Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 01 Aprili, 2017 amewaapisha wajumbe wa Kamati Maalum ya kuchunguza kiwango na aina ya madini yaliyomo kwenye mchanga wenye madini uliomo ndani ya makontena yaliyopo katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Kamati hiyo ya Wanasayansi 8 walioteuliwa na Rais Magufuli tarehe 29 Machi, 2017 inaongozwa na Mwenyekiti wake Prof. Abdulkarim Hamis Mruma ambayo itafanya kazi ya uchunguzi kwa siku 20 kisha kuwasilisha ripoti yake kwa Rais.
Akizungumza baada ya kuwaapisha, Rais Magufuli amesema ameamua kuunda Kamati hiyo yenye wasomi waliobobea katika masuala ya Jiolojia, Kemikali na Uchambuzi wa kisayansi ili wawawakilishe Watanzania zaidi ya Milioni 50 ambao wanataka kujua ukweli kuhusu rasilimali yao ya madini.
“Tunataka tujue kama tunaibiwa, tumeibiwa kiasi gani na kama hatuibiwi, haujaibiwa kiasi gani. Nendeni popote mnapohitaji kufanya kazi tutawapa ushirikiano, fungueni makontena popote yalipo, chukueni sampuli na mkazipime mjue kilichomo na naviagiza vyombo vya dola vihakikishe hakuna mtu atakayewakwamisha.” – Rais Magufuli.
Aidha, Dkt. Magufuli amesema baada ya kuunda Kamati hii ya wanasayansi, ataunda Kamati nyingine ya wachumi na wanasheria kwa ajili ya kufanya tathmini na kuiangalia sera na sheria ya madini kwa lengo la kupata taarifa zaidi juu ya biashara ya madini hapa nchini.
Bonyeza play hapa chini kuitazama.
VIDEO: Waziri Mkuu wa Ethiopia na Rais Magufuli Ikulu DSM, Bonyeza play hapa chini kuitazama