Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Joseph Kabila Kabange leo tarehe 04 Oktoba, 2016 wamefanya mazungumzo rasmi Ikulu Jijini Dar es Salaam na kisha kuzungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari ambapo viongozi hao wawili wamekubaliana kuendeleza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kidugu na kihistoria katika nchi hizi mbili marafiki na majirani.
Katika Mazungumzo hayo Rais John Pombe Magufuli amemuhakikishia Rais Joseph Kabila Kabange kuwa Serikali ya Tanzania imechukua hatua kadhaa za kuimarisha huduma katika bandari ya Dar es Salaam na kupunguza vizuizi vya barabarani hadi kubaki vitatu ili nchi ya Kongo na nchi nyingine za kusini na magharibi mwa Tanzania ziitumie bandari hiyo bila vikwazo.
Dkt. Magufuli amesema Tanzania imejiwekea malengo ya kuhakikisha uchumi wake unakua kwa asilimia 7.2 na kwamba kutokana na hali hiyo anawakaribisha wafanyabiashara wa Kongo kuja kuwekeza nchini Tanzania na wafanyabiashara wa Tanzania kwenda kuwekeza nchini Kongo.
“Mhe. Rais Joseph Kabila Kabange takwimu zinaonesha nchi zetu zinafanya biashara kubwa kwani katika mwaka 2009 tulifanya biashara iliyofikia Shilingi Bilioni 23.1 na imekuwa ikikua mwaka hadi mwaka na hivi sasa tunafanya biashara yenye thamani ya shilingi Bilioni 393.6 kwa mwaka.
“Mimi ningependa kuona sisi ndugu na majirani tunafanya biashara zaidi, wafanyabiashara wa Kongo waje Tanzania kuwekeza na Serikali yangu itawaunga mkono” amesema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli amezungumzia mikakati ya kuimarisha mawasiliano ya barabara na ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) ambapo Tanzania imetenga Shilingi Trilioni 1 kwa ajili ya kuanza ujenzi huo na kwamba hatua hiyo itarahisisha zaidi usafirishaji wa mizigo ya kwenda na kutoka Kongo kupitia bandari ya Dar es Salaam.
Kuhusu mradi wa ujenzi wa Bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania, Rais Magufuli amesema ni matarajio kuwa Kongo ambayo pia imegundua mafuta katika ziwa Albert itatumia bomba hilo kama ambavyo Tanzania pia inatarajia kulitumia kufuatia tafiti kuonesha uwepo wa mafuta katika maeneo ya ziwa Eyasi na Ziwa Tanganyika.
ULIKOSA HII YA RAIS MAGUFULI KUSEMA BANDARI YETU ILIFIKA MAHALI MELI ZILIPOTEA NA MIZIGO YA WATU? UNAWEZA KUANGALIA VIDEO HII HAPA CHINI