MTANZANIA
Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamemgeuka Rais Dk. John Magufuli na kutaka kasi yake iangaliwe upya vinginevyo inaweza kukigharimu chama hicho tawala kwa wananchi.
Tangu Rais Magufuli aingie madarakani kumekuwa na hatua mbalimbali zilizochukuliwa ikiwamo kuifumua Bandari ya Dar es Salaam na kusimamisha vigogo kadhaa pamoja na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU), Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHACO) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Hatua nyingine ni kubomoa nyumba katika bonde la Msimbazi na Mkwajuni jijini Dar es Salaam na kuwafukuza wafanyakazi wageni wasio na vibali.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana, amesema baadhi ya wabunge wanaelezwa kuonyesha hofu ya hatua hizo kuwa huenda zitakigharimu chama chao kwa wananchi.
Wabunge hao wapo mjini Dodoma kwa ajili ya semina ya siku mbili yenye lengo la kupata mbinu za kupambana na kambi ya upinzani ambayo imefanikiwa kuongeza idadi ya wabunge katika Bunge la 11 litakaloanza rasmi wiki ijayo.
Taarifa kutoka chanzo cha uhakika ndani ya vikao hivyo, zilisema kuwa wabunge hao walilalamikia suala la bomoabomoa kwamba linakichafua chama chao mbele ya wananchi na kuhoji kama hakukuwa na njia nyingine za kuwahamisha wananchi hao.
“Wabunge wametaka ubomoaji usitishwe kwa waliojenga ndani ya mita 60, ila afadhali ufanywe kwa walio mabondeni kabisa. Wengine walishauri kuwa ubomoaji ungeachwa kabisa hadi mvua zianze ndipo wawaondoe,” kilisema chanzo chetu.
MTANZANIA
Uchaguzi wa kumpata meya wa Jiji la Dar es Salaam atakayemrithi Dk. Didas Masaburi unatarajiwa kufanyika Januari 23, mwaka huu.
Msemaji wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Gaston Makwembe, aliiambia gazeti hili kwa simu jana kuwa maandalizi ya uchaguzi huo yamekamilika.
“Tupo katika maandalizi ya kuhakikisha meya wa jiji anapatikana katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Jumamosi wiki hii, na vyama vyote tunatarajia kuvitumia barua ya mwaliko muda si mrefu,” alisema Makwembe.
Alisema uchaguzi huo utafanyika katika Ukumbi wa Karimjee, huku akisisitiza kuwa vyama vyote vyenye uwakilishi wa madiwani katika jiji hilo vitashiriki.
Uchaguzi huo unatarajiwa kuwa na mvutano wa aina yake kati ya vyama vinavyounda na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Hata hivyo, Ukawa wanapewa nafasi kubwa ya kushinda kiti hicho kutokana na kuwa na idadi kubwa ya madiwani ambapo wanaizidi CCM kwa jumla ya madiwani 13.
Iwapo Ukawa watafanikiwa kutwaa jiji hilo, itakuwa ni mara ya kwanza katika historia ya Tanzania kwa wapinzani kuongozakuliongoza tangu kuasisiwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992.
Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene, alitoa wito kwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kusimamia uchaguzi huo kwa amani na haki.
“Uchaguzi huu wa meya wa jiji usifanyike kama ule wa kumtafuta meya wa Ilala na Kinondoni uliokuwa na mizengwe mingi iliyochangiwa na CCM kutokubali kushindwa na wapinzani,” alisema Makene.
Diwani wa Kata ya Vijibweni, Isaya Mwita (Chadema) ndiye atapeperusha bendera ya Ukawa huku mgombea wa nafasi ya naibu meya akitarajiwa kutoka chama cha CUF.
MTANZANIA
Serikali imesema kama Shirika la Afya Duniani (WHO), litapitisha matumizi ya dawa mpya ya ugonjwa Ukimwi wataitumia, lakini kwa sasa haiwezi kuzungumzia tafiti za ugonjwa huo ambazo zipo nyingi.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Michael John, alisema kwa sasa zipo tafiti nyingi, lakini wao kama wizara wanasubiri mwongozo kutoka WHO ambao ndiyo unathibitisha ubora wa dawa na matumizi yake.
