Kocha msaidizi wa zamani wa klabu ya Manchester United na kocha wa sasa wa Fulham Rene Meulensteen amefunguka kwamba alimwambia Sir Alex Ferguson asiwe anaenda kuangalia mechi za Manchester United katika dimba la Old Trafford msimu huu.
Kocha huyo mstaafu wa United amekuwa akihudhuria kila mechi ya United tangu David Moyes alipochukua madaraka, hata mara nyingine akisafiri kwenda kuangalia mechi za ugenini.
Lakini Meulensteen, ambaye alifanya kazi chini ya Ferguson, anaamini mscotish huyo angekaa mbali na klabu hiyo kwa japo miezi 12.
Rene ameliambia gazeti la The Sun on Sunday: ‘Nakumbuka nilisema baada ya kustaafu, itabidi ukae mbali na klabu japo kwa mwaka na kuangalia namna mambo yanavyoenda……, lakini ameshindwa kufanya hivyo.”
Huku United ikiwa imetolewa kwenye michuano ya FA na Capital One na bado wakiwa nafasi ya saba kwenye Premier League, baadhi ya watu wamekuwa wakisema kwamba uwepo wa Ferguson katika mechi umezidi kumuongezea presha Moyes.
Lakini Meulensteen anaelewa kwanini Ferguson ameshindwa kukaa mbali na klabu aliyoifundisha kwa miaka 26.
Alisema: ‘Sio jambo la kushangaza kwa sababu kama ni kitu ulichokuwa unakifanya kwa muda mrefu kwenye maisha yako, inakuwa vigumu kusema kukiacha.”