NIPASHE
Askofu Mkuu Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo, aliyekuwa amelazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa siku 10 akipatiwa matibabu, ameruhusiwa kuondoka hospitalini hapo.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Profesa Mohamed Janabi, alisema Askofu Pengo ameruhusiwa kwenda nyumbani kutokana na kupata nafuu.
Juzi Askofu Pengo alizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo na kusema kuwa awali hakuwa na imani na huduma zinazotolewa na hospitali hiyo, lakini baada ya kupata matibabu amezikubali.
Kutokana na huduma nzuri aliyoipata hospitalini hapo, Askofu Pengo alitumia fursa hiyo kutoa kadi maalum za shukrani kwa idara ya matumbo na ya dharura na pia kumpa kadi Profesa Jenabi ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa taasisi hiyo.
Juzi Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Ummi Mwalimu, ambaye alimtembelea hospitalini hapo, alisema Askofu Pengo amekataa kwenda nje ya nchi kwa matibabu akisema kuwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) inatosha kumtibu.
Mwalimu alisema alimsikia Askofu Pengo akisema kuwa watakuwa na kazi ya ziada kumshawishi kupelekwa nje kwa matibabu, kauli inayodhihirisha kuwa ameridhika na matibabu yanayotolewa hospitalini hapo na hataki kupelekwa nje ya nchi.
Waziri Mwalimu alisema amefurahishwa na kauli hiyo kwani imemtia moyo kwamba juhudi za serikali za kuwezesha huduma mbalimbali za afya zinapatikana Tanzania zimezaa matunda na viongozi mashuhuri kama yeye wameanza kufurahia huduma hizo.
NIPASHE
Acha kuanguka na kupoteza kupoteza fahamu akiwa ofisini akitoka kwenye operesheni mwanzoni mwa wiki. Imebainika kuwa Mwanasheria wa Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NECM) anayesimamia zoezi la bomoa bomoa, Heche Suguti, aliwahi kutekwa na kuteswa mwaka 2012.
Nipashe limebaini kuwa Julai, 2012, tukio la kutekwa kwa Suguti liliripotiwa na vyombo vya habari ikielezwa kuwa huenda alifanyiwa kitendo hicho na waliokuwa wamewekewa alama ya X kwenye nyumba zao wakati huo.
Ilielezwa kuwa, Suguti alitekwa wakati akisimamia mpango wa ubomoaji wa mahekalu ya baadhi ya vigogo waliojenga kandokando ya mto Mbezi Beach, Mndubwe na eneo la Hifadhi ya Taifa ya Mikoko ufukweni mwa Bahari ya Hindi, jijini Dar es Salaam.
Aidha, tukio hilo lilitokea wiki chache baada ya kutekwa, kuteswa na kupigwa kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari (MAT), Dk. Steven Ulimboka.
Habari kutoka kwa ndugu wa karibu wa mtumishi huyo wa serikali zilieleza kuwa Suguti alitekwa nyara katika eneo la Leaders Club majira ya saa 4:00 usiku, wakati alipokwenda kupata vinywaji na chakula akiwa na na kuteswawadogo zake wawili.
Ilielezwa kuwa akiwa katika eneo hilo, ghafla liliibuka kundi la watu zaidi ya 10 ambao walimkamata Mwanasheria huyo mithili ya kibaka na kumpeleka eneo la giza na kisha kuanza kumpiga.
Ilielezwa kuwa Suguti aliteswa kwa muda na watu hao hadi alipookolewa na watu waliokuwa karibu na eneo hilo, ambao walishtushwa na kelele za kuomba msaada.
Kwa mujibu wa taarifa hizo ambazo zimethibitishwa na Suguti mwenyewe baada ya kutafutwa na Nipashe, tukio hilo liliripotiwa katika kituo cha polisi cha Oysterbay.
Katika kituo hicho, mwanasheria huyo alipewa PF3 na kwenda kutibiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ambako alilazwa kwa zaidi ya wiki mbili kutokana na majeraha aliyoyapata.
