Ikiwa hadi hivi sasa soko la hisa la Dar es Salaam maarufu kama DSE lina kampuni 25 zilizoorodheshwa ambapo kampuni za ndani ni 18 na zile zilizoorodheshwa kutoka masoko ya kigeni yakiwemo London na Nairobi ni 7. Vodacom inatarajiwa kuwa miongoni mwa kampuni zitakazokuwa na mitaji mikubwa katika soko la DSE. Kampuni nyingine zenye mitaji mikubwa ni Acacia, EABL na TBL.
Kampuni ya simu za mkononi nchini Vodacom Tanzania itakuwa kampuni ya kwanza inayotoa huduma za mawasiliano kuuza hisa zake katika DSE. Hii inafuatia rasimu ya waraka wa matarajio (Prospectus) na maombi yaliyotumwa kwenye Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) kukubaliwa. CMSA ndiyo mamlaka inayosimamia masoko ya mitaji na dhamana nchini.
Uuzaji wa hisa za awali wa Vodacom Tanzania Limited PLC ni katika utekelezaji wa Sheria ya Posta na Mawasiliano iliyofanyiwa marekebisho na sheria ya Fedha mwaka 2016 ambayo inaagiza kampuni zote za simu za mikononi kuuza 25% ya hisa zao kwa umma.
Hisa za kampuni hiyo inayoongoza kwa kuwa na wateja wengi zaidi nchini, huenda sasa zikaanza kuuzwa muda wowote kuanzia wiki hii. Vodacom Tanzania inatarajia kuorodhesha asilimia 25 ya hisa zake katika soko la mitaji ambayo ni sawa ni hisa milioni 560 zitakazokuwa na thamani ya shilingi bilioni 476 huku kila hisa ikiuzwa kwa Tsh 850.
Taarifa rasmi za mauzo ya awali ya hisa hizo milioni 560 lini zitaanza kuuzwa, na wawekezaji gani watakidhi vigezo zitatangazwa hivi karibuni.
AUDIO: Tahadhari kuhusu matapeli wa fedha za M-Pesa, Bonyeza play hapa chini kusikiliza