Poland imepitisha sheria ya kupiga marufuku kuuzwa bidhaa madukani siku za Jumapili. Shirika la habari la Associated Press limesema kuwa sheria hiyo mpya itawahusu pia wafanyabiashara ndogondogo na hii ni mara ya kwanza kupitishwa kwa sheria kama hiyo tangu uliposambaratika ukomunisti.
Baadhi ya wananchi wa Poland wameilalamikia sheria hiyo wakisema inawabana wanunuzi na inakwenda kinyume na msingi mkuu na wa asili wa mfumo wa soko huru ambao unahimiza kuhudumiwa wateja muda wote.
Hata hivyo watu wengi wameipongeza hatua hiyo hasa wafanya kazi za vibarua ambao muda wote wamekuwa wakilalamika kuwa hawana mapumziko katika kipindi kizima cha mwaka. Waungaji mkono wa sheria hiyo wanasema kuwa, sasa vibarua nao wataweza kupumzika siku za Jumapili.
Sheria hiyo imeungwa mkono pia na Kanisa Katoliki ambalo lina ushawishi mkubwa nchini Poland kiasi kwamba asilimia 90 ya wananchi wa nchi hiyo ni wafuasi wa kanisa hilo.
“HATA WAKIANDAMANA NDANI YA NYUMBA, MTU AKAUMIA, ALIYEITISHA ATAWAJIBIKA” WAZIRI MWIGULU