Leo April 6, 2018 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeutaka upande wa mashtaka ifikapo April 20,2018 utoe taarifa nzuri kuhusu upelelezi wa kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili vigogo wa Kampuni ya Six Telecoms Limited.
Hayo yamesemwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi kudai upelelezi haujakamilika.
Hakimu Simba amesena kuwa kesi hiyo haipaswi kuchukua miezi 12 kuanzia sasa iwe haijatolewa uamuzi.
Amesema ifike mahali ijulikane washtakiwa kama wanafungwa ama lah.
Awali Kishenyi amedai kuwa jalada la kesi hiyo lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Kwa ajili ya mapitio.
Kishenyi amedai kuwa wanaamini muda si mrefu jalada hilo lililopo kwa DPP litakuwa limekamilika na akaomba kesi hiyo ipangiwe tarehe nyingine ya kutajwa.
Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo Wakili wa utetezi Alex Mushumbusi aliuomba upande wa mashtaka tarehe ijayo waende na taarifa ya upelelezi ulipofikia.
Baadaya ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu Simba amesema hizo sababu za upande wa mashtaka zitafikia mahali zitaisha, ambapo ameahirisha kesi hiyo April 20,2018.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mhandisi na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Six telecoms, Hafidhi Shamte, Mfanyabiashara na Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Peter Noni, Mwanasheria na Mhadhiri na Mkurugenzi wa hiyo kampuni, Ringo Willy Tenga, Mkuu wa fedha wa kampuni hiyo Noel Odeny Chacha na Kampuni ya Six Telecoms Limited.
Katika kesi hiyo namba 73 ya 2017, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka sita yakiwamo ya utakatishaji wa fedha ambapo wanadaiwa kuwa kati ya January 1, 2014 na January 14,2016 Dar es Salaam, walitoza maalipo ya Mawasiliano ya simu za kimataifa chini ya kiwango cha dola 0.25 kwa dakika kwa lengo la kujipatia faida.