NIPASHE
Jumla ya wanafunzi 108,829 sawa na asilimia 11.13 kati ya 977,886 waliofanya mtihani wa kitaifa wa darasa la nne mwaka jana, wanatakiwa kukariri darasa baada ya kupata ufaulu usioridhisha.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa jana na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania, Dk. Charles Msonde, somo lililofanya vibaya kwa kupata kiwango cha chini cha ufaulu ni Kiingereza.
Akitoa matokeo hayo jana, Dk. Msonde alisema kiwango cha ufaulu kwa somo la Kiingereza ni wa chini zaidi kwa asilimia 65.67 wakati Sayansi ufaulu wake ukiwa juu kwa asilimia 89.44.
Alisema jumla ya wanafunzi 1,037,305 waliosajiliwa kufanya upimaji huo kitaifa, wasichana walikuwa ni 535,273 sawa na asilimia 51.60 na wavulana walikuwa ni 502,032 sawa na asilimia 48.40.
Alisema wanafunzi 977,886 sawa na asilimia 94.27 ya waliosajiliwa, walifanya upimaji huo na kati yao wasichana walikuwa ni 510,211 sawa na asilimia 95.32 na wavulana walikuwa ni 467,675 sawa na asilimia 93.16.
Alisema wanafunzi 59,419 sawa na asilimia 5.73, hawakufanya upimaji huo ambapo wasichana ni 25,062 sawa na asilimia 4.68 na wavulana ni 34,357 sawa na asilimia 6.84.
Dk. Msonde alisema jumla ya wanafunzi 869,057 kati ya 977,886, wamepata alama zenye daraja la ufaulu wa A, B,C na D.
Alisema wanafunzi 108,829 wamepata daraja la E lenye ufaulu usioridhisha.
Katibu huyo alisema iliyoongoza ni Shule ya Msingi Alliance ikifuatiwa na Waja Springs, St. Peter, Tumaini, Furaha, Acacia Land, Tusiime, Imani, Kaizirege na Evenezer.
Aliitaja kuwa ni Dar es Salaam ambayo imeongoza ikifuatiwa na Iringa, Kilimanjaro, Njombe, Arusha, Tanga, Geita, Kagera, Mwanza na Shinyanga.
Halmashauri 10 zilizofanya vizuri alizitaja kuwa ni Ilala, Moshi, Mji Njombe, Arusha, Mji Makambako, Tanga Mjini, Arusha, Mufindi, Hai na Bukoba Manispaa.
NIPASHE
Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, jana ilifuta kesi ya kupinga matokeo ya ubunge yaliyompa ushindi Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lisu (CHADEMA) katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana.
Mdai katika kesi hiyo, ambaye pia alikuwa mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM, Jonathan Njau, aliamua kuiondoa kesi hiyo kwa madai kuwa inampotezea muda wa kufanya shughuli zingine ikiwa ni pamoja na kushindwa kulipa gharama za kuendesha kesi, Sh. milioni 15.
Katika shauri hilo Njau alikuwa akilalamikia utaratibu uliotumika katika kuhesabu kura zilizompa ushindi Lissu, hivyo akataka kura hizo zirudiwe kuhesabiwa upya, jambo lililopingwa na mhusika.
Mbele ya Jaji Barker Sahel, Wakili wa Njau, Geofrey Wasonga, alisema mteja wake ameamua kuifuta kesi hiyo ili kumpa nafasi ya kufanya majukumu mengine pamoja na kumpa uhuru Lissu wa kutekeleza majukumu yake ya kibunge.
Lissu alisema alikuwa na uhakika wa kushinda kesi hiyo kwa kuwa ilikuwa na makosa mengi ya kisheria yanayolingana na ile ya kipindi kilichopita.
Lissu alisema kabla ya kufutwa kwa shauri hilo, mdai alishawasilisha mara mbili maombi ya kutaka kupunguziwa gaharama za kesi na imepita zaidi ya miezi miwili ameshindwa kulipa.
Alisema latika kesi hiyo aliweka mapingamizi sita na hata kama angelipa gharama hizo asingeweza kuyavuka kwa kuwa kesi hiyo ilifunguliwa kwa ushabiki wa kisiasa.
Wakili aliyekuwa akisaidiana na Lissu, Fred Kalonga alisema walijiandaa kikamilifu katika kesi hiyo na kwamba wangeshinda mapema kuliko ilivyokuwa mwaka 2010, katika kesi iliyofunguliwa na wananchama watatu wa CCM.
