Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es salaam linamshikilia Erick Francis Chilemba (30) muhudumu wa hotel ya Sleep Inn na Mkazi wa Mwananyamala kwa Kopa kwa tuhuma za kukutwa na sare za Jeshi la Polisi, silaha, cheo cha koplo, pingu na nguo nyingine inayofanana na sare za JWTZ.
Akizungumza na waandishi wa habari leo May 26 2018 Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu SACP Lazaro Mambosasa amesema walipokea taarifa kutoka kwa msiri kuwa kuna mtu mmoja anatumia sare za Jeshi la Polisi kuwakamata watu na kuwafunga pingu, kuwatishia bastola ili kufanikisha kupora mali maeneo mbalimbali ya Jiji.
Baada ya kupata taarifa hizo Jeshi la Polisi lilianza ufuatiliaji mara moja na kuweka mtego ambapo May 12 2018 majira ya saa nne usiku huko Mwenge Bamaga Polisi walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo na ameshafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.