Wafanyabiashara wawili Naushad Mohammed Suleiman (63) na Ali Makame Juma (36) wakazi wa Zanzibar, wamekiri katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kusafirisha madini ya dhahabu vipande saba vyenye thamani ya Sh milioni 989.7 bila kuwa na leseni.
Awali, upande wa mashtaka ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali, Jehovaness Zacharia umedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), ametoa kibali cha kuipa mamlaka mahakama hiyo kusikiliza shauri hilo.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Mashauri ameutaka upande wa mashtaka kuwasomea makosa upya.
Wakili Zacharia amedai kuwa washtakiwa wanakabiliwa na makosa mawili, ambapo inadaiwa kati ya November Mosi na 29, 2017 katika siku isiyofahamika kati ya Dar es Salaam na Mkoa wa Geita, walikula njama kufanya kosa la kusafirisha madini nje ya nchi isivyohalali.
Pia wanadaiwa November 29, 2017 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Aman Karume, walikutwa wakisafirisha madini kwenda Dubai katika Falme za Kiarabu ambavyo ni vipande saba vya dhahabu vyenye uzito wa kilogramu 18.354 vyenye thamani ya Sh. milioni 989.7 bila kuwa na leseni.
Washtakiwa wamekiri makosa hayo na upande wa mashtaka umedai kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika. Hata hivyo, Hakimu Mashauri aliwatia hatiani washtakiwa kwa kukiri makosa waliyoshtakiwa nayo.
Wakili Zacharia amedai kuwa wanaomba kuahirisha kesi hiyo hadi kesho January 11, 2018 ili kuwasomea washtakiwa maelezo ya mashtaka yao (Ph), ambapo Hakimu Mashauri alikubaliana na ombi hilo.
Mahakama yakwama kutoa hukumu ya ‘Scorpion’
Fahamu hii inapotokea mtu asiye na akili timamu kabaka, Inakuwaje Mahakamani