NIPASHE
Rais John Magufuli amesema nchi yetu ni tajiri na inarasilimali nyingi ila baadhi ya matajiri ambao ni mafisadi ndio wanasababisha ionekana maskini jambo ambalo ameahidi kula nao sahani moja.
Aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Arusha waliojitokeza barabarani kumpokea huku wakimuomba aendelee kutumbua majipu.
Alisema Tanzania inarasilimali nyingi ikiwamo Tanzanite bali kuna baadhi ya matajiri ambao wanapenda kujilimbikizia mali na wamekuwa wakifanya ufisadi na kusababisha baadhi ya wananchi kuendelea kuwa maskini pamoja na nchi yetu.
“Nasema hivi, kuanzia sasa nipo tayari kulala mbele na mafisadi wote na pia nawapa onyo kali wale walimu ambao bado wanatoza ada shuleni, iwapo nitagundua mwalimu yeyote anayetoza hela naahidi nitalala naye mbele, na katika hili, sitalifanyia masihara hata kidogo,”alisema Magufuli.
Aidha, aliwaambia wananchi kuwa kuanzia sasa elimu ni bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari na serekali imeshaweka mipango hiyo tayari na imeanza kutumika.
Magufuli aliwasihi wananchi wa Mkoa wa Arusha na Tanzania kwa ujumla kuendelea kufanya kazi na kusema kuwa wakati wa kampeni umeisha, mambo ya siasa yameisha sasa hivi ni wakati wa kufanya kazi tu na sio kitu kingine.
“Nasema hivi sasa hivi ni wakati wa kufanya kazi, nitaendelea kutumbua majipu kila mahali na sitamuonea huruma mtu yeyote mimi kazi yangu kubwa ni kufanya kazi tu. Wananchi napenda kuwaambia fanyeni kazi kwani hapa ni kazi tu,”alisema Magufuli.
Pia, aliongeza kuwa katika suala la barabara pia ataendelea kuliangalia na kufuatilia kama jinsi alivyokuwa anafanya alivyokuwa waziri.
Aidha, Magufuli aliomba wananchi wamweke katika maombi kila wakati wanapokuwa katika sala zao.
NIPASHE
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi imelazimika kuahirisha kwa siku mbili mfululizo, kesi ya mauaji ya mfanyabiashara, bilionea wa madini ya tanzanite, Erasto Msuya , baada ya shahidi wa tisa, Inspekta Samuel Maimu , kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upepelezi wa Mkoa wa Kilimanjaro (RCO), kuugua ghafla wakati akitoa ushahidi.
Shahidi huyo, aliyeanza kutoa ushahidi wake juzi, aliugua ghafla jana na kupelekwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Kilimanjaro (Mawenzi) kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Msuya aliuawa kwa kupigwa risasi, Agosti 7, mwaka 2013, saa 6:30 mchana katika eneo la Mijohoroni, kando kando ya Barabara Kuu ya Arusha-Moshi, karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Kabla ya kuahirishwa kwa kesi hiyo ya mauaji ya kukusudia, Wakili Mkuu wa Serikali, Neema Mwanda, akiwa mbele ya Jaji Salma Maghimbi anayesikiliza shauri hilo, alidai kuwa kesi hiyo ilikuwa iendelee jana kwa ajili ya kusikiliza ushahidi kutoka kwa shahidi wa tisa wa upande wa mashtaka ambaye hakumaliza kutoa ushahidi kutokana na kuugua ghafla juzi wakati akitoa ushahidi wake.
Wakili Neema alidai: “Mheshimiwa Jaji, kwa bahati mbaya shahidi wetu (Inspekta Samuel), jana (juzi) alipata tatizo la kiafya akiwa anatoa ushahidi wake mahakamani na alienda kupatiwa matibabu Hospitali ya Mawenzi na kwa taarifa tulizo nazo, bado anaendelea na matibabu.
“Tumeshindwa kupata taarifa ya daktari na leo (jana), alikuwa achukuliwe vipimo. Kwa maana hiyo upande wa mashtaka tunaomba kesi hii iahirishwe hadi Jumatatu ijayo ili tuweze kufuatilia afya yake na tuwasilishe mahakamani taarifa ya daktari, kuhusu uchunguzi wa afya yake na matibabu aliyopata.
Baada ya Neema kutoa hoja hiyo, Jaji Salma alilihoji jopo la mawakili wa upande wa utetezi iwapo wana pingamizi kuhusu hoja ya kuahirishwa kwa kesi hiyo. Kiongozi wa jopo hilo, Wakili John Lundu, alisimama na kuieleza mahakama kwamba kutokana na sababu zilizotolewa, hawana pingamizi na wako tayari kuahirishwa kwa kesi hiyo.
