Leo April 25, 2018 Upande wa utetezi, umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa Puto (Balloon) lililopo tumboni mwa mmiliki wa IPTL, Harbinder Sethi linaweza kupasuka muda wowote kuanzia sasa na kuhatarisha maisha yake.
Hayo yameelezwa na wakili wa utetezi, Hajra Mungula mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU, Leornad Swai kueleza kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilka.
Wakili Mungula amedai kuwa April 11,2018 mahakama iliamuru Seth apelekwe Hospitali ya Taifa Muhimbili kupatiwa matibabu lakini aliishia kupata vipimo, huku akishindwa kupatiwa matibabu wala majibu yake.
“Mshtakiwa hajapatiwa majibu wala matibabu ni wiki ya pili sasa, hali yake ni mbaya, pia Puto lake linaweza kupasuka muda wowote na kuhatarisha maisha yake,” ameeleza Mungula.
Baada ya kueleza hayo, wakili Swai amedai kuwa Seth alishaonana na jopo la madaktari na ameambiwa majibu yake atapatiwa April 26,2018.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Shaidi amesema amefurahi kuona mshtakiwa amepelekwa hospitali, lakini anasisitiza kuwa apatiwe matibabu.
Pia ameutaka upande wa mashtaka kuhakikisha unakamilisha upelelezi kwa wakati ili kesi iishe, ambapo ameahirisha kesi hiyo hadi May 10,2018.
Mbali ya Sethi, mshtakiwa mwingine ni mfanyabiashara James Rugemarila ambapo kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi, utakatisha fedha na kuisababisha Serikali hasara ya USD 22, 198,544.60 na Shilingi Bilioni 309.
LIVE MAGAZETI: Zitto, Heche ‘wanusa’ kifo, Mwangwi wa Aprili 26