Leo January 11, 2018 nakusogezea stori kutokea Botswana ambapo kanisa la muhubiri Bushiri raia wa Malawi limelifungiwa na serikali ya nchi hiyo, Muhubiri huyo ambaye anadaiwa ‘kutembea angani’.
Serikali ya Botswana imethibitisha kufungwa kwa kanisa la Bushiri la Christian Gathering Church ECG mjini Gaborone mara kadhaa kutokana na wasiwasi kuhusu ‘fedha za miujiza’.
Katika mtandao maarufu nchini Malawi wa Malawi24 wametoa ripoti kuwa kanisa hilo lilipinga uamuzi wa kufungiwa Mahakamani mwaka mmoja baada ya muhubiri huyo kupigwa marufuku kuingia nchini humo.
Hatahivyo Waziri wa Botswana Edwin Batshu alitangaza mwezi Aprili 2017 kwamba Bushir atahitaji kuwa na Visa ili aweze kuingia nchini humo, licha ya raia wa Malawi kutohitaji kibali hicho na kwa sasa anaishi Afrika Kusini.
Serikali ya Botswana imetangaza kuwa kanisa hilo litafungwa kabisa, huku gazeti hilo la Botswana limepokea barua inayoeleza kuwa kibali cha kanisa hilo kimefutwa kutokana na kutumia ‘fedha za miujiza’ ambapo ni kuvunja sheria za Taifa hilo
Bushiri ambaye ana zaidi ya ”likes” milioni 2.3 katika mtandao wa facebook na ambaye alivutia umati mkubwa wa kuweza kujaza uwanja wa FNB mkesha wa mwaka mpya bado hajatoa tamko lolote.
Kanisa hilo ni maarufu kwa mtindo wake wa maisha ya kifahari kutokana na ufanisi wake ambao umevutia wafuasi wengi barani Afrika.
Alishatuhumiwa mwaka uliopita baada ya kubainika alikuwa akiwatoza kati ya dola 80 hadi 2000 waumini wake waliotaka kula naye chakula cha jioni.