Kutokana na pande zote kuafikiana, Jaji Salma alisema mahakama hiyo imejiridhisha baada ya kupima hoja iliyotolewa na upande wa mashtaka, na kisha kuafikiwa na jopo la mawakili wa utetezi, na hivyo imeamua kuahirisha kesi hiyo hadi Jumatatu ijayo.
Washtakiwa wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Sharif Athuman (31), ambaye ni mfanyabiashara wa madini na mchimbaji mdogo, mkazi wa Kimandolu mkoani Arusha, Shaibu Saidi maarufu kama “Mredii” (38), mkazi wa Songambele, Simanjiro mkoani Manyara na Mussa Mangu (30).
Wengine ni Jalila Said (28), mkazi wa Babati mkoani Manyara, Sadiki Jabir a.k.a “Msudani” (32), mkazi wa Dar es Salaam na Lang’ata, wilaya ya Hai, Karim Kihundwa (33), mkazi wa Lawate, wilaya ya Siha na Alli Musa maarufu “Mjeshi”, mkazi wa Babati.
Katika ushahidi wake alioutoa mahakamani hapo juzi, Inspekta Maimu alidai kuwa Agosti 7, 2013 majira ya saa sita mchana, akiwa ofisini alipigiwa simu ya mkononi na RCO (Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa) wa Kilimanjaro, akimweleza kwamba kuna mauaji yametokea huko maeneo ya Bomang’ombe, kwa hiyo achuke timu ya Seene of Crime na CRT (Crisis Response Team) na waende huko.
Shahidi huyo alidai baada ya kufika eneo la mauaji, alimtambua Msuya baada ya kufanya ukaguzi na kukuta karatasi yenye jina lake ikiwa ndani ya gari lake aina ya Range Rover, rangi ya kijivu lenye namba za usajili T 800 CKF.
Alidai kuwa alilazimika kulipekua gari hilo na kukuta bastola moja, simu mbili za Samsung na Iphone zikiwa ndani ya gari hilo, huku gari hilo likiwa na namba ya utengenezaji (Chasses number), SALG A2HE 90A104163.
Aidha, shahidi huyo alidai kuwa katika eneo la tukio la mauaji ya mfanyabiashra huyo wa madini, waliokota maganda 22 ya risasi na kuukuta mwili wa marehemu ukiwa na matundu ya risasi katika mwili wake.
Aliendelea kudai kuwa kabla ya kuuchukua mwili wa marehemu na kwenda kuuhifadhi katika Hospitali ya Wilaya ya Hai (Bomang’ombe), alichora ramani ya eneo la tukio.
HABARILEO
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuna akiba ya kutosha ya chakula huku kazi ya kugawa, kupeleka maeneo yote yenye mahitaji inaendelea na hakuna Mtanzania atakayekufa kwa njaa.
Aidha, amesisitiza marufuku ya upikaji wa pombe kwa kutumia chakula cha njaa na kile cha bei nafuu ili kupunguza makali ya njaa.
Waziri Mkuu alisema hayo juzi wakati alipofanya ziara ya kutembelea kijiji cha Majereko wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma ambacho ni miongoni mwa vijiji vilivyoathirika na njaa na kuwalazimu wananchi kuishi kwa kula zambarau na baadhi ya wadudu.
Alisema kuanzia sasa ni marufuku kutumia chakula cha msaada kwa ajili ya kupikia pombe na kila mmoja awe askari wa mwenzake na watakaobainika kufanya hivyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Alisema chakula kinachotolewa na serikali ni kwa ajili ya kukabiliana na njaa na siyo kutumika kwa matumizi mengine. Alisema sasa serikali inasambaza chakula hicho katika maeneo mbalimbali nchini ni muhimu kikatumika kama ilivyokusudiwa.
“Tuna kazi ya kugawa na kupeleka maeneo yenye mahitaji makubwa,” alisema.
Alisema hivi karibuni wilaya hiyo imepatiwa tani 1,620 za chakula na kitasambazwa maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo na serikali itapeleka chakula kingine cha bure tani 40 ili wananchi wagawiwe.
“Juzi tulipeleka tani 700 kwa wananchi walioathirika na mafuriko na tutafanya hivyo ili kunusuru maisha ya wananchi,” alisema na kuongeza kuwa ghala la hifadhi ya chakula la Dodoma lina tani 12,000.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Farida Mgomi alisema wilaya hiyo ilikusudia kupata tani 68,000 katika msimu wa kilimo, lakini kutokana na mvua kuwa chache, zilipatikana tani 34,216 na hivyo kufanya kuwa na upungufu wa chakula.