Ilielezwa kuwa kabla ya tukio hilo, mwanasheria huyo alikuwa akipokea simu na ujumbe wa vitisho kupitia ujumbe mfupi wa mkononi tangu NEMC ilipoanza taratibu za kutaka kubomoa mahekalu ya vigogo wa eneo la Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam.
NIPASHE
Mchakato wa kuanzisha Mahakama Maalum ya mafisadi, ambayo iliahidiwa na Rais John Magufuli kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana umeanza kupamba moto.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe, wakati akizungumza na Nipashe mwisoni mwa wiki kuhusu ahadi hiyo ya Rais Magufuli.
Dk. Mwakyembe alisema tayari Wizara yake imeanza maandalizi ya Muswada wa Sheria ya kuanzisha Mahakama Maalum ya mafisadi na kwamba utakapokamilika utawasilishwa bungeni kwa ajili ya kupitishwa na hamtiamye kuwa Sheria.
Ingawa hakutaja lini Muswada huo utakuwa tayari na kufikishwa bungeni, Dk. Mwakyembe alisema ofisi yake tayari imeanza kulifanyia kazi suala hilo kwani ahadi iliyotolewa na Rais lazima ifanyiwe kazi na majibu yapatikane.
“Nafahamu kwamba katika kampeni zake, Rais Magufuli alikuwa akiahidi kuanzisha mahakama hiyo kwa lengo la kudhibiti ubadhirifu wa fedha za umma unaofanwa na baadhi ya watumishi, kwa mantiki hiyo suala hilo limefika mezani na tunalifanyia kazi,” alisema Dk. Mwakwembe.
Alisema Wizara yake lazima italifanyia kazi suala hilo kwa kasi kubwa ili kuhakikisha Mahakama hiyo inaanzishwa mapema na muswada utakapokuwa tayari watanzania watajulishwa.
“Muwe na subira maana mambo mazuri hayataki haraka, sisi tumelipokea na tayari tunalifanyia kazi likikamilika basi wananchi watajua na nawahakikishia linafanyiwa kazi,” alisema Mwakyembe.
Katika mikutano mbalimbali ya kampeni kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Rais Magufuli wakati huo akiwa mgombea urais kwa tiketi ya CCM, alikuwa akiahidi kuwa akiingia Ikulu atasimamia kuanzishwa kwa mahakama hiyo.
Hivi karibuni, baadhi ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano walisema wanasubiri kwa hamu muswada wa kuanzishwa kwa Mahakama Maalum ya kushughulikia mafisadi na wala rushwa kama iliyoahidiwa na Rais.
Wakizungumza na Nipashe, baadhi ya wabunge hao walisema wanausubiri Muswada huo kwa hamu ili waupitishe kwa ajili ya kuanzishwa kwa mahakama hiyo itakayosaidia kuharakisha kesi za mafisadi.
Mbunge wa Jimbo la Manonga, Mkoa wa Tabora, Seif Gulamali (CCM), alisema wanatarajia serikali itapeleka muswada huo kwa ajili ya kutajwa, kuujadili na kuupitisha kwa manufaa ya wananchi kwani unaweza kutatua kero ya ufisadi, rushwa na matumizi mabaya ya fedha za serikali.
Alisema mahakama ya aina hiyo ni muhimu katika kupambana na watu wanaojinufaisha kwa kupora mali za Watanzania.
“Sisi kama wabunge bila kujali itikadi za vyama, tunausubiri kwa hamu muswada huo uletwe bungeni ili tuujadili na kuupitisha ili uwe sheria na hatimaye mahakama inayosemwa semwa ianzishwe na ianze haraka,” alisema Gulamali.
MWANANCHI
Wakazi wa Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma wanakula wadudu jamii ya viwavi jeshi, wanaojulikana kwa jina la fumbili kutokana na njaa kali iliyoikumba wilaya hiyo.