“Zipo tafiti nyingi tunazisikia zinafanyika, lakini hili la Ukimwi ni mapema mno kulizungumzia ila kinachohitajika ni kusubiri mwongozo wa WHO ambao ndio wanatuongoza kwenye orodha ya dawa na matumizi yake katika magonjwa mbalimbali,” alisema John.
Juzi mashirika mbalimbali ya habari yalitoa taarifa juu ya utafiti mpya wa dawa ya mseto ya kimiminika ijulikanayo kama PrEP ambayo inatarajiwa kuleta faraja kwa wenza ambao mmoja anaishi na virusi vya Ukimwi huku mwingine akiwa hana.
Dawa hiyo inadaiwa tayari imeanza kutumika kwa baadhi ya mashoga nchini Uingereza na Marekani ambapo huweza kuondoa hatari ya kuambukizwa hadi asilimia sifuri.
Pia itaondoa changamoto iliyokuwapo katika njia namba moja ikiwa pamoja na kujikinga na virusi vya Ukimwi, yaani kutumia kondomu wakati wa kufanya tendo la ndoa.
Kutokana na matumizi ya kondomu wenzi hao walikuwa hawawezi kupata watoto bila uwezekano wa kuhatarisha afya ya mwenzi ambaye hana VVU.
MTANZANIA
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, mwanamke mmoja amepanda katika paa la jengo la Wizara ya Fedha na Mipango huku tukio hilo likizua sintofahamu kwa wafanyakazi wa wizara hiyo na wapita njia.
Tukio hilo lilitokea jana Dar es Salaam majira ya asubuhi ambapo mwanamke huyo anayedaiwa kuwa raia wa Kenya alipanda juu ya paa hilo na kuanza kupiga kelele.
Katika tukio hilo inadaiwa mwanamke huyo aliwasili katika eneo hilo la wizara akionekana kama mmoja wa wananchi ambao walikwenda kwa ajili ya kupatiwa huduma, lakini baada ya muda alionekana akiwa juu ya paa huku akipiga kelele.
Mwanamke huyo aliyekuwa amebeba mkoba, ambaye haikufahamika mara moja nia yake ya kupanda juu ya paa hilo, ilimchukua saa kadhaa akiwa juu na pale walinzi wanaolinda ofisi za wizara hiyo walipokwenda katika eneo hilo na kumwomba ateremke aligoma.
Hata hivyo hali hiyo ilionekana kutowakatisha tamaa walinzi hao wanaolinda majengo ya Wizara ya Fedha na Mipango yaliyopo mita chache kutoka Ikulu ya Dar e Salaam, ambao walikwenda tena wakiwa na ngazi na kuanza kumbembeleza ambapo jaribio hilo lilifanikiwa na mwanamke huyo kuteremka.
Wakati mwanamke huyo akiwa juu ya paa, wananchi waliokuwa chini walianza kumuuliza maswali, lakini hakusikika majibu yake kutokana na kelele za watu ambao kila mmoja aliimuuliza swali lake.
Hata hivyo mmoja wa askari wa kikosi cha Usalama Barabarani ambaye alisogea kwa karibu kumuuliza mwanamke huyo, alisema kuwa alimwambia amechukua uamuzi huo kutokana na kuteswa na askari nchini Kenya.
“Tukio hili ni la ajabu na linaibua maswali… hivi inakuwaje kwa jengo kama hili la wizara ambalo lipo jirani na Ikulu mtu anapanda juu na walinzi wapo?
“Hii inasikitisha sana na ni ajabu kwa kweli, ipo siku tutakuta watu wanaingia Ikulu na kufanya mambo ya ajabu kwa viongozi wetu,” alisema mmoja wa wananchi waliokuwa katika eneo hilo ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini.
Msemaji wa wizara hiyo, Ingiahedi Mduma ili kuzungumzia suala hilo, alisema kwa sasa yupo mjini Dodoma katika maandalizi ya vikao vya Bunge na hana taarifa ya tukio hilo.
Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Lucas Mkondia, alisema hajapata taarifa hizo na kwamba atafuatilia tukio hilo.
HABARILEO
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imepanga kufungua viwanda vya kusindika ngozi katika mikoa ya Shinyanga, Geita na Dar es Salaam ili kutoa soko kwa ngozi za wanyama wanaochinjwa kwenye machinjio ya mikoa hiyo.
Alitoa kauli hiyo juzi jioni wakati akizungumza na baadhi ya Watanzania waishio Botswana kwenye kikao kilichofanyika kwenye Kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Gaborone (GICC) jijini Gaborone.
