Leo April 3, 2018 Mkutano wa Kumi na Moja wa Bunge umeanza na utamalizika June 29, Mjini Dodoma.
Mkutano huu utakuwa ni mahususi kwa ajili ya mijadala na kupitisha Bajeti ya Serikali pamoja na kujadili hotuba ya hali ya Uchumi wa Taifa itakayowasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango.
Aidha, Bunge hili pia litajadili utekelezaji wa Bajeti za Wizara zote kwa Mwaka wa Fedha 2017/18 na Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/19.
Shughuli nyingine zitakazofanyika katika Mkutano huu ni pamoja na kuapishwa kwa wabunge waliochaguliwa hivi karibuni kwenye uchaguzi mdogo akiwemo Mbunge wa Kinondoni, Maulid Abdallah Mtulia na mwenzake Dkt. Godwin Oloyce Mollel wa Jimbo la Siha wote wa CCM.
Mbali na viapo hivyo Bunge hilo pia litatekeleza zoezi la kuchagua wenyeviti watatu wa Bunge kutokana na wenyeviti waliokuwepo kumaliza muda wao kwa Mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge.
Bunge pia litajadili na kupitisha Azimio la Kuridhia Makubaliano ya Paris kuhusu Kuboresha Utekelezaji wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabia Nchi.