Leo June 19. 2018 Mwanasayansi wa Maabara ambaye ni mstaafu katika Serikali ya Kenya Dokta Moses Njue anashtakiwa katika mahakama ya Meru nchini Kenya kwa kosa la kuiba viungo vya maiti za Binadamu.
Mwendesha mashtaka wa kesi hiyo Claire Murithi amemshutumu Dokta Njue kwa kuiba moyo wa Polisi wa zamani wa nchi hiyo Benedict Karau huku akimshutumu pia kuharibu ushahidi wa kesi hiyo.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa Mahakamani March 12, 2015 yalieleza kuwa Dokta Njue ambaye ndiye aliekuwa kiongozi mkuu wa uchunguzi wa maiti katika hospitali ya Consolatha aliiba moyo wa Polisi huyo kabla haujapelekwa katika shule kwa ajili ya Wanafunzi kufundishiwa.
Katika kesi hiyo ambayo imeendelea kusikilizwa , Dokta Njue amekana mashtaka hayo huku mahakama ikimtaka kuweka dhamana ya zaidi ya shilingi Milioni 45 za Kitanzania.
Hata hivyo wakili wa Dokta Njue aliiomba mahakama kupunguza dhamana hiyo kwa kile alichokidai kuwa mteja wake ni mtumishi wa umma ambapo baadae mahakama ilimtaka Dokta Njue kutoa zaidi ya Milioni 11 za Kitanzania kama dhamana.