Waziri Mkuu alikuwa nchini Botswana kwa ziara ya siku moja, kumwakilisha Rais John Magufuli kwenye mkutano wa SADC Double Troika, yaani kikao maalumu cha Wakuu wa Nchi na Serikali na Wakuu wa Nchi wanaounda Chombo cha Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama uliofanyika GICC jijini Gaborone.
Akizungumza na Watanzania hao, Waziri Mkuu alisema: “Tumeamua kufungua viwanda vya kusindika ngozi kwenye mikoa ya Shinyanga, Geita na Dar es Salaam (kule Pugu) ili ngozi zikishachunwa, zipelekwe moja kwa moja kiwandani.”
Alisema Serikali imeamua kuongeza viwanda nchini, kama njia mojawapo ya kukuza uchumi, kuacha kuuza mali ghafi, lakini pia ni fursa ya kuongeza ajira kwa Watanzania.
Akijibu hoja zilizoainishwa kwenye risala yao, Waziri Mkuu alisema Serikali bado ina nia ya kuhamia Dodoma na kwamba itaendelea kutenga fedha zaidi ili wizara nyingi zijenge ofisi zao Dodoma.
“Serikali ilikwishaamua kwamba Dodoma ni mji wa kiserikali na Dar es Salaam ni mji wa kibiashara. Kwa sasa kuna baadhi ya wizara zimeshajenga ofisi Dodoma na kuna taasisi kama vile Benki Kuu nazo pia zimejenga ofisi zake Dodoma.
Tutaendelea kutenga fedha zaidi ili wizara nyingine zikamilishe ujenzi wa ofisi zao,” alieleza. Waziri Mkuu Majaliwa alitumia fursa hiyo kuwataka Watanzania waishio ughaibuni (Diaspora), watafute fedha za mitaji ama zao ama kupitia kwa marafiki zao ili wawekeza nyumbani (Tanzania).
“Nia ya Serikali sasa hivi ni kufungua milango kwa wawekezaji hasa wenye nia ya kujenga viwanda. Njooni nyumbani muone ni eneo gani mnaweza kuwekeza, kama mna miradi huku fungueni matawi kule nyumbani.
Serikali inajivunia uwepo wenu kwa sababu inatambua kwamba huku mliko kuna kitu mnajifunza na mnaweza kukirudisha nyumbani kwa manufaa ya Watanzania na Taifa kwa ujumla,” alisema.
Mapema, akisoma risala yao kwa niaba ya wenzake, Mwenyekiti wa Chama cha Watanzania waishio nchini Botswana (ATB), Neiman Kissasi alisema chama hicho kilianzishwa mwaka 1992 kikiwa na lengo la kuwaunganisha Watanzania waishio Botswana pamoja kujenga undugu wao na kusaidiana.
Katika risala yao, walishauri wafugaji wa Tanzania waelimishwe na kuwezeshwa kufuga kisasa na kuondokana na ufugaji wa kurandaranda. Pia waliiomba Serikali iongeze kasi ya mpango wake wa kuhamisha shughuli zote za Serikali mjini Dodoma, kwani itasaidia kupunguza matumizi ya Serikali kwa kuwa shughuli za Serikali zitakuwa zinafanyika eneo moja.
Vilevile, waliiomba Serikali ifungue fursa za kiuchumi kwenye mikoa mingine ya Tanga, Lindi, Mtwara, Pwani, Kigoma, Mbeya, Mwanza na Arusha badala ya kuziacha ziwe Dar es Salaam peke yake. “Hii itasaidia kuibua fursa za kiuchumi na kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam”, ilisema sehemu ya risala yao. Waziri Mkuu alirejea jijini Dar es Salaam juzi usiku.
HABARILEO
Shirikisho la Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo Visivyo vya Serikali (TAMONGSCO) limeliomba Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), kufanya utafiti ili kung’amua sababu za kimazingira zinazowafanya wanafunzi wafanye vibaya katika masomo ya Hisabati na Sayansi.
Katibu Mkuu wa Tamongsco, Benjamin Nkonya alisema wanaomba uchunguzi huo kwa kuwa matokeo ya hivi karibuni ya mtihani wa kidato cha pili, yaliyotangazwa na Necta yameonesha wanafunzi ambao wamefaulu mtihani huo hawakufanya vizuri katika masomo hayo.