HABARILEO
Wanazuoni na wadau wa sekta ya elimu wamepongeza hatua ya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako kufuta mfumo wa Wastani wa Alama (GPA), uliokuwa unatumiwa kupanga madaraja ya mitihani.
Wameeleza kuwa GPA ni mfumo uliokuwa unaficha hali halisi ya ufaulu wa mitihani katika shule za sekondari. Wamesema kurejeshwa kwa mfumo wa Divisheni katika kukokotoa madaraja ya mitihani, kutaisaidia nchi kutambua hali halisi ilivyo kwenye ufaulu wa mitihani na hata kama kutakuwa na tatizo la ufaulu, Serikali itajipanga namna ya kushughulikia kiini cha tatizo.
Wamedai mfumo wa GPA, uliletwa kisiasa na ulichangia kuwafanya wanafunzi wanaohitimu sekondari kwenda vyuo vikuu, kutokuwa na ubora kwani waliokuwa wamefeli na wale waliofaulu, wote walihesabiwa wamefaulu.
Juzi Profesa Ndalichako alitangaza kufuta mfumo wa GPA kwa maelezo kuwa mfumo huo haukupata baraka za Kamishna wa Elimu, kama ilivyokuwa imeshauriwa na wizara. Pia alisema mfumo huo umeonesha watahiniwa waliofaulu, kuonesha kiwango kidogo cha maarifa kuliko kiwango chao cha ufaulu.
Mtaalamu wa Elimu, Profesa Justinian Galabawa alisema mfumo wa GPA, ulikuwa unakiuka taratibu za upimaji na tathmini katika elimu, kwani ulikuwa hautofautishi mtahiniwa aliyefaulu na aliyefeli, bali wote walionekana wamefaulu.
Alisema jambo hilo halikuwa haki kwa sekta ya elimu, kwani sheria za mtihani lazima zipime alichofundishwa mwanafunzi na watahiniwa hao watofautishwe kwa ufaulu.
“Hebu angalia kuna ufaulu bora sana, ufaulu mzuri sana na vizuri, hawa utawatofautishaje. Hata mwanafunzi ambaye amepata GPA ya 0.3 naye anahesabiwa amefulu, kwa kweli haya yalikuwa ni maneno ya kisiasa na hayakulenga kusaidia kuboresha elimu,” alisema.
Aliwashutumu wanasiasa kuwa hawakuitendea haki sekta ya elimu, kwani waliwanyang’anya mamlaka Kamishna wa Elimu na Baraza la Mitihani na kuagiza kuanza kutumika kwa mfumo wa GPA, bila hata kushirikisha wadau.
Mkurugenzi wa Hakielimu, John Kalaghe alisema mfumo wa GPA ulianzishwa kisiasa na ndio maana Necta wameshindwa kuutetea. Alisema nchi inapoamua kubadilisha mfumo wowote wa elimu hasa wa kukokotoa alama za ufaulu wa mitihani, lazima kuwe na sababu za kisayansi.
Alisema wanasiasa walileta GPA kwa kuwa walibanwa katika kufikia malengo kwenye mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ambao ulitaka ufaulu katika mwaka wa kwanza uwe asilimia 60, mwaka wa pili asilimia 70 na mwaka wa tatu uwe asilimia 80. Alimpongeza Profesa Ndalichako kwa kurudisha mfumo wa madaraja.
“Kama watoto wanafeli, acha tujionee, ni aibu yetu kama taifa, ili tukae pamoja tutafute dawa na sio kuficha ukweli wa mambo,” alieleza.
Rais wa Chama cha Walimu (CWT), Gratian Mkoba alisema licha ya sekta ya elimu kuwa na changamoto nyingi na kufanya ufaulu kushuka, sio vizuri kuingiza siasa kuficha ukweli wa mambo kama ilivyofanyika kupitisha GPA.
Katibu wa Katibu Mkuu wa Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo binafsi Tanzania (Tamongsco), Benjamin Nkonya alisema Profesa Ndalichako ameitendea haki nchi yake kwa kufuta mfumo wa GPA na aliomba waziri huyo alindwe, kwa kile alichodai kuwa uamuzi wake unaweza kumfarakanisha na wakubwa wengine.
Mwenyekiti wa Taifa wa Tamongsco, Mrinde Mnzava alisema maamuzi aliyoyafanya Waziri ni bora na yatawasaidia wanafunzi na wazazi, ambao wengi wao walikuwa hawaielewi na kusababisha kuwepo kwa maswali mengi kutoka kwa wazazi na wanafunzi juu ya mfumo huo.
