Mkurugenzi mkuu na mmliki wa mtandao wa kijamii wa Facebook Mark Zuckerberg amevunja ukimya kuhusu kashfa iliyoikumba kampuni yake ambapo ameomba radhi kutokana na “kuvunja uaminifu” na weteja wake zaidi ya bilioni moja na kuapa kutorudia makosa yaliyojitokeza.
Katika matamshi yake ya kwanza kuhusiana na matumizi mabaya ya taarifa binafsi za wateja zaidi ya milioni 50 kulikofanywa na kampuni ya Uingereza iliyokuwa na uhusiano na timu ya kampeni ya rais Donald Trump mwaka 2016, Zuckerberg amewaambia watumiaji wa Facebook kuwa taasisi yake “ilikuwa na wajibu wa kulinda taarifa.“
Ameahidi pia kuwa Facebook itachunguza kila programu iliyopata mwanya wa kupitia akaunti za wateja wake na kufanya uchunguzi wa kisayansi kwa kitu chochote kilichoonekana kina wasiwasi.
“Hii ilikuwa ni uvunjifu mkubwa wa matumizi ya taarifa binafsi na uaminifu, nawaomba msamaha kwa kile kilichotokea, wajibu wetu sasa ni kuhakikisha tukio hili halitokei tena.” -Zuckerberg