“Somo la Hisabati ndilo somo ambalo wanafunzi wamefanya vibaya zaidi sambamba na masomo ya sayansi,” alisema Nkonya na kuomba Necta kufanya uchunguzi huo ili kubaini sababu ya wanafunzi kuendelea kufeli masomo hayo ambayo ndiyo yanaweza kuifanya Tanzania kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya 2025.
Alisema kufeli wanafunzi masomo hayo, kunatia shaka kama Tanzania itaweza kufikia njozi yake ya kuwa na uchumi wa kati unaongozwa na sayansi na teknolojia ifikapo mwaka 2025. Alisema matokeo hayo yanaendana na ukweli ulioandikwa katika Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 kwamba Tanzania inakabiliwa na uhaba wa walimu wa sayansi 26,998 kati ya walimu 48,407 wanaohitajika.
“Upungufu huu ni sawa na asilimia 55.8 ya jumla ya mahitaji ya walimu wa sayansi nchini,” alisema Katibu huyo na kuongeza kuwa hali hiyo si ya kujivunia hata kidogo. Alishauri Serikali iondoe vibali vya kufanya kazi na kuishi nchini kwa walimu wanaofundisha masomo ya Sayansi na Hisabati kutoka ndani ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ili shule ziajiri walimu hao kutoka nje ya nchi ambako kuna ziada ya walimu.
“Kwa sasa shule hazina uwezo huo kwa kuwa mwalimu mmoja kumtafutia kibali cha kuishi nchini na kufanya kazi nchini kinagharimu shilingi milioni saba. Hiki ni kiasi kikubwa ambacho kinatosha kujenga darasa moja, lakini tukiondoa vibali hivi tunaweza kuajiri walimu kutoka ndani ya jumuiya yetu,” alifafanua.
Nkonya pia alisema licha ya shule binafsi kuongoza kwenye mtihani wa kidato cha pili, lakini alisema hawaoni fahari kujivunia jambo hilo kwani wanafunzi wengi pia wamefeli somo la Kiingereza.
Alisema kinachosikitisha ni kuona kwamba somo la Kiingereza linalotumika kama lugha ya kufundishia, limo katika orodha ya masomo ambayo wanafunzi wamefanya vibaya zaidi. “Tamongsco tunabaki tunajiuliza itawezekanaje mwanafunzi afanye vizuri katika masomo wakati lugha inayotumika kumfundishia haielewi? alihoji Katibu Mkuu huyo.
NIPASHE
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kigoma imemuachia huru aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini, David Kafulila, baada ya upande wa mashtaka kushindwa kupeleka mashahidi mahakamani hapo kwa zaidi ya siku 60 kwa mujibu wa kifungo cha 25 cha kanuni ya adhabu.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo Slivester Kainda, katika kesi iliyokuwa ikimkabili Kafulila akidaiwa kutoa lugha ya matusi dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Hadija Nyembo.
Akitoa uamuzi huo Kainda alisema: “Kesi hii ni ya muda mrefu sana na upande wa mashtaka umeshindwa kuleta mashahidi na wakati mashahidi hao wanaishi hapa Kigoma, hivyo kutokana na upande wa mashtaka kushindwa kuleta mashahidi ninaifuta kesi hii”.
Hakimu Kainda alifuta kesi hiyo baada ya upande wa mashtaka ukioongozwa na wakili wa serikali, Shabani Masanja, kudai mahakamani hapo kuwa haukua na mashahidi na kuomba ipangwe tarehe nyingine ya kesi hiyo kutajwa.
“Mheshimiwa kwa leo (jana)hatuna mashahidi, tunaomba mahakama yako tukufu ipange tarehe nyingine ya kutajwa ili tulete mashahidi,” aliomba wakili huyo.
Awali akisoma hati ya mashitaka, Wakili wa Serikali, Shabani Masanja, alidai kuwa, Agosti 1, mwaka 2013, majira ya jioni katika uwanja wa Rest House, kata ya Nguruka, wilaya ya Uvinza, mkoani Kigoma, mshtakiwa akiwa Mbunge akiwa kwenye mkutano wa hadhara alitoa lugha ya matusi dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Nyembo.