HABARILEO
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai jana alitangaza majina ya wajumbe wa kamati mbalimbali za Bunge mjini hapa.
Baadhi ya wajumbe wamehamishwa katika kamati walizokuwa awali ikiwemo Kamati ya Hesabu za Serikali ambayo Mwenyekiti wake alikuwa Zitto Kabwe, sasa amewekwa katika Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.
Ndugai alisema orodha hiyo pia imejumuisha wabunge ambao hawakuomba kupangwa katika kamati zozote na wale ambao wameomba kamati moja. Alisema Spika , Naibu Spika , Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Kiongozi wa Upinzani ni wajumbe wa Kamati ya Kanuni za Bunge.
Aliwataja wajumbe wa Kamati ya Uongozi kuwa ni pamoja na Spika Job Ndugai (Mwenyekiti), Dk Tulia Akson (Makamu Mwenyekiti), Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Mwanasheria Mkuu George Masaju, Freeman Mbowe ( Mjumbe wa Kamati ya Bajeti pamoja na Kamati ya Kanuni ya Bunge).
Wengine ni Mwenyekiti wa Haki Maadili na Madaraka ya Bunge, Mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya Ukimwi, Mwenyekiti Kamati ya Bajeti, Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda Biashara na Mazingira, Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria, Mwenyekiti wa Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa na Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.
Wajumbe wengine ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi Maliasili na Utalii, Mwenyekiti wa Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu.
Wajumbe wengine ni Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama , Mwenyekiti wa Sheria Ndogondogo, Mwenyekiti wa Kamati za Hesabu na Serikali za Mitaa , Mwenyekiti wa Hesabu za Serikali na Mwenyekiti wa Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma.
MTANZANIA
Rais Dk. John Magufuli amemteua Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue Dar es Salaam jana ilieleza kuwa uteuzi huo ulianza Januari 17 mwaka huu.
Nafasi hiyo iliachwa wazi Febuari 22, 2014 baada ya kifo cha aliyekuwa Mkuu wa Chuo hicho, Balozi Fulgence Kazaura aliyeshika wadhifa huo kwa vipindi viwili vya miaka minne.
Balozi Kazaura kwa mara ya kwanza aliteuliwa 2005 baada ya kifo cha Paul Bomani ambaye alishika wadhifa huo kuanzia 1993.
Kuteuliwa kwa Kikwete kumemfanya afuate nyayo za marais wa wastaafu waliopita; Ali Hassan Mwinyi, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala (KIU) na Benjamin Mkapa ambaye ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
MTANZANIA
Miezi michache baada ya Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Dk. Hamis Kigwangalla, kufanya ziara katika kituo cha cha tiba mbadala cha Foreplan Clinic kilichopo Ilala Dar es Salaam, mengi yamebainika.
Katika ziara hiyo ilielezwa kuwa Dk. Kigwangwalla aligundua tabibu huyo wa tiba mbadala hakuwa na vyeti lakini taarifa zilizopo zinaonyesha Dk. Mwaka na wasaidizi wake walipewa vyeti kwa mujibu wa sheria na Baraza la Tiba Asilia.
Inaelezwa kuwa Dk. Mwaka amekwisha kukabidhi vyeti hivyo kwa Serikali na MTANZANIA ina nakala zake ikiwa ni kutekeleza agizo alilopewa Desemba 16 mwaka jana na Naibu Waziri Dk. Kigwangwalla.
Dk. Kigwangwalla amekwisha kukiri kuwa vyeti hivyo vimekwisha kufikishwa wizarani na kuhakikiwa.
Kwa sababu hiyo, Mwenyekiti wa Shirikisho la Shirikisho la vyama vya Tiba Asili amesema hatua hiyo ya Dk. Kigwangwalla haikuwa sahihi bali ilisababisha malumbano kwa jamii jambo ambalo si sahihi.
“Hivyo sisi shirikisho tuliweza kukaa na wadau wa Tiba Asili na Tiba Mbadala ambao kimsingi ndiyo hasa walikwazika na agizo hilo la wizara.
“Hatimaye Desemba 31 mwaka jana tulifanya kikao cha pamoja kati ya wadau hao, shirikisho na Wizara ya Afya tukiongozwa na uenyekiti wa Waziri Ummy Mwalimu na kukubaliana baadhi ya mambo lakini si kupiga marufuku matangazo ya tiba mbadala,” alisema Lutenga.