Hata hivyo, chakula hicho huenda kikapotea wakati wowote kutokana na mvua kutonyesha hivyo wadudu hao, ambao huishi kwa kutegemea majani, nao kupotea kwa kukosa chakula.
Mbali na fumbili, chakula kingine ambacho kilikuwa mkombozi kwa wakazi wengi, hususan Tarafa ya Chilonwa, ni matunda ya zambarau ambayo nayo yatakwisha wakati wowote kwani msimu wake umekwisha.
Chamwino ni wilaya iliyoko takriban kilomita 30 kutoka mjini Dodoma, ikikadiriwa kuwa na watu 349,714 na mazao ya chakula yanayolimwa kwenye wilaya hiyo ni mtama, uwele, mpunga, mahindi, mihogo, viazi vitamu, kunde, nyonyo, mbogamboga na choroko.
Juzi, Mbunge wa Chilonwa, Joel Mwaka aliitisha kikao cha dharura cha madiwani wote wa jimbo hilo lenye kata 14 kujadili suala hilo na kila diwani aliyechangia mjadala huo, alionyesha kujuta kugombea kwa kuwa wananchi wanamlilia.
Madiwani hao waliweka azimio la kusafiri kwenda Ikulu, Dar es Salaam kuwasilisha kilio cha wananchi wao.
Akizunguma kwenye kikao hicho, Mwaka alisema hali ya wakazi wa Chilonwa ni mbaya kiasi hakuna matumaini hata ya kupata mlo mmoja na badala yake wengi wanaishi kwa uji na matunda pori na fumbili.
Mbunge huyo alilaani mpango wa Serikali wa kuwapa vibali wafanyabiashara kwenda kuchukua mahindi katika ghala la chakula la Songea kwani bei zinakuwa kubwa.
“Ndiyo maana wanyabiashara wengi walikataa kwa kuwa bei inakuwa ni kubwa ambayo haiwezi kurudisha hata gharama zao, kitendo hicho kimefanya wafanyabiashara wa kawaida kuendelea kuwaumiza wananchi, lakini hakuna mwenye uwezo kipindi hiki, nasema walete mahindi ya bure siyo ya kununua tena,” alisema Mwaka.
Mbunge huyo alihoji ni kwa nini Serikali isiruhusu ghala la mahindi la Kizota, Dodoma kutoa mahindi kwa wafanyabiashara ili bei isiwe kubwa kama ilivyo sasa. Alisema bei ya sasa ya Sh15,000 kwa debe la kilo 20 ni kubwa na wachache ndiyo wanaoweza kuimudu.
Diwani wa Majeleko, Mussa Omari alifika kwenye kikao hicho akiwa na fumbili wengi akisema aliwakamata wakati akishirikiana na wapigakura wake kupata kitoweo.
Hata hivyo, hakuna diwani aliyeonyesha mshangao kwani kila mmoja alisema hata kwake wanakula wadudu hao na ni jambo la kawaida. Mussa alisema hali ni mbaya zaidi kwenye kata yake na tayari baadhi ya watu wameanza kuvimba miguu kwa kukosa chakula, huku kukiwa na taarifa za vifo vinavyosadikiwa kuwa vimetokana na watu kukosa lishe.
Diwani wa Zajilwa, Farida Maulidi alisema katika eneo lake, kuna kaya 10 ambazo zimeelemewa zaidi na tayari kuna taarifa za vifo viwili.
“Kwangu hali ni mbaya sana yaani naomba tuandamane kwenda hata kwa mkuu wa mkoa au niungane na wenzangu twendeni Ikulu tukamuone Rais. Mbona, pamoja na kusema hakuna mtu atakayekufa kwa njaa, huku watu wanateketea na sisi tupo? Kila siku nafanya kazi ya kutafuta uji kunusuru maisha ya watu wangu,” alisema Maulid.
Ofisa kilimo wa wilaya hiyo, Godfrey Mnyamale alikiri kuwa hali ni mbaya wilayani Chamwino na kusema kama juhudi za makusudi hazitachukulia ndani ya wiki moja, kutakuwa na madhara makubwa.