Alidai mshtakiwa huyo akiwa kwenye mkutano huo wa hadhara, alitamka kuwa “Mtu kama Hadija Nyembo unamuokota wapi na kumpa ukuu wa wilaya, unamchukua shangingi la mjini uko unasema aliwahi kuwa mkuu wa wilaya, mkuu wa wilaya akija hapa maana yake polisi wa wampigie saluti, kuna polisi wenye akili hapa kuliko huyu mkuu wa wilaya, wanampigia saluti basi tu manake hana hakili.”
Alidai lugha hiyo ilimdhalilisha mkuu huyo wa wilaya na kwamba kitendo hicho kingeweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Masanja alisema upande wa mashtaka ulipanga kupeleka mahakamani hapo mashahidi sita na kielelezo kimoja cha CD yenye maneno ya kashfa yaliyotolewa na mshtakiwa.
NIPASHE
Siri kubwa imejificha kuhusu ujenzi wa jengo la biashara na makazi unaoendelea mtaa wa Mchikichi, Kariakoo jijini Dar es Salaam ambalo limesababisha sehemu ya ghorofa lililopo mkabala nalo kutitia.
Wakati mkandarasi wa jengo linalojengwa, Salum Nassor, akisema taratibu zote za ujenzi zimefuatwa, mmiliki wa eneo, P.M. Aloyce, amewahamisha wapangaji na wamiliki wa ghorofa hilo juzi kutokana na hofu ya kudondoka.
Akizungumza na Nipashe nje ya jengo hilo, mkandarasi Nassor alikiri sehemu ya nyumba yenye ghorofa nne lililopo mkabala na eneo analolisimia kwa ujenzi, kupata tatizo.
Alisema nyumba hiyo ambayo imepata tatizo hilo ni ya muda mrefu na kwamba Jumamosi walipoanza kuchimba siku iliyofuata, waliona sehemu ya baraza la nyumba hiyo ikititia.
“Tumeanza kuchukua hatua kwa kuvunja baraza ili lisisababishe madhara, tutalijenga upya, kitaalam nyumba na nyumba zinatakiwa ziache mita tatu, ila ujenzi wa huku si mnaujua, pale wanashirikiana alama za mipaka,” alisema.
Aidha, alisema mmiliki wa ujenzi anaousimamia, alikutana na wapangaji pamoja na wamiliki nyumba hiyo ya ghorofa na kuwataka wahame na atawalipia kodi wanakokwenda kupanga.
“Alifanya hivyo baada ya hofu kutanda kuwa ghorofa litaanguka, jana (juzi), kilichotokea ni kwamba baada ya watu hawa kuhama, nimesikia ahadi haikutimizwa ya kuwalipia nyumba walizopata, ndiyo maana simu zikapigwa kwenu, yeye alimwaga mboga wao wamemwaga ugali,” alisema.
Alibainisha kuwa nyumba hiyo haitadondoka kwa sababu kitaalam tendo hilo lisingechukua zaidi ya saa 12.
Alisema ujenzi unaoendelea hivi sasa ni kukarabati baraza iliyotitia, kisha waendelee na ujenzi.
“Ujenzi wa hapa umeanzia chini tofauti na nyumba hii ya zamani ambayo ulikuwa wa kawaida,” alisema.
Msimamizi Mkuu wa ujenzi huo, Maneno Mbeyu, alisema jengo ambalo baraza lake limetitia, ujenzi wake ulishuka chini mita tatu wakati wakwao ni mita nne.
Alisema baada ya kufika mita nne, ndiyo sehemu ya baraza ya ghorofa hilo iliyokuwa na familia zaidi ya 15 ikaanza kutitia.
Mkuu wa Operesheni kutoka Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, Emmanuel Kibona, alisema hatua za awali walizochukua ni pamoja na kuvitaka vibali vya ujenzi wa majengo hayo ili wavichunguze.
Mmoja wa wamiliki wa sehemu ya jengo hilo lililotitia, Mohamed Zakaria, alisema walianza kuona ufa ulioanzia mbele ya jengo hilo kuelekea nyuma.
Alisema baada ya kuona hivyo, waliwahamisha watu waliokuwa juu ya jengo hilo kwa madai ya kuwalipia pango.
Mjumbe wa shina namba 7, Kariakoo Mashariki, Ramadhan Nassor, alisema anachojua ni kwamba baada ya tatizo hilo, mmiliki wa ujenzi unaoendelea aliwataka watu wahame kwa gharama zake.
