Katibu wa CHADEMA Wilaya ya Moshi Vijijini, Emmanuel Mlaki amepinga kusimamishwa uongozi na Katibu wa Chama hicho Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema kwa madai uamuzi huo ni wake binafsi na haujatokana na maamuzi ya vikao halali vya Chama.
Akiwa Dar es Salaam, Mlaki amesema taarifa ya Lema haina uhalali wala ukweli kwa kuwa hakuna kikao chochote cha Chama kilichowahi kukaa na kujadili na kumuelekeza kufanya hivyo.
>>>”Binafsi ni Mjumbe wa Baraza la Mashauriano la Mkoa, hatujawahi kukaa kikao kujadili ama kumuelekeza afanye alichokifanya. Pia Baraza la Uongozi la Mkoa ambalo moja ya wajumbe wake kwa mujibu wa Katiba ya Chama ni Ibara ya 7.5.3 ni Freeman Mbowe ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu katika Mkoa. Aidha Joseph Selasini ni Mwenyekiti wa Wabunge wa CHADEMA Mkoa wa Kilimanjaro.”
Mlaki amesema, kwa mujibu wa kanuni za Chama hicho, kanuni ya 6.5.6 inasema kiongozi hawezi kuchukuliwa hatua za kusimamishwa uongozi pasipo kujulishwa makosa yake, kupewa nafasi ya kujibu makosa ndani ya kipindi cha wiki mbili, kupewa nafasi ya kujitetea mbele ya kikao pamoja na kupewa taarifa ya maamuzi ya kikao.
>>>”Je, Katibu wa Mkoa kaueleza Umma na wanaCHADEMA aliyafanya haya?”
Aidha, amebainisha kuwa wiki kadhaa zilizopita Viongozi CHADEMA walilalamika kuhusu usaliti wa baadhi ya Madiwani ambao ulipelekea Chama kupoteza nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi na Kamati ya Uchumi na Mazingira.
Kutokana na kusimamishwa, Mlaki amemtaka Lema afute taarifa yake ndani ya siku saba kwa sababu haina ukweli na uhalali wa Chama.
BREAKING: Waziri Mwijage apiga marufuku watendaji kufunga viwanda
Agizo la Naibu Waziri Jafo kwa Maofisa Kilimo na Wakuu wa Mikoa