Naibu Spika Dr Tulia Ackson alikuwa mkoani Mbeya December 23, 2017 na kukutana na vijana kwa ajili ya kutoa elimu ya kujitambua ambapo hakuacha kuwakosoa baadhi ya vijana ambao hulalamika mara kwa mara kwamba hawana ajira wakati huo wanaishia kulala nyumbani wakizisubiri ajira hizo.
“Mimi nayasikia mambo mengi kwenye nafasi yangu, anakuja mtu anakuja na kuniambia Mheshimiwa nina mototo wangu kamaliza shule sasa yupo nyumbani hana kazi. Unajua pamoja na mambo mengine yote hii habari ya mtu kuwa tu nyumbani huwa siielewi, mimi kama muajiri inanipa tabu sana kuajiri mtu wa kulala na kuamka ” –Dr Tulia
“Mimi naamini sana katika mtu anayejishughulisha, huwezi wewe kama kijana na nguvu zako pamoja na akili unalala kwa wazazi wako hata hufikiri kuhusu maisha yako unasubiri siku upigiwe simu uambiwe kuna kazi sehemu, wewe mwenyewe umeanza kwa kufanya nini?” –Dr Tulia