Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mbeya imewahukumu kifungo cha miaka 15 jela Josephat Joseph Mushi (mfanyabiashara ya samaki) na Said Omary Sisige na kuwaachia huru washtakiwa saba katika kesi ya uhujumu uchumi namba 2/2017.
Upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Mawakili wandamizi Saraji Iboru na Paul Kimweri ambapo mshtakiwa wa kwanza alikuwa akitetewa na jopo la Mawakili wanne Victor Mkumbe, Simon Mwakolo, Habib Kamru na Jackson Ngonyani ambapo mshtakiwa wa pili alikuwa akijitetea mwenyewe.
Walioachiwa huru na Hakimu Michael Mteite ni Agripa Benjamin, Pius Jacob Joseph, Said Swedi, Shaban Sankwa, Lugano Francis Mwakapala, Ibrahim Miller na Andrew Kachengo.
Akisoma hukumu hiyo Hakimu Mteite amesema Mahakama inawatia hatiani mshtakiwa wa kwanza Josephat Mushi na Said Omary katika makosa saba kosa la kwanza ni kula njama, kosa la pili kughushi, kosa la tatu kutoa maelezo ya uongo, kosa la nne kuondoa lakiri, kosa la tano kumiliki mali isiyolipiwa ushuru, kosa la sita kughushi nyaraka na kosa la saba kuitia hasara Wizara ya uvuvi.
Washtakiwa Ibrahim Miller, Lugano Mwakapala na Andrew Kachengo walikuwa wanatetewa na Mawakili Ladislaus Rwekaza, Irene Mwakyusa na Faraja Msuya.
Washtakiwa wa pili hadi wa sita walikuwa wakijiwakilisha wenyewe.
Baada ya kusikiliza upande wa mashtaka na upande wa Jamhuri mahakama imewatia hatiani washtakiwa wote wawili kutumikia kifungo cha miaka kumi na tano jela, jela miaka mitano kwa kughushi, faini dola 10000 kwa kutoa maelezo ya uongo, kulipa dola 2500 kwa kosa la kuondoa lakiri, kulipa shilingi 7,265,107/- au jela miaka mitano kwa kosa la kumiliki mali isiyolipiwa us huru, kosa la sita watatumikia miaka mitatu kwa kughushi nyaraka mbalimbali.
Hakimu Mteite amesema adhabu zote zitakwenda kwa pamoja hivyo watatumikia kifungo cha miaka kumi na tano jela na kulipa fedha kama ilivyoanishwa.