Leo May 19, 2018 Katika uwanja wa Taifa kulikuwa na sherehe ya kuwakabidhi Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC ubingwa ambapo Rais Magufuli alikuwa mgeni rasmi katika sherehe ambazo Simba kakubali kupokea ubingwa kwa kufungwa goli moja bila na Kagera Sugar.
Baada ya zoezi hilo kumalizika Uwanja wa Taifa Waziri wa Mazingira na Muungano January Makamba hajakaa kimya baada ya Simba kukubali kufungwa mbele ya Rais Magufuli ameandika katika ukurasa wake wa Instagram akihadithia story aliyohadithiwa na Mzee wake.
January Makamba alianza kwa kuhadithia akimnukuu Baba yake “Ananielezea Mzee wangu kwamba mnamo mwaka 1974, Mwalimu Nyerere alienda kukaa Chamwino Dodoma kwa muda mrefu kusimamia ujenzi wa Ikulu ya Chamwino.”
“Ndugu Moses Nnauye, wakati huo akiwa Mkuu wa Mkoa wa Singida, na mlezi na mwalimu wa kikundi maarufu cha sanaa, alipendekeza kwa Mwalimu Nyerere kwamba jioni moja kikundi kile kiende kumfanyia onyesho la utamaduni”
“Mwalimu akakubali na akafurahi. Basi kikundi kikasafiri kutoka Singida hadi Chamwino. Maandalizi makubwa, ikiwemo kuweka mataa nje kwenye bustani, yakafanywa. Saa mbili usiku Mwalimu akatoka na kukaa tayari kufurahia burudani.” January Makamba
“Mzee Nnauye aliamua waanze na kwaya, ambayo miaka yote imekuwa inakonga nyoyo za watu kwenye sherehe mbalimbali. Muongoza kwaya akasimama na kuanza kuchezesha mikono yake lakini waimbaji wakawa wanapotea, wengine wakiwa kimya wengine wakiimba sivyo kabisa.” January Makamba
“Akaanzisha mara ya pili, ikawa hivyo hivyo. Mara ya tatu, ikawa hovyo zaidi. Kila mtu akapaniki. Mwalimu akasimama, akamwambia Nnauye “Moses, hii kwaya isiyoweza kuimba siku nyingine usituite, uitazame wewe na mkeo tu”. Akaondoka zake. Hakuna aliyesema neno kwenye basi la kurudi Singida.” January Makamba
“Baada ya muda mfupi, Mwalimu akawa na ziara Singida. Jioni moja Mzee Nnauye akapanga tena onyesho la utamaduni kwa ajili ya Mwalimu pale Ikulu Ndogo Singida. Akaleta kikundi kilekile kilichoshindwa ku-perform kule Chamwino.” January Makamba
“Safari hii wale vijana walionyesha miujiza. Walifanya onyesho kwa kujiamini na kwa umahiri mkubwa. Mwalimu alifurahi sana. Akamwambia Nnauye “afadhali safari hii umeleta watu wanaojua nini wanafanya’.” January Makamba
“Nnauye akamjibu Mwalimu kwamba kile kikundi ni kilekile. Mwalimu akauliza sasa nini kilitokea Chamwino? Nnauye akamjibu “hawa vijana siku ile walikuwa hawajawahi kukuona kwa karibu hivi, na siku zote wanajua wewe ni mkali sana, sasa pale Chamwino walichokuwa wanafanya ni kukushangaa na wakashindwa ku-perform.” aliendelea kuhadithia
“Sasa leo hii hawakuwa na shida kwasababu walishakuona, wameondoa hofu na kushangaa”. Yaliyotokea uwanja wa taifa leo kwa wachezaji wa Simba (ambao walikuwa na pressure ya ku-perform mbele ya Rais Magufuli) ndio yaliyowatokea wale vijana wa kwaya wa Singida kule Chamwino. Next time watafanya miujiza” alimalizia January Makamba