Razack Hamad (26) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na kosa la kuchapisha taarifa za uchochezi kupitia mtandao wake wa Telegram.
Razack ambaye ni mkazi wa Mbezi Juu DSM, amesomewa kosa hilo na wakili wa serikali, Patrick Mwita mbele ya Hakimu Mkazi, Martha Mpazi.
Wakili Mwita amedai mshtakiwa anakabiliwa na kosa moja la kuchapisha taarifa ya uchochezi kinyume na kifungu cha 53(1)(c) na 52(1)(a) cha sheria ya habari namba 12 ya mwaka 2016.
Inadaiwa mshtakiwa ametenda kosa hilo, March 9,2018 akiwa jijini Dar es Salaam alitumia mfumo wa kompyuta katika simu yake kupitia mtandao wake wa Telegram kwa kuandika;
“Nimepata wazo kwa group jingine huko tunaweza kukwepa garama pia kuandika hata kwenye kuta za wazi #April 26 Magufuli Out, pinga Dictator” Maneno ambayo yangeibua chuki kwa Watanzania.
Baada ya kueleza hayo mshtakiwa alikana shtaka hilo, ambapo Wakili Mwita amedai upelelezi bado haujakamilika, pia hana pingamizi na dhamana.
Hakimu Mpazi ametoa masharti ya kumtaka mshtakiwa kuwa na wadhamini 2 watakaosani bondi ya Sh.Mil 5.
Hata hivyo mshtakiwa ameshindwa kutimiza masharti ambapo amerudishwa rumande na kesi imeahirishwa hadi May 24,2018.