Leo April 11. 2018 Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Huruma Shaidi amesema kila chombo kinapaswa kufanya kazi zake kwa kuheshimiana na haipendezi kila mara zitolewe amri ambazo hazitekelezwi.
Hakimu Shaidi ameyasema hayo baada ya upande wa mashtaka kushindwa kutekeleza amri aliyoitoa ya kumpeleka mmiliki wa IPTL, Harbinder Sethi kutibiwa katika Hospital ya Taifa Muhimbili.
“Ninaamini kila chombo kinapaswa kufanya kazi zake kwa kuheshimiana, haipendezi kila wakati tutoe amri ambazo hazitekelezwi, hivyo naamuru apelekwe hospital kinyume na hapo nitatoa amri nyingine kwa mujibu wa sheria,” -Hakimu Shaidi.
Awali, Wakili wa serikali, Nassoro Katuga amedai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, pia
wameshindwa kumpeleka Sethi hospital kwa sababu maalum.
Katuga amedai kuwa miongoni mwa sababu hizo ni kwamba Sethi alihamishwa gereza kutoka Segerea kwenda Ukonga, pia mshtakiwa aliomba daktari wake kutoka Afrika Kusini awepo wakati akipatiwa matibabu.
“Kuhamishwa gereza kumechangia kuchelewesha matibabu yake, lakini pia mshtakiwa aliomba daktari wake kutoka Afrika Kusini ashiriki katika matibabu yake,”.
Hoja hizo zilipingwa na Wakili wa utetezi, Hajra Mungula akidai hazina msingi kwa sababu Sethi hakuwahi kuzungumzia suala la daktari.
Pia Mungula amedai kuwa katika gereza la Ukonga Sethi haruhusiwi kuonana na mtu yoyote hata mke wake wa ndoa.
Baada ya kutolewa hoja hizo, Hakimu Shaidi ameahirisha kesi hiyo hadi April 25,2018.
Mbali ya Sethi, mshtakiwa mwingine ni mfanyabiashara James Rugemarila ambapo kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi, utakatisha fedha na kuisababisha Serikali hasara ya USD 22, 198,544.60 na Sh.Bil 309.