi za makatibu, ambao hata hivyo baadhi amewarudisha wizarani ambako watapangiwa kazi na kubakiwa na makatibu 27.
“Si kweli kwamba kapunguza ukubwa wa Serikali, bali kaongeza ukubwa wake. Sina hakika kama wasaidizi wa Rais wamemshauri na kumweleza kwamba wizara si ofisi ya waziri bali wizara ni ofisi ya katibu mkuu,” alisema Dk Mahanga akifafanua kuwa katibu mkuu ndiye mtendaji mkuu wa wizara na afisa masuhuli.
Alisema katibu mkuu ndiye mwenye dhamana ya utendaji na ndiyo maana hata katika ngazi ya kata, ofisi inaitwa ofisi ya ofisa mtendaji wa kata na si ofisi ya diwani.
Kwa maana hiyo, Dk Mahanga, ambaye kitaaluma ni mhasibu, alisema Rais alipounda Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, ambazo awali zilikuwa mbili tofauti na kuteua makatibu wakuu watatu, kiuhalisia hakuunganisha wizara mbili kuwa moja bali ameunda wizara tatu kutoka mbili za awali. “Ongezeko la gharama kwa kuongeza waziri mmoja ni ndogo sana kulinganisha na kuongeza katibu mkuu mmoja.
Waziri anapoteuliwa tayari anakuwa ni mbunge mwenye mshahara wake wa ubunge na kinachoongezeka ni kama laki tano tu juu ya ule mshahara wa ubunge na gharama nyingine ndogo za gari, pia mishahara na gharama za katibu muhtasi, msaidizi na dereva,” alisema Dk Mahanga.
Alisema kwa ujumla ahadi ya Rais Magufuli aliyotoa kwenye kampeni kwamba ataunda Serikali ndogo, hakuitimiza badala yake ameongeza ukubwa wa Serikali.
Wakati wa kampeni na alipoapishwa, Rais Magufuli alisema ataunda baraza dogo la mawaziri, hiyo ilijenga shauku kwa wananchi kufahamu kiwango cha ukubwa au udogo wa baraza hilo ikilinganishwa na mabaraza yaliyoundwa na watangulizi wake, tangu Tanzania ipate uhuru mwaka 1961. Dk Magufuli pia alitoa ahadi hiyo alipozindua Bunge Novemba mwaka jana mjini Dodoma.
MWANANCHI
Wingu zito linaendelea kutanda kwenye anga za siasa visiwani hapa baada ya Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi kusema mchakato wa kupanga bajeti kwa ajili ya marudio ya uchaguzi umekamilika, huku CUF ikishangazwa na kupinga tamko hilo.
Rais wa Zanzibar, Dk Mohamed Shein na katibu wa CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad wako kwenye mazungumzo ya kujadili kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Rais, wawakilishi na madiwani na hadi sasa hawajatoa tamko la maendeleo ya mazungumzo yao.
Lakini viongozi wa CCM wamekuwa wakitoa taarifa za kuwataka wafuasi wao wajiandae kwa marudio ya uchaguzi, huku CUf ikisema inachosubiri ni kutangazwa kwa mshindi wa uchaguzi wa Rais na haiku tayari kurudia uchaguzi.
Kauli nyingine ya namna hiyo ilitolewa jana na juzi na Balozi Seif alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya sherehe za kutimia miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar, akisema kwa kuwa matokeo ya uchaguzi yalifutwa basi ni wazi kuwa hakuna utaratibu ambao utakaofanyika wa kuyamaliza matokeo yaliobaki isipokuwa kurudia uchaguzi upya.
“Tuache kusikiliza maneno ya porojo bali nawaambia suala la kurudia uchaguzi lipo kama kawaida na kilichobaki sasa ni kusubiri amri ya Tume (ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC)) kutangaza siku ya uchaguzi huo,” alisema Balozi. “Kwa upande wetu CCM tupo tayari kushiriki uchaguzi huo.
Hata kama CUF hawatashiriki, sisi hawatubabaishi.” Kwa upande wa mazungumzo yanayofanyika Ikulu kwa kuwashirikisha viongozi wa wakuu wa Serikali, Balozi alisema kuwa hajui nini kinaendelea hadi sasa, lakini akawataka wananchi wasubiri taarifa rasmi mazungumzo hayo yatakapomalizika.
“Kikubwa zaidi nilichokisikia mimi katika mazungumzo hayo ni suala la kudumisha amani na utulivu ila kwa upana zaidi tusubiri mazungumzo hayo yatakapomalizika taarifa itatolewa kwa wananchi wote,” alisema.
Lakini kwa mara nyingine, CUF walipinga vikali kauli hiyo wakisema hawako tayari kurudia uchaguzi. Kaimu mkurugenzi wa habari, uenezi na mawasiliano ya umma wa CUF, Ismail Jussa alisema matamko hayo yanashangaza wakati bado mazungumzo yanaendelea.
Jussa alidai kuwa kuna timu imejifungia mahali inafanya hujuma na inampotosha Dk Shein. Kuhusu sherehe za miaka 52 ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif alisema kutoshiriki kwa viongozi wa CUF hakutaathiri sherehe hizo.
Alisema kamati ya maadalizi ya sherehe na mapambo tayari imeshajipanga vya kutosha na kilichobaki ni ufanikishaji wa maadhimisho hayo ambayo shamrashamra zake zilitarajiwa kuanza jana.
Alisema madhimisho hayo yapo kama kawaida na mwaka huu wamepanga siku ya kwanza ya shamrashamra zake kuitumia kufanya usafi wa mazingira ya mji wa Zanzibar.
Alisema kuwa shamrashamra nyingine za maadhimisho hayo zitaendelea kama kawaida kwa kufungua miradi mbalimbali ya maendeleo
Unataka kutumiwa MSG za habari zote kubwa kutoka kwa Millard Ayo? ukiwa na line ya tiGO andika ‘AYO’ tuma kwenda 15510, msg utayotumiwa jibu OK ili uanze kupokea matukio yote kwa sms, pia ungana na Millard Ayo kwenye Twitter, FB, Instagram na YouTUBE wa kubonyezahapa>>>INSTAGRAM TWITTER FB YOUTUBE