Vigogo wawili wa Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA) wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kosa la kuisababishia serikali hasara ya Tsh. Bilioni 1,097,681,107.
Vigogo hao ni aliyekuwa Kaimu Mtendaji Mkuu, Shaha Hanzuruni na Mkuu wa Kitengo cha Fedha, Onesphor Luhungu ambapo wamesomewa makosa yao na Mwendesha Mashitaka wa TAKUKURU, Leonard Swai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
Inadaiwa kuwa washtakiwa wote wanakabiliwa na kosa la matumizi mabaya ya madaraka ambapo January 1, 2012 na December 30, 2014 katika Ofisi za TIA zilizopo Temeke DSM, wakiwa wafanyakazi wa Chuo hicho mmoja akiwa Kaimu Mtendaji Mkuu na mwingine Mkuu wa Kitengo cha Fedha hawakufuata taratibu za manunuzi ya kununua ardhi kampasi ya Mwanza na kusababisha Vedastus Lukago kupata faida ya Tsh Bilion 1,097,681,107.
Kosa jingine inadaiwa wameisababishia Mamlaka hasara kati ya January 1, 2012 na December 30, 2014 kwa nafasi zao na matendo yao walisababisha hasara ya Tsh Bilion 1,097,681,107 fedha za TIA.
Inadaiwa wamesababisha hasara kwa kutokufanya taratibu za manunuzi wakati wa kusaini mkataba wa kununua eneo la kampasi Mwanza.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa wote walikana mashtaka hayo.
Wakili Swai alidai kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika na kuomba tarehe nyingine ya usikilizwaji wa maelezo ya awali na kwamba masharti ya dhamna yako wazi.
Wakili wa utetezi Jamuhuri Jonson aliiomba mahakama iwape wateja wake dhamana.
Hakimu Simba alitoa masharti ya dhamana ambapo kila mshtakiwa anatakiwa kuwa na wadhamini wawili na kila mmoja atasaini bondi ya Tsh Milion 250 ambazo zinatakiwa kupelekwa Mahakamani hapo huku akisema washtakiwa wawasilishe hati zao za kusafiria Mahakamani hapo na kila mshtakiwa asitoke nje ya Mkoa wa Dar es Salaam bila kibali cha Mahakama.
Washtakiwa wote wamerudishwa rumande kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana na kesi hiyo imeahirishwa hadi October 24, 2017.
KILIMANJARO: Polisi wamuua jambazi sugu, kakutwa na simu 19 na line 58