Siku moja baada ya rekodi ya kutofungwa katika uwanja wa nyumbani wa Nou Camp katika mechi 25 kuvunjwa, mwanasoka bora wa dunia wa zamani kwa mara ya nne mfululizo Lionel Messi amekielezea kwamba kipigo cha Barcelona cha mabao 3-2 kutoka kwa Valencia kwamba ilikuwa ni siku mbaya kwa klabu yake.
Barcelona wamekuwa wakishika nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa ligi tangu kuanza kwa msimu huu, lakini kipigo chao cha jana kutoka kwa Valencia kumewapa nafasi Atletico Madrid na Real Madrid kuweza kukaa kileleni kama watashinda mechi za leo.
Mshambuliaji huyo wa Argentina amechukizwa sana na kipigo cha jana lakini hata hivyo amefurahia kwa kuweza kurudi kwake dimbani baada ya kukaa nje kwa wiki sita baada ya kupata maumivu ya misuli.
“Ilikuwa siku mbaya,” Messi alikiri katika mkutano wake na waandishi wa habari leo, akizungumzia kipigo chao cha kwanza nyumbani baada ya muda mrefu.
“Nina furaha kwa sababu nimeweza kucheza mfululizo michezo kadhaa. Kiakili, nipo vizuri sana. Ni kweli kuna vitu havikuenda sawa kwa upande wa kimwili lakini sasa yamepita naangalia mbele.”