Onesmo Machibya maarufu ‘Nabii Tito’, mkazi wa mtaa wa Ng’ong’ona Manispaa ya Dodoma mwenye umri wa miaka 45, January 29, 2018 amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya wilaya ya Dodoma kwa kosa la kujaribu kujiua.
Akisoma shtaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo James Karayemaha, wakili wa serikali Salome Magesa amesema mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo January 25 2018 huu katika kijiji cha ng’ong’ona.
Amesema ‘Nabii Tito’ alitaka kujiua kwa kutumia wembe ambapo alijijeruhi kwenye baadhi ya maeneo ya mwili wake wakati akikamatwa na polisi na kwamba ametenda kosa hilo kinyume na kifungu namba 217 na kanuni zake.
Hata hivyo mshtakiwa huyo alipoulizwa na Hakimu amesema alichukua uamuzi huo baada ya kusikia sauti ikisema ajikate na wembe nakudai alitekeleza alichokisikia .
Baada ya kupata maelezo hayo Hakimu huyo amesema kutokana na alichokisikia kutoka kwa Nabii Tito anachukulia kuwa amesema si kweli kuwa ametenda kosa hilo na kuhoji upande wa mashtaka kuhusu upelelezi wa kesi hiyo kama umekamilika.
Hata hivyo kwa mujibu wa kifungu cha sheria 148(5) (b) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai sura ya 20 amesema amewasilisha mahakamani kiapo cha kupinga dhamana kwa mshtakiwa chenye sababu saba ambazo hakuziainisha ndani ya Mahakama hiyo.
Kutokana na pingamizi hilo Hakimu Karayemaha amesema mshtakiwa huyo ataendelea kuwa rumande hadi hapo Mahakama itakapoamua kuhusu dhamana yake.
ILICHOKIBAINI BODI YA MIKOPO BAADA KUFANYA UKAGUZI SHULE YA GREEN ACRES