NIPASHE
Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamefunguliwa milango na chama chao kuhakikisha wanaibana serikali itekeleze ilani na kuziba mianya ya ubadhirifu wa fedha za umma.
Hatua hiyo imelenga kuhakikisha kwamba wapinzani wanakosa hoja za kuidhoofisha serikali bungeni.
Wabunge wa vyama vya upinzani wamekuwa wakiibana serikali kwa kuikosoa na kufichua mianya yote ya ufisadi inayofanywa viongozi mbalimbali waliopo madarakani.
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, ndiye aliyetoa rungu hilo katika semina ya siku mbili ya wabunge wa chama hicho iliyofanyika Makao Makuu ya CCM mjini hapa jana.
Kikao hicho kilianza juzi chini ya Kinana, na kwa siku ya kwanza kinadaiwa kilikuwa na ajenda tatu; wajibu wa wabunge wa CCM kwa serikali, tathmini ya uchaguzi mkuu na mchakato wa kura za maoni ndani ya Chama, huku siku ya pili ambayo ni jana kulikuwa na ajenda moja ya Ilani ya chama hicho na namna ya kuitekeleza.
Mbali na hilo, Kinana aliwataka wabunge kuhakikisha wanapambana ili sheria zote kandamizi kwa wananchi zifutwe, jambo litakalowawekea wananchi mazingira mazuri.
Hata hivyo, katika ajenda ya wajibu wa wabunge wa CCM kwa serikali kwenye mfumo wa vyama vingi, iliwasilishwa na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Pius Msekwa, ambayo ilibainisha namna ambavyo kambi ya upinzani bungeni ilivyo na mkakati wa kuidhoofisha serikali ili katika uchaguzi wao wachukue madaraka.
Katika mada hiyo, Msekwa aliwataka wabunge wa CCM kutafuta mbinu za kujilinda na kujitetea ili wapinzani wakose hoja za kuidhoofisha serikali.
“Wajibu wa kila mbunge wa CCM ni kuiwezesha serikali ya chama chake kutekeleza majukumu yaliyoahidiwa katika ilani ya uchaguzi kwa kupitisha miswada ya sheria inayowasilishwa na serikali kwa madhumuni hayo, ikiwamo bajeti zinazopendekezwa na serikali,” ilieleza sehemu ya mada hiyo iliyowasilishwa na Msekwa.
Aidha, Msekwa alisema ni halali kabisa kwa wabunge wa CCM kutumia wingi wao kuidhinisha maombi ya bajeti yanayopelekwa bungeni na serikali ili kuiwezesha kutimiza ahadi zilizotolewa kwa wananchi kupitia ilani ya uchaguzi ya Chama.
Kwa upande wa Kinana, aliwataka wabunge hao ‘kufinya’ hoja ili isiwe kazi ya wapinzani kuchokonoa moto, jambo litakalowafanya kukosa mwanya wa kuilipua serikali.
“Katibu Mkuu katutaka tufanye kazi kama wabunge, tutetee na wananchi na amesema hakuna kamati kuu iliyoagiza wabunge wasiibane serikali, hasa Kinana anachotaka ni nchi hii kufanikiwa kwa kuziba mianya yote ya ubadhirifu wa fedha za umma na kutatua matatizo yanayowakabili wananchi ili wapinzani wakose hoja,” walisema baadhi ya wabunge katika semina hiyo.
Kuhusu kufuta kodi ambazo ni mzigo kwa wananchi, wabunge hao wamejadili na kukubaliana namna ya kuhakikisha wanaondoa kodi mzigo ambazo ni kero kwa wananchi na kandamizi.
Inadaiwa miongoni mwa kodi ambazo ni mzigo kwa wananchi ni kodi ya Ewura ambayo ina kodi ya ukaguzi, uthibiti ambazo ni kitu kimoja, hivyo zitachambuliwa na kufutwa ili kuleta unafuu kwa wananchi, hivyo kusaidia hata bei ya mafuta kushuka.
Hata hivyo, wakichangia mijadala baadhi ya wabunge wametaka kuwapo na bandari ya nchi kavu mkoani Dodoma kwa kuwa ni mkoa wa kati ambao ni rahisi kwa kila sehemu kuchukulia mizigo yake hata nchi za jirani.
