Upande wa Mashtaka umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa jalada la kesi ya Mhasibu Mkuu wa (TAKUKURU), Godfrey Gugai anayedaiwa kumiliki mali za Tsh. Bilioni 3 zisizoendana na kipato chake lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Hayo yameelezwa na Wakili wa serikali, Wankyo Simon mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
Wankyo amedai shauri hilo limeitishwa kwa ajili ya kutajwa lakini jalada la kesi limepelekwa kwa DPP kwa ajili ya kukaguliwa, kisha litarejeshwa TAKUKURU ili waangalie maelekezo waliyopewa na DPP.
Baada ya kueleza hayo, Wakili wa utetezi, Alex Mshumbusi amedai kuwa hategemei upelelezi wa kesi hiyo utachukua muda mrefu kwa sababu mshtakiwa wa kwanza alikuwa mtumishi wa TAKUKURU na tayari alishashtakiwa kinidhamu.
Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi January 31, 2018.
Mbali na Gugai, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni George Makaranga, Leonard Aloys na Yasini Katera.
Washtakiwa hao wanaokabiliwa na mashtaka 43 yakiwemo 20 ya utakatishaji fedha, kumiliki mali zisizoendana na kipato na kughushi mikataba ya mauziano ya viwanja katika maeneo mbalimbali.
Shtaka la kumiliki mali zilizozidi kipato linamkabili Gugai, ambaye anadaiwa kati ya January 2005 na December 2015, jijini Dar es Salaam, akiwa Afisa wa umma ameajiriwa na TAKUKURU alikutwa akimiliki mali zenye thamani ya Sh.Bilioni 3.6 ambazo haziendani na kipato chake cha sasa wala cha nyuma.
MWANZO MWISHO: KINGUNGE ASIMULIA ALIVYONG’ATWA NA MBWA WAKE