WACHEZAJI nyota wa zamani wa Yanga, Stephen Marashi (kipa) na Mmalawi Wisdom Ndlovu (beki) wameibuka kidedea katika kesi ya madai dhidi ya klabu hiyo iliyosikilizwa na Mahakama ya Rufaa ya Tanzania.
Katika uamuzi wa rufaa yao ya kesi namba 163 ya mwaka 2013 uliosomwa jana Jumatatu mbele ya Jaji Sauda Mjasiri, Yanga imeamriwa kuwalipa nyota hao kiasi cha zaidi ya Sh106 milioni ikiwa ni gharama ya kuvunja mikataba ya wawili hao pamoja na ile ya uendeshaji wa kesi.
Rufaa hiyo ilikatwa na uongozi wa klabu hiyo uliopinga hukumu ya awali ya Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi, hivyo kuiomba mahakama ya rufaa kufanya marejeo ya hukumu hiyo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Wakili wa wachezaji hao, Dk. Ringo Tenga, alisema hata hivyo maombi ya Yanga katika mahakama ya rufaa yalikutana na kizuizi kwa vile yaliwasilishwa nje ya muda.
“Mahama imetoa hukumu kwa Yanga kuheshimu hukumu ya awali, hivyo inatakiwa kulipa kiasi hicho,” alisema wakili huyo.
Kesi hiyo ilifunguliwa na wachezaji hao miaka miwili iliyopita.
Source: Gazeti la Mwanaspoti