Leo March 15, 2018 ndani ya Jiji la Dar es salaam Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, mhandisi Hamad Masauni amezindua vituo Sita (6) vya Polisi vinavyohamishika kutoka eneo moja mpaka jingine vyenye lengo la kusaidia kukabiliana na wimbi la matukio ya uhalifu.
Masauni amesema vituo hivyo pia vitasaidia kusogeza huduma za kipolisi karibu zaidi na wananchi zitakazopatikana kwa wakati.
Polisi imeanza mpango huo katika mkoa wa kipolisi wa Kinondoni ambapo Masauni amesema Kinondoni ndiyo inayoongoza kwa matukio ya kihalifu kwenye makosa mbalimbali ikiwemo ya usalama barabarani.