Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemuagiza Waziri na Katibu Mkuu katika Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kusitisha mara moja utekelezaji wa zoezi la kuwaondoa wafanyabiashara wadogo maarufu kwa jina la Machinga katika Jiji la Mwanza pamoja na mikoa mingine mpaka hapo mamlaka husika zitakapokamilisha maandalizi ya maeneo watakapohamishiwa na kwa kuwashirikisha wamachinga wenyewe.
Rais Magufuli akiwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa agizo hilo leo tarehe 06 Desemba, 2016 Ikulu Jijini Dar es Salaam huku akionya kuwa kiongozi yeyote ambaye hayupo tayari kutekeleza agizo hilo aachie ngazi.
‘Sipendi Wamachinga wafanye biashara kwenye hifadhi ya barabara lakini hakuna sheria katika nchi hii inayosema mtu wa biashara ndogondogo au Mmachinga hatakiwi kukaa katikati ya mji, tukianza kwenda kwenye utaratibu wa namna hiyo maana yake tunaanza kutengeneza madaraja’-Rais Magufuli
Wakati huo huo, Rais Magufuli ameagiza Wizara ya Nishati na Madini kusitisha mara moja zoezi la kuwaondoa wachimbaji wadogo katika Kijiji cha Nyaligongo kilichopo katika Kata ya Mwakitolyo Mkoani Shinyanga na badala yake wachimbaji hao waachwe waendelee na shughuli zao, na leseni ya mwekezaji anayedai eneo hilo ni lake aondolewe.
‘Wale waliofukuzwa Shinyanga wabaki palepale, kama ni leseni ya huyo mwekezaji ifutwe, Makamu wa Rais fuatilia hili, mweleze Waziri wa Nishati na Madini, waache kufukuza wananchi hovyohovyo, wale wanapata riziki yao, wanasomesha watoto wao lakini wanafukuzwa tu’-Rais Magufuli
Hata hivyo Rais Magufuli amesema maagizo yake hayana maana kuwa Wamachinga na Wachimbaji wadogo waendeshe shughuli zao kwa kuvunja sheria bali wazingatie sheria na Mamlaka zisiwanyanyase watu wanyonge.
VIDEO; Agizo jingine la Rais Magufuli kwa waziri wa Elimu, Bonyeza play hapa chini kutazama