Hata hivyo, Dk. Mwaka alisema hataki kuingia katika malumbano na Serikali na kwa sasa anasukumwa na utoaji huduma kwa jamii kama sheria inavyotaka.
Alisema kutokana na hali hiyo kituo chake kimeandaa utaratibu maalumu wa utoaji matibabu kwa wazee wenye umri wa miaka 60 na kuendelea, pamoja na watoto chini ya umri wa miaka mitano.
Alisema pamoja na misukosuko aliyoipata, Foreplan Clinic pia imejikita kusaidia jamii kama vile ujenzi wa nyumba za ibada ikiwamo misikiti na makanisa na hata kujihusisha masuala ya michezo.
MTANZANIA
Serikali imeombwa kupunguza masharti ya vibali vya walimu wa kigeni kwa kuwa yamekuwa yakisababisha wenye shule binafsi kutoza ada kubwa kufidia gharama hizo ambazo ni zaidi ya Sh milioni saba.
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyuo na Shule Binafsi Tanzania (TAMONGSCO), Mzinde Mzava, alisema endapo Serikali itapunguza masharti itawasaidia kuwapata walimu kwa gharama nafuu na gharama za ada zitapungua.
“Tunamuomba waziri mwenye dhamana ya elimu, Profesa Joyce Ndalichako na timu yake, wafikirie hili la vibali vya walimu wageni kutoka nje kwa sababu itatusaidia hata sisi kuwapata walimu wenye fani mbalimbali na kupunguza gharama za ada,”alisema Mzava.
Alisema wanalazimika kutafuta walimu kutoka nje kwa kuwa hawana mgao wa walimu wanaotoka kwenye vyuo mbalimbali vya serikali nchini.
“Hapa nchini kuna upungufu wa walimu wa sayansi 27,000 hivyo hata huko shule za serikali nako wana upungufu wa walimu…endapo serikali itapunguza masharti sote tutanufaika katika hilo,” alisema Mzava.
Pia alisema Serikali imekuwa na changamoto ya uhaba wa walimu wa shule za watoto wadogo wenye stashahada hivyo wao hulazimika kuagiza walimu kutoka nchi kama Kenya ambako kuna walimu wengi wa aina hiyo.
“Kwa hapa Tanzania walimu wa watoto wadogo ambao wanafika hadi chuo kikuu wameanza mwaka jana kuhitimu, hivyo inatulazimu nasi kuagiza nje ya nchi ili tupate elimu bora yenye kukidhi matakwa ya soko la dunia,” alisema Mzava.
Naye Makamu Mwenyekiti wa TAMONGSCO, Emmanuel Rwegenyeza, alisema elimu bora ni lazima igharamiwe kwa vile ina ushindani mkubwa katika soko la ajira.
Rwegenyeza alisema upo mchakato na serikali wa kupata ada elekezi na baada ya hapo nao watatoa msimamo wao.
“ Tunaendelea na mchakato wa pamoja na serikali…tunategemea serikali itapanga ada ya kuanzia na mwisho ni shilingi ngapi kwa shule binafsi na ndipo sisi tukapotoa msimamo wetu kama tunaridhika nayo au la…,”alisema Rwegenyeza.
Alisema shule hizo hazipo kwa ajili ya kuwaumiza wananchi kwa kutoza ada kubwa lakini kinachoangaliwa ni gharama za uendeshaji na ubora wa elimu inayotolewa.
MWANANCHI
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Serikali iliyopita, Bernard Membe ameungana na waziri mwenzake wa zamani, Dk Makongoro Mahanga kukosoa sera ya kubana matumizi ya Rais John Magufuli ya kudhibiti safari za nje na kuteua baraza dogo la mawaziri.
Kama ilivyokuwa kwa Dk Mahanga, waziri huyo aliyedumu kwa miaka tisa kwenye Wizara ya Mambo ya Nje amesema kiuhalisia, Rais hajapunguza idadi ya wizara kama alivyosema bali amepunguza “idadi ya mifuko”, huku akisisitiza kuwa mkuu huyo wa nchi atalazimika kutoka nje “atake asitake”.
Membe amekuwa waziri wa pili wa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kukosoa sera ya kubana matumizi ya Serikali ya Awamu ya Tano baada ya Dk Mahanga, ambaye sasa amehamia Chadema, kumkosoa akisema idadi ya wizara inapimwa kwa kuangalia makatibu wakuu na si wizara na hivyo ukubwa wa Baraza la Mawaziri bado uko palepale.
