Waziri wa wizara ya kilimo Dr. Charles Tizeba amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya kilimo Mhandisi Methew Mtigumwe kusitisha mkataba wa kazi wa Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania Hassan Jarufo.
Waziri Tizeba ametoa agizo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Dodoma ikiwa ni muda mchache mara baada ya kumalizika kwa dhifa ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa maghala na vihenge vya kisasa.
Akielezea sababu za kuagiza kusimamishwa kazi kwa Mkurugenzi huyo, Dr. Tizeba amesema kuwa hayo yamejili baada ya kuangalia mwenendo wa Jarufo na kutafakari jinsi zao la korosho linavyoendeshwa, ikiwa ni pamoja na kutoridhishwa na upatikanaji wa viuwatilifu kwa wakati.
Amesema ndani ya muda mfupi Wizara ya kilimo itamtangaza Kaimu Mkurugenzi wa Bodi hiyo ili kuchukua nafasi hiyo kuendeleza kusimamia sekta hiyo.
“Hizi hatua tunazochukua ni kuhakikisha kuwa wadau wakubwa wa korosho ambao ni wakulima wanaendelea kunufaika na zao lao, hivyo wakulima wasiwe na wasiwasi kwani pamoja na kuondolewa Mkurugenzi huyo lakini shughuli za serikali zitaendelea kama kawaida na maslahi yao yatasimamiwa ipasavyo” -Dr. Tizeba