Aliyekuwa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamadunu na michezo, Nape Nnauye leo amekabidhi ofisi kwa Waziri Mpya wa Wizara hiyo, Dk. Harrison Mwakyembe. Makabidhiano hayo yamefanyika katika ofisi za Wizara Dodoma.
Aliyekuwa Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Nape Moses Nnauye leo amekabidhi rasmi ofisi kwa Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe aliyeteuliwa hivi karibuni kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Katika makabidhiano hayo yaliyohudhuriwa na watendaji wakuu wa Wizara, Mhe. Mwakyembe ameahidi kuwa licha ya kukabidhiwa ofisi, anaamini kuwa Mhe. Nnauye bado ni mdau mkubwa wa sekta za Wizara na kuwa anategemea kuendelea kupata ushirikiano kutoka kwake.
Aidha Waziri Mwakyembe ameahidi kuendeleza yote mazuri yaliyo anzishwa na Nnauye katika kuimarisha ufanisi wa Wizara na kuhakikisha inakuwa ni moja ya Wizara za mifano nchini. Amesisitiza kuwa katika kipindi kifupi alichokaa Wizarani, Mhe. Nnauye alianzisha mabadiliko makubwa na watu wameanza kuifahamu vizuri Wizara.
Kwa upande wake Nnauye amemshukuru Rais John Pombe Magufuli kwa kumuamini na kumpa dhamana kubwa ya kusimamia Wizara kwa kipindi cha miezi 15 huku akiwa ndio kwanza amekuwa mbunge katika awamu yake ya kwanza. Aidha Nnauye ameahidi kuendela kushirikiana na Wizara kwa ukaribu kwani ni kweli yeye ni mdau mkubwa wa sekta za wizara hii.
“Heshima aliyonipa Rais ni kubwa mno na nitaendelea kumuunga mkono katika dhamira yake njema ya kuleta mageuzi nchini,” Nnauye. Aidha alisisitiza kuwa, tofauti na maneno ya mitandaoni, yeye atabaki kuwa mtiifu kwa Rais, Serikali na chama chake.
VIDEO: Nay wa Mitego ajibu kuhusu kudaiwa kutumika kisiasa, Bonyeza play hapa chini kuitazama