Katika mahojiano maalumu na Mwananchi mapema wiki hii, Membe alikuwa na maoni kama hayo na akaenda mbali zaidi kuzungumzia hata sera ya kudhibiti safari za nje na Rais kujizuia kusafiri, akisema “Tanzania haiwezi kuishi kama kisiwa” katika dunia ya leo.
Kubana matumizi Membe, ambaye alikuwamo kwenye kinyang’airo cha urais na kufika hadi tano bora, alisema Rais hajabana matumizi yoyote kwa kupunguza ukubwa wa Baraza la Mawaziri, bali alichofanya ni kupunguza idadi ya mawaziri na siyo wizara.
“Alichofanya ni sawa na kuwa na mayai kumi halafu ukaamua kuyaweka kwenye mifuko kumi, maana yake ni kwamba utakuwa na mifuko kumi yenye mayai,” alisema Membe.
“Lakini unaweza kuwa na idadi hiyo hiyo ya mayai na ukaamua kuyagawanya; mayai matatu unayaweka kwenye mfuko mmoja, mawili kwenye mfuko mwingine na yaliyobaki kwenye mfuko mmoja. Maana yake ni kwamba utaendelea kuwa na mayai kumi lakini idadi ya mifuko imepungua.
Hapa sasa utakuwa hujapunguza gharama za kuyatunza hayo mayai.” Rais aliahidi kwenye kampeni na hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge kuwa atapunguza ukubwa wa Baraza la Mawaziri ili kubana matumizi.
Alitekeleza ahadi yake kwa kuunda baraza lenye mawaziri 34 tofauti na lililopita ambalo lilikuwa na mawaziri 55.
Upunguzaji huo wa baraza ulifanywa kwa kuunganisha wizara na hivyo kufanya makatibu wakuu, ambao ni maofisa masuhuli wa wizara kuwa zaidi ya mmoja kwenye baadhi ya wizara.
“Ameendeleza wizara zilezile, lakini akaamua kuzikusanya pamoja. Hiyo haimaanishi kuwa atakuwa amepunguza gharama za uendeshaji wake,” alisema Membe. “Hilo tutaliona kwenye Bajeti ya Serikali ya mwaka huu.
Tuone kama bajeti itaongezeka au itapungua? Kwa sababu kama wizara zimepungua kama tunavyoamini, lazima bajeti ipungue, sasa bajeti ikiongezeka au ikibaki vilevile maana yake hakuna kilichofanyika.
” Membe alitoa mfano wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambayo sasa inaitwa “Wizara ya Mambo ya Nje, Kikanda na Ushirikiano wa Afrika Mashariki”, akisema itapaswa kuwa na bajeti mbili; ya Mambo ya Nje na Bajeti ya Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki kinyume chake ni vigumu kuiendesha.
Membe alikiri kuwa hata yeye angeingia kwenye mtego wa kupunguza idadi ya wizara kama angefanikiwa kuchaguliwa kuwa Rais kama ilivyokuwa nchini Namibia ambako wizara zilipunguzwa kutoka 32 hadi 20.
Alisema siku ya kuapishwa Rais Magufuli, alikutana na Makamu wa Rais wa Namibia, Nickey Lyambo na baada ya kusalimiana na kumpongeza kwa hatua ya kupunguza wizara, kiongozi huyo wa Taifa hilo la kusini mwa Afrika alimweleza kuwa uamuzi huo umewasababishia matatizo makubwa bungeni “Aliniambia katika Bunge la Namibia kuna mjadala mkali wa kutaka wizara ziongezwe,” alisema Membe akimnukuu makamu huyo wa rais wa Namibia.
Membe alibainisha kuwa kwa Tanzania, mfumo huo mpya wa wizara pia unaweza kuathiri uwasilishaji wa bajeti bungeni kwa kuwa mawaziri sasa watahitaji muda mwingi zaidi kuliko ilivyokuwa awali ili kuzungumzia wizara kadhaa zilizounganishwa, jambo ambalo lililalamikiwa pia na kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, Tundu Lissu.
Alichofanya Rais Magufuli ni kubadili form na siyo content ya wizara, wizara ni zilezile na mzigo ni uleule,” alisema.
Safari za nje Mbunge huyo wa zamani wa Mtama mkoani Lindi, pia alikosoa udhibiti wa safari za nje, akisema Tanzania si kisiwa.
Alikuwa akijibu swali lililomtaka aeleze uhalisia wa mpango wa Rais Magufuli kubana matumizi kwa kufuta safari za nje za mawaziri na watumishi wengine wa umma.
