Mpelelezi kinara aliyefanikisha kukamatwa kwa Yang Feng Glan maarufu kama ‘Malkia wa Meno ya Tembo’ Wayne Lotter ameuawa kwa risasi na watu wasiojulikana.
Taarifa iliyochapishwa na mtandao wa The Guardian imesema kuwa Wayne Lotter, 51, alipigwa risasi Jumatano jioni katika maeneo ya Masaki, Dar es Salaam wakati akitokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ambapo taxi alilopanda lilisimamishwa na gari lingine kabla ya watu wawili kutelemka na kumpiga risasi.
Lotter alikuwa Mkurugenzi na mwanzilishi-mwenza wa PAMS Foundation, Shirika lisilo la Kiserikali ambalo linajihusisha na masuala ya kupinga Ujangili ambalo lilianza shughuli zake Tanzania mwaka 2009 na mara kadhaa amekuwa akipokea vitisho vya kifo.