MWANANCHI
Aliyekuwa Meneja wa kampeni za mgombea urais wa CCM, Abdalah Bulembo amesema haoni dosari katika uamuzi wa kufuta uchaguzi wa Zanzibar na kumshauri mtoto wa aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Fatma Karume akae pembeni badala ya kuwachanganya wananchi.
Bulembo alisema katika mahojiano maalumu na gazeti hili kuwa, uchaguzi wa Zanzibar ulifanyika na kufutwa kwa mujibu wa sheria, hivyo siyo vyema Fatma akatoa kauli za kuchanganya watu. “Fatma Karume ni nani kusema maneno hayo.
Ukizaliwa katika familia ya rais, so who are you? Namshauri (Fatma) akae pembeni kwenye mgogoro wa Zanzibar na aendelee kuwatetea watu mahakamani,” alisema.
Alichosema Fatma Kauli ya Bulembo imekuja siku kadhaa baada ya Fatma kumshauri Rais wa Zanzibar, Ali Mohammed Shein kuachia madaraka kwa kuwa kuendelea kubakia ni kuwanyang’anya Wazanzibari haki yao ya msingi.
Alisema mzozo wa Zanzibar umesababishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanziba (ZEC), Jecha Salum Jecha kutangaza kufutwa matokeo yote ya Uchaguzi Mkuu visiwani humo wakati hana mamlaka kisheria ya kufanya hivyo.
“Akidi ya vikao vya ZEC ni mwenyekiti na wajumbe wanne. Kama kikao kilifanyika akidi ilitimia na jambo hilo likakubaliwa na tume hiyo, basi waonyeshe ni wapi walipokubali wajumbe wengine.
Hata makamu mwenyekiti hajashiriki kwenye maamuzi hayo kwa sababu kisheria uchaguzi hauwezi kufutwa bila akidi hiyo. Msimamo wa Bulembo Kinyume na kauli hiyo ya Fatma, Bulembo alisema kufutwa uchaguzi wa Zanzibar siyo doa kwa sababu ZEC ipo kisheria na sheria inazuia kuhoji uamuzi wake mahali popote.
“Uchaguzi Zanzibar utarudiwa tu kwani kwa mujibu wa sheria zetu, akishasema Mwenyekiti wa Tume amesema, hahojiwi tena popote na ndiyo maana CUF haiwezi kwenda mahakamani.
Hili ni suala la kisheria na tukitaka ifanyike vinginevyo, tubadili kwanza sheria,”alisema. Alisisitiza kuwa watu wenye uelewa kama Fatma wanapaswa kuwaeleza ukweli wasioelewa.
HABARILEO
Muswada wa Sheria ya Habari ambao uliwahi kupelekwa bungeni kisha kuondolewa kimya kimya, sasa unatarajiwa kurejeshwa tena bungeni mwezi huu.
Uwezekano wa kurejeshwa tena bungeni kwa muswada huo, kunatokana na kuundwa kwa kamati ya wanahabari sita, itakayoshirikiana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye kupitia muswada huo kabla ya haujawasilishwa bungeni baadaye mwezi huu.
Akizungumza Dar es Salaam jana na wahariri wa habari wa vyombo mbalimbali vya habari nchini, Nnauye alisema serikali inathamini mchango mkubwa wa vyombo vya habari na watendaji wake, na kwamba itashirikiana nao kuhakikisha sheria bora ya habari inapatikana.
Kamati hiyo imeundwa baada ya mapendekezo ya Waziri Nnauye ambaye alitaka kamati hiyo iundwe na ikutane naye Januari 13 mwaka huu, kwa ajili ya kuanza kupitia muswada huo wa sheria ya habari.
Wanaounda kamati hiyo ni Naibu Mhariri Mtendaji wa kampuni ya TSN, Tuma Abdallah, Mhariri Mkuu wa gazeti la Nipashe, Jesse Kwayu na Mhariri Mtendaji wa gazeti la Jamhuri, Deodatus Balile.