Mara tu baada ya kuingia madarakani, Rais Magufuli alifuta safari zote za nje ya nchi kwa watendaji na watumishi wa umma, isipokuwa zile tu ambazo zingepata kibali cha Ikulu, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kubana matumizi ya Serikali.
Rais Magufuli alisema katika hotuba yake ya kuzindua Bunge kuwa kuanzia mwaka 2013 hadi 2015, safari hizo ziliigharimu Serikali Sh356.3 bilioni na kwamba kati ya fedha hizo, Sh183.1 bilioni zilitumika kwa ajili ya tiketi za ndege, Sh68.6 bilioni kwa ajili ya mafunzo na Sh104.5 bilioni kwa ajili ya posho.
MWANANCHI
Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Simon Group, Robert Kisena ameeleza kusikitishwa na taarifa zisizo za kweli zinazoihusisha familia ya Rais mstaafu, Jakaya Kikwete na umiliki wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) na kusisitiza kuwa yeye ndiye mmiliki halali.
Kisena alidai kwa muda mrefu watu wenye nia mbaya dhidi yake, wamekuwa wakihoji umiliki wa shirika hilo licha ya kuonyesha vielelezo vyote.
Alisema taarifa zilizosambaa hivi karibuni zinazodai kuwa anaimiliki Uda kwa ushirikiano na Khalfan ambaye ni mtoto wa Kikwete hazina ukweli.
Alidai kuwa Kampuni ya Simon Group ambayo ilisajiliwa Mwanza 2007, inamilikiwa na watu wanane wa familia ya Kisena isipokuwa Profesa Juma Kapuya ambaye ana asilimia tano ya hisa kwenye kampuni hiyo.
“Kampuni hii inamilikiwa na watu wanane, hata mkisoma hizi nyaraka mtaona majina ya watu hao ambao ni mimi, wanangu; Simon, Gloria, Kulwa na George; mdogo wangu William Kisena, mama yangu Modesta Pole na Profesa Kapuya.
“Hakuna jina la Khalfan Kikwete hapa, sijui hizo taarifa watu wanazitoa wapi,” alihoji Kisena huku akionyesha vielelezo.
Alisema hata wakati kampuni hiyo inaanzishwa, Khalfan alikuwa mtoto mdogo ambaye asingeweza kumiliki kampuni hiyo ambayo inakua kwa kasi.
Kisena alidai taarifa hizo za uongo zinaenezwa na watu ambao ni washindani wake kibiashara na wengine ni maadui wa kisiasa wa Kikwete.
Alisema yeye ni kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na amekuwa hivyo siku zote, lakini hajihusishi na siasa bali anafanya biashara.
“Kama kuna wanaoichafua familia ya Kikwete waache kuniunganisha na mimi, sifanyi siasa. Na kama kuna wanaonichafua kibiashara basi waache kuiingiza familia ya Kikwete, wapambane na mimi kwenye biashara,” alisema Kisena.
Hata hivyo, mwenyekiti huyo alisema kampuni yake ya Uda RT ndiyo itakayoendesha mradi wa mabasi yaendayo kasi na kuwa nauli zilizopendekezwa zilitokana na tathmini ya gharama halisi za uendeshaji wa mradi huo.
Alisema baadhi ya vitu vilivyowafanya wapendekeze nauli hizo kuanzia Sh700 mpaka Sh1,200 ni pamoja na kulipia barabara za Dart.
Pia, alisema mabasi hayo yatakuwa hayakai vituoni kwa hiyo huenda wakati mwingine yatakuwa yanatembea bila abiria.
“Sababu hizo ndiyo zimetufanya tupendekeze nauli hizo, lakini tuko kwenye mazungumzo na Serikali ili waondoe malipo ya barabara ili nauli ipungue.
Mazungumzo yanaenda vizuri, ninaamini nauli zitapungua,” alisema. Kisena alisema ifikapo Machi, mwaka huu, Kampuni ya Uda itaorodheshwa kwenye Soko la Hisa ili wananchi waweze kumiliki wenyewe kampuni hiyo. Alisema wanaendelea kufanya mipango kwa ajili ya kuuza asilimia 70 ya hisa kwa wananchi wote.
Unataka kutumiwa MSG za habari zote kubwa kutoka kwa Millard Ayo? ukiwa na line ya tiGO andika ‘AYO’ tuma kwenda 15510, msg utayotumiwa jibu OK ili uanze kupokea matukio yote kwa sms, pia ungana na Millard Ayo kwenye Twitter, FB, Instagram na YouTUBE wa kubonyezahapa>>>INSTAGRAM TWITTER FB YOUTUBE