Raia wa Afrika Kusini, ambaye ni Mechanical Engineer, Menelaos Tsampos leo amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa kosa la kumtishia mtu kwa njia ya mtandao kupitia mfumo wa Computer.
Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga amemsomea Tsampos mashtaka yake mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha ambapo alidai mshtakiwa anakabiliwa na makosa manne.
Katuga amedai June 22, 2017 maeneo ya Dar es Salaam kupitia mfumo wa computer alituma ujumbe wa E-mail uliokuwa na maneno ya vitisho kwa mtu anayeitwa Costa Gianna, ikiwa ni kinyume na sheria ya mtandao kifungu cha 23(1) na (2) namba 14 ya mwaka 2014.
Pia anadaiwa July 20, 2017 amemtishia tena mtu huyo kupitia email yake, ambapo alimwambia anampa saa 48 ili watatue mgogoro baina yao kinyume na hapo atamfanyia kitu kibaya.
Katuga amedai kosa jingine ni kuishi nchi bila kibali na kukutwa na hati ya kughushi ya kusafiria ambapo aliyatenda kati ya July 6, 2017 na August 7, 2017 Dar es Salaam.
Baada ya kusomewa makosa hayo, mshtakiwa alikana ambapo Katuga aliiomba Mahakama imnyime dhamana mshtakiwa kutokana na uhalisia wa makosa aliyoyafanya ambapo hata hivyo, Wakili wa utetezi Jebrah Kambole amedai makosa hayo yanadhaminika, hivyo anaomba dhamana.
Kutona na hatua hiyo, Hakimu Mkeha ameahirisha kesi hiyo hadi August 16, 2017, huku akiamuru mshtakiwa huyo akaguliwe Visa na makazi yake ili apewe dhamana.