Wengine ni Mhariri wa Upendo Media, Mengda Johanes, Prudence Constantine wa Shirika la Taifa la Utangazaji(TBC1) na Joyce Shebe wa Clouds Media.
Awali, akizungumza na wahariri hao, Nnauye alisema vyombo vya habari nchini vina mchango mkubwa katika taifa na vinapaswa kuwa na sheria inayowasimamia, ili kuhakikisha uhuru wa habari unakuwepo na pia kuwa kuwa na mipaka yake.
Nape aliongeza kuwa yeye ni muumini mzuri wa uhuru wa habari nchini, hivyo atahakikisha anatekeleza wajibu wake kwa kuharakisha mchakato wa muswada wa sheria hiyo, kwa kuhusisha wadau watoe mapendekezo kabla ya kuupeleka bungeni.
Alisema nia ya serikali kutunga sheria hiyo ni nzuri kwa kuwa inaweka utaratibu wa kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya vyombo vya habari ili kuwa na mazingira mazuri na yenye tija.
Akizungumzia masuala ya vitambulisho vya waandishi (press card), Nnauye alitoa wiki moja kwa Idara ya Habari (Maelezo) kuangalia kanuni na utaratibu mzuri wa jambo hilo na kutoa mwongozo utakaotumika kwa ajili ya utoaji vitambulisho hivyo na kwa muda gani.
“Nawapa siku saba Maelezo, mkakae, muangalie kanuni na taratibu zikoje, ili mniletee ripoti juu ya jambo hili,” alisema Waziri Nnauye. Kuhusu Muswada wenyewe Katika Bunge la Juni mwaka jana, serikali iliuondoa Muswada wa Sheria ya Haki ya Upatikanaji Habari wa mwaka 2015, uliokuwa usomwe kwa mara ya pili.
Ilieleza kuwa muswada huo utasubiri bunge jipya litakapokaa, baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka 2015. Akitoa taarifa ya kuondolewa kwa muswada huo bungeni mbele ya Naibu Spika, Job Ndugai (wakati huo), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), kwa wakati huo, Profesa Mark Mwandosya alisema, “Uamuzi wa kuuondoa umeafikiwa na Serikali baada ya Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Huduma za Jamii kuishauri hivyo.”
Mwandosya alisema sheria hiyo ya upatikanaji habari ilichapishwa Februari 20 mwaka 2015 na kusomwa bungeni kwa mara ya kwanza Machi 12 hadi Aprili mosi mwaka huo. Alisema muswada huo si wa dharura, kwa kuwa umepitia hatua mbalimbali, ikiwemo kujadiliwa na kamati hiyo Juni 22.
HABARILEO
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesisitiza kwamba ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, unatarajiwa kuanza mwezi Julai mwaka huu. Pia, Profesa Mbarawa alisema hadi Desemba mwaka jana, jumla ya wananchi 2,183 sawa na asilimia 98.69 wamelipwa fidia ya Sh bilioni 45.65 ili kupisha ujenzi wa bandari hiyo.
Profesa Mbarawa alisema ifikapo Machi mwaka huu, majadiliano ya kiufundi na kibiashara, yatakuwa yamekamilika. Alisema Januari 8, mwaka huu kuna gazeti moja la kila siku liliandika ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo utasubiri, jambo ambalo si kweli.
“Napenda kuwataarifu kuwa ujenzi wa bandari ya Bagamoyo hausubiri kukamilika kwa uongezaji wa kina cha maji katika bandari ya Dar es Salaam na uboreshaji wa bandari ya Mtwara, kama ilivyoandikwa katika gazeti hilo. Napenda kuwaarifu kwamba habari hiyo siyo sahihi na imepotosha umma,” alisema.
Jiwe la msingi Profesa Mbarawa alisema Serikali ya China, Serikali ya Oman na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zilitia saini ya makubaliano ya ujenzi wa bandari ya Bagamoyo mbele ya Rais mstaafu, Jakaya Kikwete Oktoba 16, mwaka jana, siku ya uzinduzi wa ujenzi wa bandari hiyo.
