Leo March 30, 2018 Mbunge wa Singida, Tundu Lissu amesema ameona taarifa ya Msemaji wa Ikulu, Gerson Msigwa, kwamba ndege aina Bombardier iliyokuwa imezuiliwa Canada inakuja nchini.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram Lissu ameandika baadhi ya mambo ambayo angependa baadhi ya watu wanaodai kuwa alitumwa kipindi cha nyuma alipokuwa anazungumzia kushikiliwa kwa ndege hiyo Canada wafahamu.
Jambo la kwanza alilolisema Lissu katika ukurasa wake wa Instagrama ni kuhusu kuvunjwa kwa mkataba uliosababisha ndege kuzuiliwa “Mwaka 2003, kampuni ya Sterling Construction and Engineering Ltd. (SCEL), ilivunjiwa mkataba wake wa ujenzi wa Barabara ya Bagamoyo. Mkataba huo ulivunjwa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.”
“Baada ya kuvunjwa kwa mkataba, SCEL ilishtaki Serikali ya Tanzania kwenye Mahakama ya Usuluhishi ya International Chamber of Commerce, London. Tunaambiwa baadhi ya hearings, au zote, zilifanyikia Dar Es Salaam.” -Lissu
Jambo la pili aliloliandika Lissu ni kuhusu serikali kuamriwa kulipa kampuni “December 2009 na baadae June 2010, Arbitral Tribunal ya ICC ilitoa uamuzi kwamba Serikali ya Tanzania ilivunja mkataba wa SCEL bila uhalali wowote na kuamuru Serikali kuilipa SCEL takriban USD milioni 25, na riba ya 8% kwa mwaka kuanzia tarehe ya hukumu hadi tarehe ya malipo ya mwisho.”
“Kwa sababu tunazostahili kuambiwa na Serikali , deni la SCEL halikulipwa kwa miaka saba hadi SCEL walipoenda kwenye Supreme Court of Quebec, Canada, na kupata amri ya mahakama kuikamata Bombardier.” -Lissu
Lissu akaendelea kuandika kwamba baada ya kusikia Bombardier imekamatwa, Waziri wa Mambo ya Nje, Dr. Augustine Mahiga, na Balozi wetu Canada, Jack Zoka, walitumwa kwenda Toronto kufanya mazungumzo na SCEL juu ya namna ya kujinasua. Waziri Mahiga na Balozi Zoka waliiomba SCEL isitoe habari za Bombardier kukamatwa hadharani.
“August 18, 2017, baada ya kupata nyaraka mbali mbali zinazohusu kukamatwa kwa Bombardier, nilitoa taarifa za kukamatwa ndege hiyo kwa waandishi wa habari Courtyard Hotel, Dar Es Salaam.” -Lissu
“August 19, Kaimu Msemaji wa Serikali, Zamaradi Kawawa, alithibitisha kukamatwa kwa Bombardier ya Magufuli na kutulaumu sisi wapinzani kuwa ndio tuliosababisha ndege yetu ikamatwe Canada.” -Lissu
“Licha ya Serikali kukiri ukweli wa maneno yangu, tarehe 20 August, nilikamatwa na askari polisi walioniambia hawajui kosa langu ila wanatekeleza ‘maagizo.’ Nililazwa mahabusu hadi kesho yake nilipopelekwa kwa Mkemia Mkuu ili kupimwa mkojo. Nilipokataa kupimwa mkojo nilirudishwa mahabusu hadi kesho yake tarehe 22 August nilipoachiliwa huru bila kupelekwa mahakamani.” -Lissu
“September 7, 2017, siku kumi na moja baada ya shambulio la mabomu dhidi ya IMMA Advocates, ikawa zamu yangu kushambuliwa kwa risasi za submachine guns na ‘watu wasiojulikana.’ Nilijeruhiwa vibaya sana, lakini Mungu ni mwema sikufa. Hadi ninapoandika maneno haya, hakuna mtu hata mmoja aliyetuhumiwa au kukamatwa na kushtakiwa kwa kuhusika na shambulio hilo la kigaidi dhidi yangu.” –Lissu
Lissu akamaliza kwa kusema “Nafurahi kusikia taarifa za kuachiliwa kwa ndege yetu. Nitafurahi zaidi tukiambiwa Bombardier hiyo imeachiliwa kwa masharti gani, kwa vile tulikuwa tunadaiwa karibu USD milioni 40 zilizotokana na kuvunja mkataba na Serikali kushindwa kesi na SCEL. Hili ni swali ambalo kila mmoja wetu anatakiwa kuwahoji hawa watoa taarifa za kuachiliwa kwa Bombardier.”