Aidha, wabunge wengi wametaka upatikanaji wa maji mijini na vijijini huku wengi wakisema yasipopatikana itakuwa ni hati hati kwa CCM kushinda uchaguzi ujao kwa hofu ya kusulubiwa na wapigakura wanawake ambao hiyo ndiyo kero yao kubwa.
Kuhusu sheria kandamizi, Kinana aliwaambia wabunge hao kuwa sheria zingine za mkoloni mpaka sasa zipo na kwamba hazimsaidii mwananchi wa kawaida.
Kadhalika katika kikao hicho Kinana alisema vyombo vya habari vinapendwa lakini wabunge hao wajitahidi kutunga sheria hasa itakayotetea maslahi kwa waandishi wa habari.
“Katibu Mkuu anasema ikiwekwa sheria ya aina hiyo, waandishi kulipwa vizuri hasa kwenye vyombo binafsi, magazeti mengine yatakufa yenyewe huna haja ya kugombana nayo, maana mwandishi anatakiwa aajiriwe na apate haki zake…hii itafanya kusiwe na uholela holela wa kusajili magazeti wakati mmiliki hana uwezo wa kuajiri na matokeo yake utakuta gazeti habari zake nyingi na mwandishi wetu,” alisema mmoja wa wabunge ambaye aliomba hifadhi ya jina lake.
NIPASHE
Wakati fukuto la bomoabomoa likiendelea katika maeneo mbalimbali nchini, imedaiwa kuwa mamia ya watu wanaooneka kwenye maeneo ambayo nyumba zimebomolewa, si waaathirika bali hukaa humo mchana tu.
Uchunguzi katika eneo la Mkwajuni, jijini Dar es Salaam, umebaini kuwa matapeli hao wamefikia hatua ya kujenga vibanda kwenye vifusi ambavyo serikali ilibomoa nyumba za wahusika.
Licha ya kuwapo kwa matapeli hao, gazeti hili lilibaini pia kwamba watu wachache waliobomolewa nyumba zao katika eneo hilo, bado wanaishi hapo kutokana na kile walidai ni kukosa sehemu ya kwenda.
Wizara ya Aridhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), lilibomoa zaidi ya nyumba 600 za wakazi wa eneo la Mkwajuni waliokuwa wamezijenga pembezoni mwa Mto Msimbazi. Juzi pia serikali ilivunja vibanda 186 vilivyokuwa vimejengwa juu ya vifusi hivyo.
Baadhi ya wananchi wa eneo hilo, waliiambia Nipashe kwamba baadhi ya watu waliondoka eneo hilo hata baada ya bomoabomoa, lakini baada ya kusikia kuna uwezekano wa kupewa fidia, wakaamua kurudi.
“Si kwamba hawa si wakazi. Walikuwa hapa na nyumba zao tunazifahamu, sema wenzetu kidogo wamefanikiwa kuhama lakini baada ya kusikia kuna kuorodheshwa majina, wamerudi ili wapate chochote kitu endapo serikali itatoa msaada,” alisema Fatma Abasi.
Alisema walio na mahitaji ya kweli hawakuondoka eneo hilo tangu Desemba 17 walipoanza kubomolewa.
Fatma ambaye awali alijenga kibanda kilichoezekwa na mabati na mbao lakini kikabomolewa wiki iliyopita, kwa sasa amejiegesha kado ya bonde hilo akisubiri kupata msaada wa aina yoyote kutoka serikalini.
“Nina watoto wawili na mume, maisha tunayoishi ni ya kulala hapa unapopaona (mwonekano wa nzi na majitaka yaliyotuama) hakuna masaada wowote na sina pa kwenda na familia yangu ndiyo maana hadi leo nimekaa hapa,” alisema Fatma.
Mkazi mwingine wa eneo hilo, Mgasa Wambura, alikiri kuwapo kwa watu wasio waathirika akisema miongoni mwao ni waliofunga barabara ya Kawawa juzi kwa kuchoma matairi.
MWANANCHI
Kila kukicha watu hubuni mbinu ili wafanikiwe kwenye jambo fulani. Hivi ndivyo ilivyotokea Januari 16, kwa Ukawa kuja na mbinu ya kununua kalamu maalumu ya kuandikia na kupiga picha wakati wa upigaji kura wa uchaguzi wa mameya wa manispaa za Kinondoni na Ilala za jijini Dar es Salaam.
