Katika kuhakikisha hadhi ya mtoto wa kike na thamani yake inapanda katika jamii hasa kwenye elimu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mwigulu Nchemba ameanzisha Ujenzi wa Hostel 22 za wanafunzi wa kike katika Shule 22 za Sekondari zilizopo katika Kata 20 ndani ya Jimbo la Iramba.
Lengo la Mradi huu ni kukuza kiwango cha elimu Jimboni hasa kwa watoto wa kike ambao wanakutana na vikwazo vingi na unafanywa kwa ushirika wa Ofisi ya Mbunge na Wananchi wa Jimbo hilo na utakapokamilika utasaidia zaidi ya 70% ya wanafunzi wa kike kwenye jimbo hilo.
Hadi wakati huu Waziri Nchemba amechangia mifuko 100 kwa kila Kata pamoja na nondo kwa ajili ya ujenzi na Wananchi wakitoa matofali na Mafundi wa kujenga Hostel ambapo ujenzi umeshaanza katika Kata zote ukifikia sehemu nzuri.
“Nimekagua Mradi katika Shule ya Kizaga iliyopo Kata ya Ulemo. Nimefurahishwa na Wananchi walivyojitoa. Nitaleta mifuko 100 ya cement kukamilisha Hostel hii. Kupaua tumepata Mfadhili atamaliza kila kitu mpaka kukamilika kwake na kuanza kutumika. Ikikamilika itachukuwa Wanafunzi wa kike zaidi ya 160 wakati Shule ina Wanafunzi wa kike 180.” – Mwigulu Nchemba.