Leo January 6, 2018 President Magufuli amefika katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ambapo amewajulia hali baadhi ya wagonjwa waliolazwa akiwemo Mzee Kingunge Ngombale Mwiru na Mapacha walioungana Maria na Consolata Mwakikuti.
Katika wodi ya Mwaisela, Rais Magufuli amemjulia hali Mzee Kingunge Ngombale Mwiru ambaye anatibiwa majeraha baada ya kushambuliwa na mbwa, nyumbani kwake Jijini Dar es Salaam.
Mzee Kingunge amemshukuru President JPM kwa kwenda kumuona na amemueleza kuwa sasa anajisikia nafuu baada ya kupata matibabu.
Rais Magufuli amemuombea Mzee Kingunge apone haraka na amesema anatambua mchango mkubwa alioufanya katika siasa na maendeleo ya nchi.
President Magufuli leo pia amewajulia hali mapacha walioungana Maria na Consolata Mwakikuti ambao wamelazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kwa matibabu ya moyo na Richard Kajumulo ambaye ni Kaka wa Mbunge wa Muleba Kusini Prof. Anna Tibaijuka.
Rais Magufuli amewashukuru na kuwapongeza madaktari wa hospitali ya Taifa Muhimbili na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kwa kazi kubwa wanayofanya kutibu wagonjwa na amesema Serikali itaendelea kutatua changamoto zinazowakabili ili kuboresha huduma zaidi.
“Nawashukuru sana madaktari na wafanyakazi wote, mnafanya kazi kubwa ya kuwatibu wagonjwa, pia mmeboresha hospitali na inaonekana ni safi, mimi niwaahidi kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira yenu ya kazi ili muendelee kutoa huduma nzuri” -Rais Magufuli.
Baada ya maneno hayo ya JPM, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Prof. Mohamed Janabi amesema matibabu kwa Maria na Consolata ambao ni wanafunzi mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Kanisa Katoliki Ruaha yanakwenda vizuri.
Prof. Janabi amesema taasisi hiyo imefanikiwa kutoa matibabu kwa wagonjwa wa moyo 14,000 katika mwaka uliopita na kwamba inashika nafasi ya tatu barani Afrika kwa utoaji wa huduma bora za matibabu ya moyo.
KINGUNGE AMWAMBIA JPM “CCM NI CHAMA CHANGU KILE”