Alisema mpaka sasa kikosi kazi maalumu cha nchi hizo tatu, kipo katika hatua mbalimbali za kuandaa mikataba ya kiufundi na kibiashara kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo. Ujenzi wa bandari hiyo utagharimu Sh trilioni 21.5.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Rais Kikwete alisema ujenzi huo utakapokamilika, utakuwa ni mradi mkubwa utakaoinua uchumi wa nchi na kuongeza uwekezaji kwenye sekta nyingine. Aliwataka watanzania kuwekeza katika viwanda na sekta za huduma.
Aidha, aliwataka Watanzania kujiendeleza kielimu na mafunzo ya ufundi stadi ili waweze kupata ajira kupitia mradi huo. Alisisitiza kuwa hilo litawezekana ikiwa wananchi watadumisha amani na utulivu.
Aliwataka wananchi wa Bagamoyo kujenga ushirikiano na wawekezaji hao ili mradi huo ukamilike kwa wakati na ulete manufaa kwao na taifa. Mradi huo utakapokamilika utakuwa na uwezo kutoa tani 600,000 za shehena ya makontena 1,000 na pia utatoa ajira kwa watu zaidi ya 1,000.
HABARILEO
Askari Polisi wa kituo cha Ulyankulu wilaya ya Kaliua mkoani Tabora wamelalamikiwa kwa kudai malipo ya Sh 300,000 kutoka kwa wananchi kama gharama ya mafuta ya kuwafikisha kwenye matukio ya kihalifu.
Akizungumza na askari hao, Mbunge wa Jimbo la Ulyankulu, John Kadutu alisema hivi karibuni askari hao walidai wapewe kiasi hicho cha fedha ili waweze kufika kijiji cha Sasu kulipotokea uhalifu.
Alisema kitendo cha kudai fedha kutoka kwa wananchi ili watekeleze majukumu yao ni miongoni mwa kero walizonazo wananchi na kuwataka askari hao kuacha kuwaomba fedha wananchi kwa kuwa ni ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza shughuli za utekelezaji wa majukumu yao.
Mbunge huyo alisema endapo askari hao watatenda haki na kuacha kuwaomba wananchi fedha za mafuta, kupokea rushwa na kuwabambika kesi hawataingiliwa katika majukumu yao na kazi yao itakuwa nyepesi kwani watapata ushirikiano mkubwa.
“Kumekuwa na malalamiko mengi juu yenu jambo ambalo linapaswa kuangaliwa… Tekelezeni majukumu yenu kwa mujibu wa taratibu zenu badala ya kutanguliza tamaa ili kujinufaisha,” alisema.
Mbunge huyo wa Ulyankulu aliwahimiza askari hao kuacha vitendo vya kukiuka haki za binadamu kwa kuwapiga watuhumiwa au kuwanyanyasa kwa namna yoyote hata kama wametii kuwa chini ya ulinzi.
Kadutu alibainisha kuwa vitendo hivyo vinazidi kuchochea chuki kutoka kwa wananchi, hali ambayo inadhoofisha dhana nzima ya polisi jamii, ulinzi shirikishi na utii wa sheria pasipo shuruti.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kaliua, Haruna Kasele, alikemea tabia ya baadhi ya askari hao kuvujisha siri wanazopewa na raia wema kuhusu uhalifu au wahusika wa uhalifu kwa nia ya kujinufaisha.
Mbunge wa Ulyankulu alifanya ziara ya siku ya tatu ya kutembelea taasisi za umma na binafsi kwa lengo la kupokea ushauri, kero na maoni kabla ya kuanza kwa vikao vya bunge Januari 26 mwaka huu.