Katika uchaguzi huo, Diwani wa Ubungo (CHADEMA), Boniface Jacob alishinda umeya wa Kinondoni kwa kura 38 dhidi ya 20 alizopata Benjamin Sitta wa CCM.
Naibu Meya alichaguliwa Jumanne Mbunju wa Kata ya Tandale (CUF) aliyepata kura 38 dhidi ya 19 za John Manyama (CCM).
Kwa upande wa Ilala, aliyeshinda ni Charles Kuyeko (CHADEMA) aliyepata kura 31 na naibu ni Omari Kumbilamoto (CUF) ambaye pia alipata kura 31 za madiwani wa Ukawa baada ya wale wa CCM kususia.
Kabla ya uchaguzi huo, kulikuwa na vuta nikuvute na ushindani mkali, hali iliyosababisha Ukawa kuwa na wasiwasi wa kuhujumiwa na hivyo kuandaa mazingira ya kushinda, ikiwamo kununua kalamu hizo.
Kwa mujibu wa ofisa mmoja wa Ukawa ambaye hakutaka kutajwa jina lake, viongozi walibuni mkakati huo uliowagharimu takriban Sh30 milioni katika ununuzi wa kalamu za kupigia kura na wakati huo huo kuwapiga picha wanaozitumia na kuandaa sehemu ya kufuatilia jinsi kura zilivyopigwa.
Kila mjumbe alipewa kalamu yenye jina lake na kuitumia katika upigaji wa kura.
Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee alisema kuwa waliamua kufanya hivyo baada ya Manispaa ya Temeke ambako madiwani wawili Ukawa waliipigia kura CCM.
“Ukiumwa na nyoka lazima ukiona jani ushtuke, hiki ndiyo tulichokifanya baada ya madiwani wetu wawili kutusaliti,” alisema Mdee.
Alisema walishanusa harafu ya rushwa kwa baadhi ya madiwani wao kuhongwa fedha kupitia kwa mmoja wa maofisa wa Chadema makao makuu. Alisema baada kusikia taarifa hizo, walikaa chini na kutafakari na kuja na mbinu hiyo ambayo imekuwa mwarobani wa kuhakikisha Ukawa wanapata kura sahihi za wajumbe wake.
“Wanakinondoni wangetushangaa kama tungekosa umeya kwa idadi ya madiwani waliotupatia,” alisema Mdee ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha). “Kuna wajumbe mnakubaliana vizuri, lakini wakifika kwenye sanduku la kura wanabadilika.
Kalamu imetusadia sana kwani tulikuwa 38, CCM 20, kura zilivyopigwa tulizipata zote kama tulivyotarajia,” alisema.
Alifafanua kuwa walimweka mtu maalumu wa kufuatilia mwenendo wa kila mjumbe wa Ukawa wakati wa kupiga kura. “Kama nilivyosema juzi zile kalamu ukifungua tu ina kamera. Ukianza kuitumia kuna mtu maalumu aliyetarishwa kwa ajili ya kuangalia wajumbe wote wa Ukawa wanaopiga kura,” alisema.
Hata hivyo, alisema licha ya baadhi ya wajumbe wa Ukawa kuchukua fedha, lakini wametimiza wajibu wao wa kuhakikisha meya anakuwa chini ya umoja huo na iwe fundisho siku nyingine kwa wajumbe wao wengine.
Akizungumzia umeya wa Dar es Salaam, Mdee alisema wanajipanga vyema ili kuhakikisha jiji hilo linakuwa chini ya Ukawa kwa kuwa wana hazina kubwa ya madiwani wakataowawezesha kuibuka kidedea. “Kwenye umeya wa Jiji tutakuja na staili tofauti, hizi tulizozitumia katika manispaa za Ilala na Kinondoni, tunaziboresha na tuna uhakika wa kunyakua umeya wa Dar es Salaam,” alisema Mdee.
Unataka kutumiwa MSG za habari zote kubwa kutoka kwa Millard Ayo? ukiwa na line ya tiGO andika ‘AYO’ tuma kwenda 15510, msg utayotumiwa jibu OK ili uanze kupokea matukio yote kwa sms, pia ungana na Millard Ayo kwenye Twitter, FB, Instagram na YouTUBE kwa kubonyeza hapa >>>INSTAGRAM TWITTER FB YOUTUBE.