Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Kenya Uhuru Muigai Kenyatta wamewaagiza Mawaziri wa Tanzania na Kenya kutatua tofauti ndogondogo zinazojitokeza katika biashara kati ya nchi hizi mbili.
Marais hao wametoa maagizo hayo leo asubuhi Februari 23, 2018 walipokutana na kufanya mazungumzo katika hoteli ya Munyonyo mjini Kampala muda mfupi kabla ya kuanza kwa vikao vya mkutano wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Rais Magufuli na Rais Kenyatta wamesema wanataka kuona biashara kati ya Tanzania na Kenya inazidi kukua na bidhaa zinauzwa na kununuliwa baina ya nchi hizo bila vikwazo vyovyote na hivyo kuagiza tofauti zilizojitokeza katika baadhi ya bidhaa zimalizwe.
“Kuna mambo madogomadogo yanakuwa yanajitokeza katika biashara kati ya Kenya na Tanzania, tunataka kwa haya yote Mawaziri wa Kenya na Mawaziri wa Tanzania mkae myatatue,” -Rais Magufuli
“Sisi hatuna tatizo, mambo mengine madogomadogo mno, mambo ya viatu, nguo, ngano, gesi ni madogo sana, mnatakiwa myatatue nyinyi yasifike kwetu, sisi huku tuko sawasawa” –Rais Magufuli na kuungwa mkono na Rais Kenyatta.
Wametoa maagizo hayo kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Katiba na Sheria wa Tanzania Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Balozi Monica Juma na Waziri wa Afrika Mashariki na Maendeleo ya Ushoroba wa Kaskazini wa Kenya Peter Munya.
JPM AMEHUTUBIA MKUTANO WA 19 WA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI