Leo December 30, 2017 Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Dr. Mary Mwanjelwa amefanya ziara ya kikazi katika mkoa wa Morogoro na kuwaagiza wafanyabiashara wa mbolea kote nchini walioweka mgomo wa kupeleka mbolea kwa wakulima kufikia December 30, 2017 wawe wamefungua maghala.
Amesema endapo wafanyabiashara hao wasipofanya hivyo serikali itawanyang’anya leseni zao haraka iwezekanavyo ili kuruhusu wafanyabiashara wenye uwezo wa kufanya jukumu hilo pasina kuwaumiza wakulima kutokana na bei ghali ya mbolea.
Dr. Mwanjelwa ametoa agizo hilo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari alipotembelea Wakala wa mbegu za kilimo (Agricultural Seeds Agency-ASA) mara baada ya kubaini kuwa kuna wafanyabiashara wameanza kufunga maghala kwa madai ya kupanda kwa mbolea katika soko la Dunia.
Amesema kuwa kufanya hivyo ni kinyume na sheria na kuijaribu serikali kwani malalamiko yao ya kupanda kwa bei katika soko la Dunia hayana tija kwani mbolea zote zilipo nchini tayari wakishanunua kipindi soko likiwa kwenye unafuu mkubwa.
Amesema kuwa wafanyabiashara hao kwa makusudi wameamua kufifisha juhudi za Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na President Dr. John Pombe Magufuli ya kuwakomboa wakulima kupitia gharama nafuu ya mbolea hivyo kufikia kesho wasipofungua maghala hayo watanyang’anywa leseni zao ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa sheria.
“TUNATAFUTA WATAFITI WENYE UZOEFU” – NAIBU WAZIRI MWANJELWA