Barbara Bush, mke wa Rais wa zamani wa Marekani na mwanaharakati amefariki akiwa na umri wa miaka 92, baada ya kuzidiwa kwa siku mbili na kukataa kuendelea zaidi na matibabu.
Barbara alikuwa nguzo ya kisiasa ya marais wawili wa taifa hilo mumewe George HW Bush na mtoto wake George W Bush.
Alikuwa mke wa rais kutoka 1989 hadi 1993. Mumewe aliye na umri wa miaka 93 ndiye rais aliyeishi kwa muda mrefu nchini Marekani.
Mtoto wao George alichaguliwa 2000 na kukaa madarakani kwa mihula miwili kama rais wa 43 wa Marekani.
Salaam na pole zimeendelea kumiminika kwa familia ya Bush, kufuatia msiba huo mkubwa huku miongoni mwa waliowasilisha salamu zao hizo ni pamoja na Rais wa sasa wa Marekani, Donald Trump, Rais mstaafu Bill Clinton, pamoja na viongozi wengine mbalimbali wa Marekani na duniani kwa ujumla.
Wengine ni rais mstaafu Barack Obama na Jimmy Carter ambao wamesema wanatambua mchango wa mwanamama huyo ambaye alikuwa nguzo kwa wamarekani katika kusambaza upendo na kupigiania haki ya kuondoa ujinga kwa mamilioni ya Wamarekani.
Kwa mujibu wa taarifa ya familia mwanamama huyo anatarajiwa kuzikwa siku ya Jumamosi baada ibada ya saa 5 asubuhi itakayofanyika kwenye kanisa la St. Martin Episcopal huko Houston.