Leo October 11, 2017 Mbunge wa Kawe kupitia tiketi ya CHADEMA, Halima Mdee amekana mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kumtolea lugha ya matusi Rais John Magufuli.
Mdee alikana kosa hilo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa baada ya kusomewa maelezo ya awali na Wakili wa Serikali, Janeth Magoho ambapo katika maelezo hayo, Magoho alidai kuwa Mdee ni Mbunge wa Kawe (CHADEMA), anaishi Makongo, kabila lake ni Mpare na ana miaka 39.
Wakili huyo ameeleza kuwa July 3, 2017 Mdee akiwa Makao Makuu ya CHADEMA, maeneo ya Ufipa alitoa lugha ya matusi dhidi ya Rais Magufuli ambapo inadaiwa alitukana kuwa “Rais anaongea ovyo ovyo, inabidi afungwe break”.
Baada ya kutoa lugha hiyo, July 4, 2017 alikamatwa na Polisi maeneo ya Kibangu, kisha kupelekwa kwa ZCO ambapo alihojiwa na kukiri kutoa maneno hayo.
Baada ya kusomewa maelezo hayo, Mdee alikubali wasifu wake ambao ni Jina, umri, nafasi ya uongozi, mahali anapokaa, kukamatwa na kufikishwa Mahakamani, lakini alikana kumtolea lugha ya matusi Rais Magufuli, pamoja kukiri maneno hayo wakati akihojiwa katika Ofisi za ZCO.
Baada ya kuelezwa hayo, Hakimu Nongwa ameahirisha kesi hiyo hadi November 8, 2017 ambapo ameutaka upande wa mashtaka ufike na mashahidi.
Awali kabla ya kusomewa maelezo hayo, Wakili Magoho alimkumbusha mshtakiwa makosa yake.
Alidai kuwa Mdee anakabiliwa na kosa la kutumia lugha ya matusi, ambapo July 3, 2017 akiwa Makao Makuu ya CHADEMA, mtaa wa Ufipa alitoa lugha hiyo dhidi ya Rais Magufuli akidaiwa kusema; “Rais Magufuli anaongea hovyo hovyo inabidi afungwe break”.
ULIPITWA? DC Ally Hapi alivyoagiza kukamatwa kwa Mbunge Halima Mdee