Leo March 14, 2018 stori ninayokusogezea ni kuhusu Watu sita wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi wa kusafirisha magunia 400 ya Mkaa yenye thamani ya Shilingi Milioni 30.
Washtakiwa hao ambao ni wakazi wa Zanzibar ni Buruhan Haji(25), Juma Mche (24), Ally Salum (22), Salum Zubery (25), Bahari Kombo (22) na Omary Ahmed (23).
Wakisomewa mashtaka yao na Wakili wa serikali, Mossie Kaima mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba amedai kuwa washtakiwa wanakabiliwa na makosa mawili.
Kosa la kwanza ni kusafirisha isivyo halali mazao ya misitu ambapo inadaiwa March 2,2018 kati ya Ufukwe wa Dar es Salaam na Unguja katika bahari ya Hindi walikutwa wakisafirisha mazao ya misitu.
Inadaiwa mazao hayo ya misitu ni magunia 400 ya Mkaa yenye thamani ya Shilingi Milioni 30 yakiwa ni Mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kosa la pili ni la kukutwa na mazao ya Misitu, inadaiwa walilitenda March 2,2018 ambapo walikutwa na magunia hayo 400 ya Mkaa bila leseni kutoka kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Misitu Tanzania.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Simba amesema washtakiwa hawaruhusiwi kujibu lolote kwa kuwa kesi hiyo ni ya uhujumu uchumi.
Wakili Mossie amedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, ambapo Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo March 19,2018.