Upelelezi wa kesi ya utakatishaji fedha wa Dola za Kimarekani Milioni 6 inayomkabili aliyekuwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Harry Kitilya na wenzake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu bado haujakamilika ikiwa ni mwaka mmoja na nusu sasa.
Mbali ya Kitilya, Washtakiwa wengine ni aliyekuwa Miss Tanzania mwaka 1996 ambae pia ni Ofisa wa Stanbic Bank, Shose Sinare na Sioi Graham Solomon ambao walifikishwa Mahakamani hapo kwa mara ya kwanza April 1,2016 kwa kukabiliwa na mashtaka ya kula njama, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha.
Wakili Mwandamizi wa Serikali Mutalemwa Kishenyi amemueleza Hakimu Mkazi, Godfrey Mwambapa kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kwamba wanasubiri awamu ya pili ya upelelezi kutoka Uingereza hivyo akaomba kesi hiyo iahirishwe hadi tarehe nyingine.
Baada ya kuelezwa hayo, Mwambapa ameahirisha kesi hiyo hadi November 10,2017 ambapo kwenye kesi hii, Washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya March 2013 na September 2015 wakati wa mchakato wa mkopo wa dola za Marekani 550 milioni kwa serikali ya Tanzania kutoka Benki ya Standard Uingereza.
Pia wanadaiwa kuwa March 2013 Dar es Salaam walijipatia Dola za Marekani Milioni 6 wakionyesha kuwa fedha hizo zilikuwa ni malipo ya ada ya uwezeshaji upatikanaji wa mkopo na zililipwa kupitia Kampuni ya Egma T Ltd.
ULIPITWA? Baada ya Adam Malima kuachiwa huru, Kaka na Dereva waongea
.