Leo April 24, 2018 Naibu Waziri wa Kilimo Mary Mwanjelwa amewataka Wakuu wa Wilaya zote wanao lima Korosho kuwa na usimamizi mzuri wakati wa ugawaji wa pembejeo za zao hilo ambazo zitaanza kugawiwa mwishoni mwa mwezi May 2018 akiwataka kudhibiti ulanguzi.
Dr. Mwanjelwa amesema zao la Korosho linahujumiwa hali ambayo inatishia kulivuruga zao hilo ambalo ni la kimkakati kati ya mazao matano yanayotegemewa na Serikali ikiwa na lengo la kuliwezesha kufanya vizuri hivyo ameonya wanaojaribu kulihujumu watashughulikiwa.
Akizungumza wakati wa ziara yake Mkoani Mtwara, Naibu Waziri Mwanjelwa amesema kuwa pamoja na pembejeo kuwahi msimu huu Serikali haitaruhusu ulanguzi wowote kwenye uuzaji ili wakulima waanze maandalizi mapema.
“Hamasisheni wakulima wajue kuwa hakuna pembejeo za bure bali wanapaswa kutunza fedha zao. Bei imepangwa na Serikali hakuna ulanguzi wa aina yoyote utakaofanyika juu ya hilo kwa upande wa salfa na viwatilifu vingine.” amesema Dr. Mwanjelwa
“Atakae thubutu kuhujumu zao la Korosho naye atahujumiwa. Bei elekezi iliyopangwa na Serikali ndio itakayouzwa bila kupunguza wala kuongeza ili kuwasaidia wakulima.” Dr. Mwanjelwa