HABARILEO
Serikali imewatoa hofu Watanzania kuhusu uwepo wa mafuta ya kutosha nchini baada ya kuamriwa kurudishwa kwa meli iliyokuwa imebeba shehena ya mafuta yenye kiwango kisichofaa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa huduma za Nishati na Maji (EWURA), Felix Ngamlagosi, alisema kuna akiba ya kutosha na hivyo watanzania wasiwe na hofu kwani kurudishwa kwa meli hiyo hakuna athari zozote kwa upande wa mafuta.
Alisema ipo akiba ya mafuta ya kutosha na kwamba Ewaura inaendelea kupokea shehena za mafuta kama kawaida na kwa kiasi kitakachoendelea kutosheleza mahitaji ya nchi. Aliongeza kuwa hadi kufikia Januari 8 mwaka huu kulikuwa na kiasi cha lita 255,052,370 kwa ajili ya soko la ndani, lita milioni 143.547 kwa ajili ya soko la nje, na lita milioni 27.875 za dizeli kwa ajili ya matumizi ya migodi.
“Wananchi wasiwe na hofu. Kilichofanywa na TBS hakijaathiri chochote. Kwa takwimu hizi ni dhahiri kuwa nchi ina akiba ya kutosha ya mafuta na bado tunaendelea kupokea,” alisema Ngamlagosi.
Aidha alisema katika kipindi cha Desemba 2015 na Januari 2016 bei za mafuta katika soko la dunia zimeendelea kushuka na kwamba bei za mafuta katika soko la Tanzania zilifuata mwenendo wa bei za mafuta katika soko la dunia.
Katika kudhibiti ubora wa mafuta, alisema Ewura inaendelea kuchukua sampuli kwenye vituo vya mafuta, maghala makubwa ya kuhifadhi mafuta na magari ya kubeba mafuta, lengo likiwa ni kukagua ubora wa mafuta.
HABARILEO
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Magalula Said Magalula amesema shule za msingi na sekondari za umma mkoani humo zimepokea zaidi ya Sh milioni 336 kwa ajili ya mpango wa elimu bure.
Magalula alisema fedha hizo zilizotolewa na serikali zitatumika kwa ajili ya mpango wa elimu bure katika shule za msingi na sekondari za umma, ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM sambamba na ahadi ya Rais John Magufuli ya elimu bure.
Kwa mujibu wa Magalula, kati ya fedha hizo, kiasi cha Sh 143,859,000 zimepelekwa katika shule za msingi zipatazo 360 wakati kiasi shilingi 212,482,000 zimeshapelekwa katika shule 105 za sekondari.
Mkuu huyo wa mkoa ameeleza kuwa kiasi hicho cha fedha kilichotolewa na serikali ni kwa ajili ya mwezi Januari mwaka huu ambapo kila mwezi serikali itakuwa ikitoa kiasi cha fedha kwa ajili ya mpango huo.
“Nawaagiza wakuu wa shule na walimu wakuu mkoani hapa wahakikishe fedha hizo zinatumika kwa mujibu wa maagizo ya serikali vinginevyo atakayekwenda kinyume hatua kali za kinidhamu na kisheria zitachukuliwa dhidi yake,” alisisitiza.
Hata hivyo, alibainisha kuwa shule mbili tu za msingi ndizo ambazo hazijapelekewa fedha hizo kutokana na kutokuwa na akaunti benki na kuongeza kuwa jitihada zimefanyika kuhakikisha zinafungua akaunti haraka iwezekanavyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Kalangasa, Manispaa ya Sumbawanga, Gabriel Hokororo, alikiri kuwa shule yake tayari imepokea kiasi cha Sh 1,400,000 kwa ajili ya mwezi Januari.
Unataka kutumiwa MSG za habari zote kubwa kutoka kwa Millard Ayo? ukiwa na line ya tiGO andika ‘AYO’ tuma kwenda 15510, msg utayotumiwa jibu OK ili uanze kupokea matukio yote kwa sms, pia ungana na Millard Ayo kwenye Twitter, FB, Instagram na YouTUBE wa kubonyezahapa>>>INSTAGRAM TWITTER FB YOUTUBE.